Mwenyekiti wa mpango wa kujitathmini kiutawala bora Afrika (APRM) kwa upande wa Tanzania Bw. John Shibuda akitoa utangulizi wa muhtasari wa ripoti ya mpango huo kwa Zanzibar mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, wakati wajumbe wa mpango huo walipofika OMKR Migombani kwa ajili ya kutoa muhtasari wa ripoti hiyo
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akipokea ripoti ya tathmini ya mpango wa kujitathmini kiutawala bora Afrika (APRM), kutoka kwa Katibu Mtendaji wa mpango huo Tanzania Bi. Rehema Twalib. Katikati ni mweyekiti wa mpango huo Tanzania Bw. John Shibuda.
(Picha, Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesifu juhudi zinazochukuliwa na Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Afrika (APRM) nchini Tanzania, kwa kuwashirikisha ipasavyo wananchi wa Zanzibar katika kutoa maoni na ushauri katika nyanja zote zinazogusa maisha yao.
Maalim Seif amesema wananchi wa Zanzibar wanahitaji sana kusikilizwa maoni yao juu ya mambo wanayowazunguuka, ikiwemo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwamba hatua hiyo itawawezesha kupendekeza njia muafaka za kudumishwa utawala bora na haki za raia wote kwa serikali zote mbili.
Alisema hayo leo huko ofisini kwake Migombani Zanzibar, alipokuwa na mazungumzo na wajumbe wa Baraza la Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM) kwa upande wa Tanzania.
Wajumbe hao walifika ofini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kumueleza maendeleo ya mpango huo, pamoja na kumkabidhi ripoti maalum ya mpango huo kwa upande wa Zanzibar, pamoja na mpango kazi wake.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema matokeo ya mpango huo yatakuwa na mafunaa zaidi kwa wananchi wa Zanzibar, pale yatakapogusia kwa kina maendeleo ya kukuza demokraisa na haki za raia, ikiwemo yale yanayozua mashaka na kuwepo dhana kwamba baadhi ya watu wanakosa haki zao.
Alieleza miongoni mwa mambo hayo ni uboreshaji dafatari la kudumu la wapiga kura, vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, malalamiko katika mahakama, polisi, maliasili ndani ya Muungano pamoja na mgawanyo wa rasilimali.
“Masuala haya ni muhimu kwa utulivu na amani ya nchi yetu katika siku zijazo, lazima wananchi wapewe nafasi ya kujadili na kutoa ushauri juu ya mambo hayo, na baadaye serikali na wadau wote waweze kuchukua hatua zinazofaa”, alisema Maalim Seif.
Hata hivyo, alisema amefarajika sana kuona sekta ya watu binafsi inapewa umuhimu mkubwa katika mchakato huo, kwasababu sekta hiyo ina mambo mengi ambayo serikali inapaswa kuyajua kwa undani hatua ambayo itachangia kuchukuliwa hatua zinazopaswa katika kufikiwa malengo yaliyokusudiwa.
Mwenyekiti wa ujumbe huo, John Shibuda alisema lengo la mchakato huo kuchukua maoni na mawazo ya kila upande, ni kuziwezesha serikali mbili kujua kwa undani zaidi hali halisi ya mambo, ikiwemo malalamiko na maoni ya wananchi juu ya mambo mbali mbali, ili iweze kuchukua hatua na maamuzi yanayofaa.
“Ni imani yetu mchakato huu wa miaka mitano utakapokamilika utazaa mambo mazuri kwa wananchi wa Tanzania na tunapata faraja kubwa kuona viongozi wa kitaifa na wananchi wote wanatupa mashirikiano ya hali ya juu”, alisema Shibuda.
Mapema akiwasilisha ripoti ya maendeleo ya mchakato huo wa kujitathmini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Katibu Mtendaji wa Mpango huo, Rehema Twalib alisema wameamua kutenganisha ripoti ya mpango huo katia ya Tanzania Bara na Zanzibar, baada ya kupokea maoni mengi kutoka Zanzibar kwamba ripoti yao kwa upande wa Zanzibar itenganishwe.
Alieleza kwamba baada ya ripoti hiyo kukamilika, Rais wa Jamhuri ya Muungano ataiwasilisha katika mkutano utakaowashirikisha viongozi wa nchi Barani Afrika ili ripoti za nchi mbali mbali ziweze kujadiliwa na baadaye nchi hizo kuchukua hatua za utekelezaji wake.
No comments:
Post a Comment