BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imemtunuku mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis sarafu maalum ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania bara kutokana na mchango wake wa kulitumikia taifa.
Akikabidhi sarafu hiyo Mkurugenzi wa Benki kuu ya Tawi la Zanzibar, Joseph Samwel Muhando alisema kuwa sarafu hiyo yenye thamani ya shilingi 50,000 iliyotolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika ni maalum kwa ajili ya kuwatunuku na kuwaenzi viongozi mbali mbali wa kitaifa.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa, Abdalla Mwinyi ni miongoni mwa viongozi wanaostahiki kupewa tunzo hiyo kutokana na umahiri wake katika kutekeleza majukumu yake na mashirikiano mazuri aliyoyatoa kwa uongozi wa benki hiyo.
Alisema kuwa sarafu hiyo ya medali ya fedha kwa kiwango cha asilimia 92.5 na uzito wa gramu 12 yenye nembo ya picha ya Mwalimu Nyerere na ramani ya Tanzania na kwa upande wa pili kuna nembo ya Jamuhuri ya Muungano.
Alisema haitokuwa katika mzunguko wa matumizi ya kawaida na itakuwa ni kumbukumbu ya kuwaenzi viongozi katika kipindi cha uongozi wao na baada ya kustaafu utumishi wa umma.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi aliushukuru uongozi wa benki hiyo kwa kuthamini mchango wake kwa taifa na kuweza kumtunuku tunzo hiyo yenye thamani kubwa.
Aidha aliiomba benki hiyo kuwaelimisha wakulima wa karafuu juu ya umuhimu wa kuhifadhi fedha zao benki sambamba na kuanzisha ‘mobile bank’ katika maeneo mbali mbali ili kuwasogezea kwa ukaribu wananchi huduma za kibenki.
Alisema katika msimu wa karafuu wazalishaji wa zao hilo hasa katika kisiwa cha Pemba wamekuwa wakipata fedha nyingi lakini bado hawajawa na muamko wa kuweka fedha zao benki na badala yake wanazihifadhi majumbani.
Mkuu huyo alisema kuwa jamii pia inahitaji kuelimishwa juu ya kupanda na kushuka kwa thamani ya sarafu hivyo kuiomba BoT kutoa taaluma kwa wananchi hasa vijijini na wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo wajasiriamali.
Hata hivyo alifahamisha kuwa haitoshi masuala ya kifedha na huduma nyengine za kibenki kufahamika na wafanyabiashara wakubwa pekee, na kwamba hali hiyo inawakosesha fursa kufaidika na huduma mbali mbali za kifedha kwa wananchi wa kipato cha chini.
No comments:
Post a Comment