JUMUIYA ya Al Yamin, iko mbioni kujenga ukumbi wa kisasa wa mikutano wa kimataifa, utakaokuwa na daraja ya nyota tano.
Azma hiyo inayopangwa kutekelezwa baada ya miaka miwili ijayo, inalenga kuiimarisha zaidi jumuiya hiyo, na kuiongezea uwezo wa kutekeleza majukumu yake.
Hayo yalifahamika katika hafla ya ufunguzi wa ukumbi mpya wa Baytul Yamin uliopo kwenye makao makuu ya jumuiya hiyo hapo Funguni mjini Zanzibar.
Hafla hiyo iliyoambatana na maulid ya kuadhimisha uzawa wa kiongozi wa Waislamu Mtume Muhammad (SAW), ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kidini, masheikh, maulamaa kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis.
Akizungumzia ujenzi wa ukumbi huo, Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Mohammed Al Sheikh, alisema ni azma ya jumuiya ya Al Yamin, kukamilisha ghorofa mbili zilizobaki katika jengo hilo, huku pia ikijipanga kuwa na ukumbi wa kimataifa wa nyota tano, utakaotumika kwa mikutano mbalimbali mikubwa.
Al Sheikh, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi huo, alisema, kazi za kukamilisha ukumbi huo wa pili katika jengo hilo la Baytul Yamin, ilianza Aprili 28, mwaka jana, kutokana na msukumo wa mwanachama wa jumuiya hiyo Salum Bakhresa.
"Baada ya kuona tunasuasua, mtoto wetu huyu aliwafuata wazee wa kamati kuu kueleza azma yake ya kutaka kujenga na kuwa msimamizi wa ujenzi huu, na kamati ikampa baraka na kumtaka aanze bila kusita", alifahamisha Al Sheikh.
Alieleza kuwa, ujenzi wa ukumbi huo umegharimu shilingi milioni 95 hadi kukamilika kwake, ambazo zimetokana na misaada, kutoka kwa wahisani mbalimbali, mikopo pamoja na mfuko wa jumuiya.
Kwa niaba ya jumuiya hiyo, alitoa shukurani kwa wote waliochangia kwa hali na mali, pamoja na kutoa ushauri juu ya kumaliza kazi ya ujenzi hadi kufunguliwa hiyo juzi.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuishukuru jumuiya ya Yemen ya mjini Dar es Salaam, kwa kuwakopesha fedha ili waweze kumaliza kwa haraka ujenzi huo.
Kwa upande mwengine, hafla ya maulidi iliyofanyika ukumbini hapo ilichangamsha hadhira, ambapo baadae Sheikh Sameer Zulfiqar, alitoa nasaha kwa waumini waliohudhuria.
Sheikh Zulfiqar aliwakumbusha waumini juu ya haja ya kumpenda Mtume Muhammed (S.A.W) kwa dhati, kwa kufuata mwenendo wake ili wapate manusura duniani na Akhera.
Alisema haitoshi kwa waumini kujigamba kuwa wana mapenzi kwa kiongozi wao huyo, lakini tabia na vitendo vyao vikawa vinakwenda kinyume na alivyokuwa mtume (S.A.W).
Miongoni mwa waalikwa mashuhuri katika hafla hiyo, alikuwa Sheikh Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Sheikh L-Hadi, Mufti Mkuu wa Zanzibar aliyewakilishwa na Naibu Kadhi Sheikh Khamis Haji, pamoja na maulamaa wengine mbalimbali.
No comments:
Post a Comment