Habari za Punde

Malaria Yainyemelea Upya Zanzibar

Kesi nyingi zaripotiwa wilaya saba Januari

Na Salum Vuai, Maelezo

UGONJWA wa malaria katika baadhi ya wilaya za Unguja na Pemba, umeripotiwa kuibuka upya baada ya awali kupungua kwa asilimia kubwa nchini kote.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake Mwanakwerekwe, Kaimu Mdhamini wa Kitengo cha Kudhibiti Malaria Zanzibar (ZMCP), Mwinyi Issa Mselem, amesema imegundulika kuwa ongezeko hilo limebainika wiki chache tangu kuanza kwa mwaka huu.

Amefahamisha kuwa, huenda hali hiyo imetokana na kuzaliana kwa wingi mbu wanaosababisha malaria katika msimu wa mvua za vuli uliomalizika hivi karibuni.


"Tumegundua kuwepo ongezeko kubwa la malaria kulinganisha na miaka mitatu iliyopita, ambapo Zanzibar ilifanikiwa sana katika vita vya kutokomeza maradhi hayo", alieleza ofisa huyo.

Alisema kwa mujibu wa taarifa zinazowasilishwa kutoka katika vituo mbalimbali vya afya vya serikali Unguja na Pemba, kati ya kesi sita na 26 za watu waliobainika na ugonjwa huo ziliripotiwa ndani ya wiki ya kwanza ya mwezi Januari, mwaka huu katika maeneo tafauti visiwani humu.

Aliyataja maeneo hayo kwa Unguja, kuwa ni Jendele Wilaya ya Kati, Kidoti na Kivunge Wilaya ya Kaskazini A, ambapo kwa Wilaya ya Kaskazini B, vijiji vya Donge Mchangani na Vijibweni, ndivyo vilivyoripotiwa kurudi tena kwa maradhi hayo.

Aidha aliitaja shehiya ya Mkele katika Wilaya ya Mjini, na Wilaya ya Micheweni Pemba, ambapo alisema ugonjwa huo umezuka upya katika vijiji vya Mkia wa ng'ombe, Msuka, Tundauwa, Konde, Makangale, Shumba viamboni na Tumbe.

Kwa upande wa Wilaya ya Mkoani, Mselem alisema vijiji vilivyoathirika ni Uondwe, Vumba na Njuguni wakati katika Wilaya ya Wete, kijiji cha Wambaa pekee kimeripotiwa kurudi kwa ugonjwa huo.

Aliwatahadharisha wananchi kutojisahau kwa mafanikio yaliyopatikana, kwani mbu wa malaria bado wanaendelea kuzaliana, licha ya jitihada za serikali kupitia kitengo chake, kuendeleza mapambano dhidi ya maradhi hayo.

"Kuna kila dalili kuwa, mafanikio tuliyopata miaka mitatu iliyopita, yamewafanya wananchi wajisahau na kupuuza umuhimu wa kujikinga na maradhi hayo kwa kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa, au kutokwenda hospitali wanapojihisi dalili za malaria", alifafanua.

Alisema kwa mazingira ya visiwa vya Zanzibar, mbu wa aina zote hawatalazika kzualiwa, kwani mbali ya Wizara ya Afya kuwa na mpango wa kupiga dawa majumbani, mikono ya binadamu inachangia sana kuzalisha mbu kwa njia tafauti ikiwemo uchafu wa mazingira pamoja na kuacha maji yakituwama katika maeneo yao.

Akizungumzia mipango ya kitengo chake kwa mwaka huu,Mselem alisema mwezi Februari, zoezi la kupiga dawa ya kuulia mbu katika maeneo sugu kwa maradhi hayo litaanza, sambamba na ugawaji wa vyandarua nchi nzima.

Alisema takriban vyandarua laki nane vitasambazwa nchi nzima, ambapo kila familia inatarajiwa kufaidika, huku akisema sehemu kuwa ya vyandarua hivyo, imetolewa msaada kutoka kwa mtoto wa Malkia wa Uingereza aliyefanya ziara hapa nchini miezi kadhaa iliyopita.

Hata hivyo, alisema katika kupiga dawa mara hii, kitengo chake kitatumia dawa mpya baada ya ile ya awali kuonekana kuwa sugu kwa mbu waenezao malaria.

Katika mwaka 2011, Zanzibar ilifanikiwa saba kupunguza kasi ya ugonjwa wa malaria hadi kufikia asilimia 0.06, na kuwa nchi ya kupigiwa mfano barani Afrika na duniani kwa jumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.