Habari za Punde

CCM Isirejee Makosa ya 2010 – Samia

Na Asya Hassan

CHAMA cha Mapinduzi kimesema kitahakikisha hakitorejea kufanya makosa ambayo yalifanyika katika uchaguzi uliopita katika taratibu za uendeshaji ili kisiweze kupoteza majimbo yake.

Hayo yameelezwa na Mjumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho katika maadhimisho ya kutimiza miaka 35 ya chama hicho yaliofanyika uwanja wa Hamburu Nungwi Mkoa wa Kaskazini A.


Alisema uchaguzi uliopita, chama hicho kilikosea na kupoteza baadhi ya majimbo, hivyo anaamini kuwa makosa kama hayo hayatofanyika tena kwa kufuata matakwa ya wananchi kwa kumchaguwa kiongozi wanaemuhitaji.

Samia alitoa wito kwa wanachama wenye sifa wajitokeze kwa wingi katika uchukuwaji wa fomu ili waweze kugombea nafasi zilizopo katika chama ifikapo mwishoni mwa mwaka.

Alisema wanachama watakaochaguliwa katika uchaguzi huo ndio watakaoweza kushiriki katika uchaguzi mkuu ifikapo mwaka 2015 hivyo, wananchama wahakikishe wanamteua mtu mwenye uwezo na hekima katika kukifanyia kazi chama.

Mjumbe huyo aliwataka vijana kuwa na msimamo katika kusimamia maendeleo ya chama na kulijenga Taifa ili chama kiweze kusimama imara katika uongozi wake.

Hata hivyo, aliwataka viongozi wa chama cha Mapinduzi wawe na msimamo wa pamoja katika kupambana na propaganda zinazoanzishwa na vyama vya upinzani na kujibu hoja na sio kukaa kimya kwani hali kama hiyo inaweza kusababisha vikwazo miongoni mwa wananchi.

Samia alisema viongozi wa majimbo akiwemo Mbunge na Mwakilishi wakae pamoja na wananchi ili waweze kutatua kero za wananchi ili katika chaguzi zijazo wananchi wawe wametatuliwa matatizo yao mbali mbali.

Katika hafla hiyo, Mjumbe huyo wa kamati kuu ya CCM alichangia shilingi 500,000 kwa vijana walioshiriki Sarakasi na kukabidhi pea 50 za viatu kwa vijana walioshiriki matembezi ya mshikamano.

Nae Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini, Katerina Pita akitoa ujumbe wa maadhimisho ya miaka 35 alisema una malengo ya kuhamasisha wanaCCM kugombea nafasi za uongozi,kupiga vita rushwa na kutetea na kusimamia Muungano.

Alisema kuwa pia wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika Mkoa wao kama vile migogoro ya ardhi,ubakaji na ulipaji wa ada kwa wanachama.

Maadhimisho hayo yaliyoshirikisha majimbo manane kutoka Mkoa huo pia yamepata fursa kwa kuchukua fomu wanachama wapya wa CCM waliojiunga 350 na wanachama wa Jumuiya za vijana na wazazi waliochukua fomu za kujiunga ni 250.

1 comment:

  1. Usijaidanganye wewe mnafiki Samia,Nungwi sio ile ya Zamani,Wanungwi tuko macho hatuja lala,tumenyonyoka wichwa kwa kubeba madumu ya maji tangu mapinduzi ya 64,huna cha kutueleza.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.