ALIYEKUWA kocha wa Miembeni United, Salim Bausi amelilalamikia Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFA) na lile la Tanzania (TFF) kwa kukalia kimya suala la upangaji matokeo ya mechi ya Simba na Miembeni katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi yaliyomalizika Januari 12.
Bausi alisema kuna uwezekano mkubwa TFF na ZFA wamefungwa mdomo kwa kupewa rushwa kutokana na hali halisi ya sakata hilo linavyopigwa danadana tofauti na hapo awali.
Bausi ambaye aliamua kujiuzulu kwa madai ya kuambiwa akubali timu yake ifungwe na Simba katika mechi ya hatua ya makundi katika mashindano hayo alisema awali viongozi wa ZFA walikuwa wakimuunga mkono, lakini sasa hakuna hatua zozote wanazochukua hali inayompa wasiwasi.
"Unajua wakati mchezo ukiendelea na matokeo yakiwa sare ya mabao 3-3 huku wakati wowote filimbi ingepulizwa kumalizika kwa mpira, aliyekuwa kiongozi wangu wakati huo, Amani Makungu alitoka jukwaani na kunifuata na kunitaka niwambie vijana wangu waachie ili Simba ifunge bao la ushindi.
"Kwa kweli ile hali ilinishangaza, mimi kama kocha sikukubaliana naye ndipo akamfuta msaidizi wangu, baada ya hapo aliitwa Uhuru Suleiman wa Simba kama anapewa maji na kuambiwa atapatiwa pasi na yeye kwenda kufunga huku tayari wachezaji wa Miembeni wakiwa 'wamesetiwa'," alisema kocha huyo ambaye sasa anafundisha Bandari inayoshiriki ligi daraja la kwanza.
Bausi alisema katika mechi hiyo Simba ilionyesha uwezo mdogo na ilikuwa ikiyaaga mashindano hayo katika hatua ya makundi licha ya kwamba walijaribu kuibeba, lakini kutokana na uwezo mdogo haikuweza kusonga mbele.
"Hii inadhihirisha wazi kuwa ZFA na TFF ambao ndiyo wenye dhamana ya kusimamia soka hapa nchini wamehongwa sababu haiwezekani kulifumbia macho suala hili wakati ni kitendo kilichodhihirika wazi," alisema.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa ZFA, Masoud Attai alishindwa kulizungumzia suala hilo na kudai kuwa mwenye uwezo wa kulizungumzia ni yeye mwenyewe Bausi.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:
Post a Comment