MASHINDANO ya Kombe la Mapinduzi kwa mchezo wa Netiboli ya Afrika Mashariki na Kati yanatarajiwa kufanyika Januari 6 mwakani.
Mashindano hayo ambayo yatashirikisha timu za wanawake na wanaume yameandaliwa na Chama Cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA), yatakuwa yakichezwa katika kiwanja cha Gymkhana mjini Unguja.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho Rahima Bakari amesema kuwa tayari timu zote ambazo zitashiriki michuano hiyo zimeshathibitisha ushiriki wao.
Alisema kuwa mashinadano ahayo ambayo yatasimamiwa na kamati ya kombe la Mapinduzi yatakuwa yakichezwa kwa mtindo wa ligi.
Alizitaja nchi zitakazoshiriki michuano hiyo ni Zambia, Zimambabwe, Msumbiji, Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania.
Alifahamisha kuwa maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo yanaendelea vizuri na timu zote hizo zinatarjiwa kuwasili Januari 5 mwakani, ambayo kila moja imeagizwa ilete mwamuzi wake.
Hata hivyo alisema kuwa timu zitakazoshiriki zitajigharamia usafiri wa kuja na Kurudi kwao wakati usafiri wa ndani, malazi, chakula na mambo mengine yatagharamiwa na kamati ya Kombe la Mapinduzi huku akisema
chama nacho kitasaidia baadhi ya mambo.
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kuadhimisha Mapinduzi ya Matukufu ya Zanzibar ambayo mwakani yanatimiza miaka 48 lakini kwa mchezo wa Netiboli hii ni mara yake ya
kwanza kufanyika.
Kilele cha mashindano hayo hufanyika Januari 12 ya kila mwaka, ambapo bingwa mtetezi katika mchezo wa soka ni Simba kutoka Jijijini Dar Es Salaam.
No comments:
Post a Comment