47, 548 waajiriwa mwaka jana Zanzibar
Na Mwashamba Juma
WIZARA ya Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika inakusudia kutoa ajira 3,500 kupitia vyama vya ushirika.
Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa wizara hiyo huko ofisini kwake Mwanakwerekwe.
Waziri Haroun alisema katika kuvipa uwezo wa kiuendeshaji vyama vya ushirika wizara yake inatarajia kuanzisha mfuko mpya wa uwezeshaji wananchi kiuchumi mwezi Aprili mwaka huu, ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Kuzinduliwa kwa mfuko huo kunakusudia kupunguza msururu mkubwa wa uhaba wa ajira kufuatia zaidi ya wazanzibari 17,000 wakiwa hawana ajira, hivyo kupitia mfuko huo ambao unakusudia kupunguza tatizo hilo.
Akizungumzia sheria za kazi kwa wafanyakazi waziri Haroun alisema, wizara yake inasimamia kikamilifu sheria za kazi hasa kwa waajiri wanao wanyanyasa wajiriwa wao.
Alisema serikali kupitia wizara yake tayari imewafutia vibali vya kazi pamoja na mikataba yao, baadhi ya waajiri katika ngazi ya uongozi wa juu kwa baadhi ya mahoteli yakiwemo Neptune, Lagema ya Nungwi, Dolphin, African House na Dream of Zanzibar.
Akizungumzia ajira za nje waziri huyo alisema kuwa zitapatikana kwa utaratibu maalum wa serikali ambapo kupitia wizara yake kwa makubaliano ya serikali ya Oman Wazanzibari watapelekwa kihalali nchini humo pamoja na kuwapatia ajira zenye heshima na staha.
Kwa upande wa ajira za ndani waziri alisema zaidi ya Wazanzibari 47,548 waliajiriwa mwaka jana kupitia sekta rasmi ambapo watumishi wa serikali 31433 waliajiriwa na wa sekta binafsi 13148 na watumishi 4871 sawa na asilimia mbili wameongezeka kwa mwaka huu.
Waziri huyo alifahamisha kuwa wizara yake inatoa fursa maalum kwa wajasiriamali ambapo imeanzisha soko la Jumapili ‘Sunday Market’ kwa ajili ya bidhaa za wajasiriamali wote.
Alisema kwa mashirikiano mazuri baina ya wizara yake na manispaa pamoja na afisi ya mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi wamejipanga vizuri katika kusimamia uendelezwaji mzuri wa soko hilo.
Aidha aliwataka wafanyabiashara wadogo wadogo na wa juakali kuitumia fursa ya soko la Jumapili kwa kufanya biashara zao siku hiyo.
Nae mratibu Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kwa Wazanzibari waishio nje ya nchi (diaspora) Hassan Khamis Hafidh, aliitaka wizara hiyo kwa kushirikiana na idara yake pamoja na umoja wa Wazanzibari waishio nje ya nchi, kuwatumia Wazanzibari hao katika kuchangia maendeleo ya nchi.
Alisema kuwa wao ni rasilimali ya nchi pia ni mawakala wazuri watakaozishughulikia haki na sheria wa Wazanzibari wanaofanyishwa kazi za majumbani na kutotendewa haki wakiwa nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment