SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho amesema Zanzibar ina fursa nzuri ya kujifunza jinsi China ilivyoweza kufikia hatua kubwa za kimaendeleo.
Spika Kificho alisema hayo jana katika ukumbi wa wizara ya Biashara ya China uliopo mjini Beijing, kwenye ufunguzi wa mafunzo ya wiki mbili yanayohusu uimarishaji wa uwekezaji wa vitega uchumi inayowahusisha mawaziri na baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali ya Zanzibar.
Alisema China imepiga hatua kubwa kwenye eneo la uwekezaji, fursa ambayo inaweza kuigwa na Zanzibar katika kuchapuza uwekezaji hali itakayowezesha kukuza na kustawisha uchumi wake.
Spika Kificho alisema Zanzibar inaamini uwekezaji wa vitega uchumi na kufungua milango ya kibishara ni miongoni mwa eneo ambalo linaweza kuvikomboa visiwa hivyo na kuondokana na umasikini na kuinua hali za maisha ya wananchi wake.
"Ujumbe wa Zanzibar umekuja China kujifunza na kujionea wenzetu mlivyoweza kufanikiwa kenye nyanja hii, tukiamini inaweza kuwa njia nzuri na sisi kufanikiwa na kusonga mbele katika hatua za kimaendeleo", alisema Kificho.
Aidha alisema China ni mshirika mkubwa na muhimu wa maendeleo ya Zanzibar, kwani misaada inaotolewa na nchi hiyo imekuwa ikisaidia mipango ya Zanzibar ya kuondokana na umasikini.
Akitoa mfano alisema ujenzi unaondelea wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Zanzibar, mradi wa E goverent, afya, elimu na miundombinu ni ushahidi wa hayo.
Akizungumzia uchumi wa Zanzibar, alisema pamoja na kuwepo kwa mitikisiko na midororo ya uchumi duniani, Zanzibar imekuwa ikifanya vyema kwani uchumi wake umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 6.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Biashara wa China, LI Jinzao, alisema nchi yake itaendelea kuwa mshirika kwa nchi za kiafrika ikiwemo Tanzania na kwamba itaendelea kuzisaidia nchi hizo.
Alisema maendeleo yaliyopatikana na China katika miaka ya hivi karibuni yanatokana na kujiiingia kikamilifu na kuzifuata sera za uwekezaji vitega uchumini na maeneo tengefu.
"Tumekuwa katika hali nzuri ya kukua kwa uchimi wetu, hivi sasa tunashikilia nafasi ya pili duniani kasi tunataka kuiendeleza lakini pia kuwafundisha wenzetu njia tulizopita ili nao wafike", alisema Naibu huyo
Aidha alifahamisha kuwa sera za mapinduzi ya kiuchumi za China zitaendelea kuimarisha ili taifa hilo liweze kupiga hatua na wananchi wake waishi maisha mazuri.
Ufunguzi wa mkutano huo, ulihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Omar Ramadhan Mapuri, Balozi Mdogo wa China aliye Chen Qiman, Rais wa kituo cha kimataifa cha Biashara cha China Zou Chuanming.
Baadhi ya mawaziri wa Zanzibar wanaoshiriki ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii Wanawake na Watoto Zainab Omar Mohammed, Waziri wa Ardhi Maji Makaazi na Nishati, Ali Juma Shamuhuna, Waziri wa Biashara na Masoko Nassor Ahmed Mazrui.
Wengine ni Juma Duni Haji waziri wa Afya, Said Ali Mbarouk waziri wa Mifugo na Uvuvi, waziri wa Sheria na Katiba Aboubakari Khamis Bakary, waziri wa Kazi uwezeshaji wananchi Kiuchum Harouna Ali Suleiman.
No comments:
Post a Comment