Habari za Punde

Inspekta alalamikiwa kutumia vibaya magwanda

 Kamishna akiri kupokea malalamiko

Na Mwandishi wetu

KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amesema jamii inapaswa kufahamu kuwa maofisa wa polisi ni binadamu kama watu wengine, hivyo nao inatokezea kufanya makosa.

Kamishna huyo alieleza hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na gazeti hili, kufuatia mwananchi mmoja kumlalamikia ofisa wa polisi mwenye cheo cha Inspeta kutumia vibaya cheo na magwanda yake vibaya.


Alisema kutokana na ubinadamu walionao polisi nao hufanya makosa iwe kwa makusudi, kutojua au kwa bahati mbaya, lakini hiyo haizuii jeshi kumchukulia hatua kwa kumchunguza na kumchukulia hatua pale anapobainika kufanya kosa.

Alisema kutokana na hali hiyo inapotokezea ofisa wa polisi kufanya makosa abebeshwe lawama kama binadamu wengine na sio kulilaumu jeshi zima kwani halina dhamira hiyo kwa wananchi.

Katika malalamiko yake, Hassan Mtwana aliwataka maofisa wa polisi kuacha kutumia vibaya fursa walizonazo za kimamlaka kwa kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wananchi kwa kutumia vyeo na magwanda yao.

Mwananchi huyo alisema wapo baadhi ya maofisa wa jeshi hilo wanatumia vibaya magwanda na vyeo vyao, jambo linalosababisha raia kukosa imani na jeshi hilo na kunyimwa haki zao kwa makusudi.

Alisema endapo jeshi hilo litaendelea kuwalea na kuwalinda maofisa wa namna hiyo, raia wengi watakosa imani na hiyo dhana ya polisi jamii itakosa muelekeo.

Kadhia hiyo ya Hassan, ambaye malalamiko yake ameyafikishwa kwa Kamishna wa Polisi alisema, amefanyiwa kitendo alichokiita kuwa si cha kiungwa na Inspekta wa polisi aliyemtaja kwa jina, kutumia vibaya madaraka yake na kumvunjia nyumba na kuisambaratisha familia yake.

Akizungumza kwa masikitiko alisema Inspekta huyo alitumia mwanya wa mzozo wa wake zake, hatimae mmoja kati ya wake hao kufika kituo cha polisi kupata muongozo na msaada wa kisheria kufuatia mzozo uliosababisha mapigano na mke mwenziwe.

Alisema baada ya Inspekta huyo kupata mwanya wa kumpatia msaada wa kisheria mke wa Hassan, mambo yalianza kugeuka na kuanza kudaiwa talaka, huko polisi huyo akichochea moto wa kudai talaka ulioanzishwa na mke huyo.

“Inspekta huyo kinyume na utaratibu alikuwa akifika nyumbani kwangu mara kwa mara ambapo baada ya muda mama watoto wangu alikuwa akinidai talaka hatua ambayo sikuona mantiki yake hatimae aliiomba mahakama ya kadhi isimamie talaka yake, lakini nilipopata waraka wa mahakama nikaamua kumruhusu aende”, alisema.

“Kama hiyo haitoshi Inspekta huyo kabla na baada ya kufunga ndoa na mama watoto wangu aliendelea kuishi katika nyumba yangu kwa zaidi ya miezi mitano mbali ya juhudi za kisheria nilizozichukuwa kutaka waondoke nyumbani kwangu kukwamishwa na Ispekta Jaku”, alibainisha.

Aidha alisema alifika kwa sheha wa shehia ya Pangawe kuomba msaada na kumtaka kwenda kituo cha Polisi Fuoni kupeleka lalamiko lake ambako lilitoka agizo la kutakiwa kuhamishwa Ispekta huyo lakini siku ya utekelezwaji kwa mkono wa bosi huyo ilishindikana kutokana na amri aliyoitoa.

“Nilishtuka nilipopata wito wa Polisi nilipofika kituo cha Polisi Fuoni niliambiwa nisijaribu kabisa kutekeleza azma yangu ya kuwahamisha katika nyumba yangu, nilipodadisi nimeambia agizo hilo limetoka juu na wao wanachopaswa kufanya ni kutekeleza na sio vyenginevyo”, alisema.

“Kauli hiyo imefuatiwa na maneno machafu na ya kejeli kutoka kwa wanandoa hao kuwa wao hawawezi kuhama kwa shinikizo langu bali watahama watakapojisikia kuhama, nami sina chochote cha kufanya wala kwa kwenda, kauli hiyo imenichoma na kuongeza chuki dhidi ya jeshi la Polisi”, Hassan alilalamika akieleza hisia zake mbele ya Kamishna.

Kwa upande wake Kamishna Mussa alithibitisha kufikishwa tuhuma na mwananchi huyo na kwamba ameshaamuru Inspekta huyo kuhama kwenye nyumba ya mlalamikaji na kwamba kama anahisi amevunjiwa sheria anayo haki ya kumshitaki.

Hata hivyo alieleza kuwa Inspekta huyo alikuwa akiishi nyumba hiyo kutokana na mke mpya kuwa na makubaliano na Hassan ya kuishi katika nyumba hiyo.

Kamishna Mussa alimshauri mwananchi huyo apelekea malalamiko yake kwa Kamanda wa polisi Mkoa wa Kusini kama anahisi kuna sheria zimekiukwa.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mwananchi huyo amewasilisha malalamiko hayo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini akidai kodi ya nyumba yake kwa miezi mitano ambayo Inspekta huyo alikuwa akiishi na mkewe mpya pamoja na kuungiwa umeme ambao ulikuwa umekatwa.

1 comment:

  1. Namsikitikia sana Bw. Hassan, na naamini hiyo 'imekula kwake'..kama kumbukumbu zangu ziko sahihi, hatuna kosa la namna hiyo kwenye penal code yetu(kuvunjiwa nyumba) unless kuwe na matumizi ya nguvu ama hila( without consent).

    Labda kosa la kimaadili kwa upande wa huyo kamanda au madai kuhusiana na hiyo kodi, ila hii naamini watamlipa.

    Ila nimpe pole Bw. hassan kwa mara nyingine! mapenzi ya 'kizushi' ya namna hii yanavyokolea, kwa kweli itamuumiza sana jamaa!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.