Habari za Punde

Kupanga Bei kwa Dola ni Kuvunja Sheria - Mkulo

Na Kunze Mswanyama, DODOMA

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo amesema ni kinyume na sheria kwa wafanyabiashara kupanga bei ya bidhaa zao kwa kutumia dola za Marekani.

Mkulo alieleza hayo alipokuwa akitoa tathmini ya hali ya uchumi kwenye semina ya Wabunge iliyofanyika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.

Alisema kupanga bidhaa na kulazimisha kulipwa dola za Marekani ni kosa kwa mujibu wa kifungu nambari 26 cha sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, sura ya 197.


Waziri huyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa kwenye vyombo vya sheria pale watakapowabaini wafanyabiashara wakilazimisha kulipwa fedha za kigeni baada ya kutoa ama kuuza huduma.

Alisema mara nyingi wafanyabiashara wa namna hiyo, hulazimisha kulipwa fedha za kigeni kwa kuhofia kuporomoka thamani ya shilingi na kulinda biashara zao.

Alisema kufuatia hatua zilizochukuliwa na serikali, shilingi imeanza kuimarika thamani yake tangu mwezi Januari mwaka huu.

“Sehemu kubwa ya kupungua kwa thamani ya shilingi ya Tanzania imetokana na mfumuko wa bei kati ya Tanzania na nchi tunazofanya nazo biashara na tofauti kati ya mahitaji ya bidhaa kutoka nje na mapato ya mauzo yetu nje”, alisema Mkulo.

Waziri huyo alisema Tanzania inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi hasa kutokana na kutegemea kuingiza vitu zaidi kuliko kusafirisha nje.

Aidha alisema tatizo jengine linalotishia hali ya uchumi wa Tanzania ni madeni makubwa yanayozikabili nchi za Ulaya hasa Ugiriki mahitaji ya dola ya Marekani yameongezeka sana na hivyo kusababisha sarafu zote kubwa duniani kuporomoka dhidi ya dola ya kimarekani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.