Habari za Punde

NORWAY ITAENDELEA KUISAIDIA ZANZIBAR

Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Igun Klepsvik huko Wete Pemba. Picha na Salmin Said (OMKR)

Khamis Haji,

NORWAY imesema itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kudumisha umoja na mshikamano uliopatikana baada ya kufikiwa maridhiano ya kisiasa, kwa vile hali hiyo imeonesha dalili nzuri za kukuza maendeleo ya wananchi katika kipindi cha mwaka mmoja chini ya serikali ya umoja wa kitaifa.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Igunn Klepsvik wakati alipofanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad huko nyumba ya serikali Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba. Balozi Klepsvik alisema yeye mwenyewe binafsi amefurahishwa namna wananchi wa Zanzibar wanavyodumisha umoja na kuiunga mkono serikali yao, baada ya kuzika tafauti zilizokuwepo kwasababu ya itikadi za kisiasa.


Balozi huyo alitoa mfano wa mshikano walioonesha wananchi wakati wa maafa ya kuzama kwa meli mwezi Septemba mwaka huu.
Alisema tathmini yake ya mwaka mmoja chini ya mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa, Zanzibar inaendelea vizuri kusimamia mipango ya maendeleo, hali ambayo inatoa ishara za kupatikana mafanikio katika kuwapunguzia wananchi hali za umasikini, hivyo itaendelea kutoa misaada kuona mikakati iliyoandaliwa inafanikiwa.

“Norway inaunga mkono juhudi za kuendeleza maridhiano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar, na ndio maana tumeelekeza nguvu kubwa kufadhili uendelezwaji wa maridhiano haya, ikiwemo kuhamasisha wananchi umuhimu wa maridhiano kupitia matamasha na burudani, ambayo ndio njia sahihi ya kufikisha ujumbe”, alisema Balozi wa Norway.

Katika mazungumz hayo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alisema miongozi mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya mwaka mmoja wa serikali ya umoja wa kitaifa ni kuwepo uwazi serikalini na wananchi kupata uhuru mkubwa wa kutoa na kupokea taarifa.

Alitoa mfano Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein Novemba 3 mwaka huu alifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo alieleza mambo mbali mbali yanayogusa wananchi wa Zanzibar na kutoa uhuru wa kuulizwa maswali yoyote na akaweza kuyatolea maelezo kwa kina.

Mbali na hayo, alisema vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa zake kwa uhuru mkubwa na wananchi kivitumia kueleza maoni na kero zao, jambo ambalo huko nyuma halikuwepo na kulikuwa na lawama baadhi ya vyoho vilinyimwa uhuru huo. Alisema kwa upande wa kuimarisha hali za maisha ya wananchi, katika kipindi hicho cha mwaka mmoja serikali imefanikiwa uinua hali za wafanyakazi serikalini, baada ya kufanikiwa kupandisha mishahara kwa asilimia 25 na kutoa nyongeza kwa wafanyakazi wanaostahili.
Vile vile, Maalim Seif alisema mipango mizuri imetandikwa kukuza maendeleo ya wavuvi pamoja na wakulima, wakiwemo wa zao la karafuu, ili kuinua hali zao za kimaisha.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.