Habari za Punde

Waislamu Watakiwa Kuimarisha Umoja

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein juzi alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya sherehe ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) na kuungana na waislamu wote duniani katika kuadhimisha siku hiyo adhimu ambapo waislamu wametakiwa kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao.

Maadhimisho hayo, ambayo kitaifa yalifanyika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali, vyama vya siasa na viongozi wa dini ya kiislamu akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Qabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji pamoja na viongozi wengine.


Akisoma khutba, Ustadhi Hemed Ahmed Chum kutoka chuo cha kiislamu alieleza kuwa wajibu wa umma wa kiislamu ni kushirikiana ili kufanikisha maslahi yao ya kidunia na akhera pamoja na kuondosha matatizo yao kwa kushikamana na kamba ya Allah.

Alisema haramu kwao kutengana, kufitiniana, kutokuwajibika katika dhamana zao na kughafilika kwa namna yoyote ile.

Alisema kila muislamu kwa kila dhamana aliyoibeba akiwa ni baba, mama, mke au mume, mwajiri au mwajiriwa, mwanachuoni au mwanafunzi, kiongozi au mfuasi ana wajibu wa kunasihi, kufanya islahi ya maendeleo ya umma na kuondosha kila jambo linalokwenda kinyume na uislamu.

Alisisitiza kusaidiana, kushirikiana na kujenga umoja sambamba na kuwasidia viongozi na kuwaombea dua ili waweze kufanya mema na yenye maslahi zaidi.

“Tutambue kuwa kwa miongozo mema ya viongpzi wa kijamii na kidini ndio hupatikana maslahi ya watu wote katika jamii,” alisema ustadhi Chum.

Aidha, alieleza kuwa mshikamano wa waislamu hautodhuriwa na watakaoukhalifu, wala watakaouchukia, madhali waislamu wamefungamana na kamba ya Allah na huku wameshikamana na kitabu cha Allah na sunna za Mtume (S.A.W), wakisaidiwa na mafungamano yao, kusafiana nia na kuwatii viongozi wao.

Sherehe hiyo ya Maulid yalianza kwa kusoma Qur-an tukufu suratul Aaraaf aya ya 156 hadi 158 iliyosomwa na Ustadhi Hamdan Juma kutoka Magogoni mjini Unguja.

1 comment:

  1. Umoja miongoni mwa waislamu haiwezi kupatikana kama viongozi wa dini watashindwa kuhubiri umoja na mshikamano miongoni mwetu, huku wakitambua tofauti zilizopo ktk madhheb mbalimbali.

    Hivi kwa mfano inakuwaje kiongozi wa sunni anapoeleza tofauti ziliopo baina yetu na madhheb nyingine kama vile; Shia,Ahmadia,Ismailia,Ibadhi,Bohora nk...aende mbali zaidi na kusema "hawa ni makafiri ndugu zangu" hivi, kweli patakua na umoja tena hapo?

    Mimi nadhani tungehesabu wale wote waliotamka kalima'La..ilaha illa allah' upande mmoja na wale wanaokataa upande mwaingine hapo kidogo, tungefanikiwa!

    Ila tukishindwa kufanya hivyo umoja wa waislamu utaendelea kua ndoto na matokeo yake yatakua kama vile Pakistan,Iraq,India,Afghanistan na kwengineko ambako waislamu wanauwana.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.