ILI kuwa na Zanzibar bora yenye na maadili mema jamii haina budi kukumbatia malezi yenye misingi itokanayo na mafundisho ya dini ya kiislam.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Haji Mwadini Makame alipokuwa akizungumza na waumini wa dini ya kiislam waliohudhuria sherehe za kuukaribisha mwaka mpya wa kiislam zilizofanyika mwishoni mwa wiki kijijini Potoa Wilaya ya kaskazini “A” Unguja.
Alisema kutokana na jamii ya Wazanzibari kwa kiasi kikubwa kukumbwa na wigo wa maadili yanayoingizwa na wageni, maadili ambayo hayaendani na dini yao ndio sababu kubwa ya mporomoko wa maadili visiwani humo.
Alisema kitendo cha Wazanzibari kuiga silka na utamaduni usio na misingi ya uislam ni kuijengea sifa mbaya Zanzibar na pia ni kuvitayarishia malezi mabovu vizazi vijavyo ambavyo ndio warithi na waendelezaji wa taifa hilo.
“Ndugu zangu Wazanzibari tujitahidi kulea vijana wetu katika malezi mema, kwani hakuna maadili mema bila ya maadili yatakayokuwa na malezi ya kiislam,” alisema Haji.
Aidha alisema Serikali ya Zanzibar inathamini shughuli za kiislam na kwamba ipo pamoja na Waislam bega kwa bega katika kuhakikisha uislam unastawi na kusaidia kwa namna moja katika ujenzi wa Zanzibar mpya yenye neema tele.
Sherehe hizo zilizopendeza kutokana na shamra shamra za aina yake, na kuhudhuriwa na Waislam wasiopungua 3500 kutoka ndani na nje ya nchi, zilitanguliwa na mashindano ya kuhifadhi Qur-an kwa watoto na maandamano ya hisani kabla ya michezo kama kuvuta kamba na gwarige lenye taathira halisi ya jeshi la kiislam kuchukua nafasi yake.
Mapema akiwasilisha risala ya wanakijiji mbele ya mgeni rasmi, Idd Zubeir Idd alisema changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa fedha za kuendeshea gharama za sherehe hizo zinazofanyika na kukua kila mwaka.
Sherehe kama hizi za kusherehekea mwaka mpya wa Kiislam katika kijiji cha Potoa kilichoko Kaskazini mwa Unguja, zimefanyika kwa mwaka wa kumi mfululizo sasa tangu zilipoasisiwa mwaka 2002 na zimekuwa zikilinganishwa kama ni za pili kwa ukubwa badala ya zile zinazofanyika kitaifa mjini Zanzibar.
No comments:
Post a Comment