Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Dokta Islam Seif akibadilishana mkataba wa zabuni ya kusambaza mabomba ya maji katika kijiji cha Nungwi na mwakilishi wa kampuni ya DPI Simba Limited ya Dar Es Salaam Bwana Abdulrahman Abuu Abdul. (Picha na Salmin Said OMKR).
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar leo imetiliana saini na kapuni ya DPI Simba Limited ya Dar Es Salaam, mkataba wa zabuni ya kusambaza mabomba kwa ajili ya mradi wa maji katika kijiji cha Nungwi.
Kwa upande wa serikali mkataba huo umesainiwa na Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dokta Islam Seif ambapo kampuni hiyo imewakilishwa na meneja mauzo Bwana Abdulrahman Abuu Abdul.
Akizungumza mara baada ya utiaji saini huo uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Migombani, Naibu Katibu Mkuu Dokta Islam Seif amesema hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Amewataka wananchi wa Nungwi kushirikiana na wadau wengine wa mradi huo wa majaribio ili uweze kukamilika kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
Amesema mafanikio ya mradi huo yatakuwa kichocheo cha kuibuka kwa miradi mengine ambayo ni muhimu katika maendeleo ya wananchi hasa katika maeneo ya vijijini.
Nae mwakilishi wa kampuni ya DPI Simba Limited Bwana Abdulrahman Abuu Abdul amesema kampuni yake inakusudia kukamilisha kazi ya usambaji wa mabomba katika kipindi cha wiki mbili walichokubaliana.
Mapema akitoa ufafanuzi wa mdari huo, mkurugenzi wa Mazingira Zanzibar Bwana Sheha Mjaja Juma amesema mradi huo utakapokamilika utaweza kuwaondoshea tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama wananchi wa kijiji cha Nungwi ambao wamekuwa wakiikosa huduma hiyo muhimu kwa muda mrefu sasa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyopelekea visima vyao kuingia maji ya chumvi.
Mradi huo unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kupitia Idara ya mazingira, pamoja na mambo mengine unahusisha uchimbaji wa kisima katika eneo la Kilimani, ununuzi wa mabomba na trasfoma pamoja na kununua tangi jipya la maji.
Jumla ya shilingi milioni 535 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya mradi huo unaotarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Hassan Hamad (OMKR).
No comments:
Post a Comment