MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Seif Iddi ametoa changamoto kwa wanawake nchini kujenga utamaduni wa kuzaa watoto kwa kuzingatia uzazi wa mpango hali itakayowasaidia kumudu kuwatunza watoto hao.
Alitoa changamoto hiyo alipokuwa akizungumza kwenye kituo cha Green Hill kinachowahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kilichopo mtaa wa Sabasaba wakati wa ziara yake ya maadhimisho ya sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM.
Alisema kwamba kuzaa kwa mpangilio unaotakiwa humuwezesha mzazi wa watoto kumudu gharama za maisha ndani ya familia yake, zikiwemo za masomo pamoja na makuzi mazuri ya mtoto.
Alisema tabia ya baadhi ya wanawake kuzaa bila ya kanuni za uzazi wa mpango ni hatari kwa maisha yao na pia inasababisha kuwa na hali ngumu kimaisha kwa kuwapatia huduma watoto hao.
“Kwa kweli wanawake wenzangu mtu asiwadanganye katika suala hili la uzazi usiokuwa wa mpangilio, jaribuni kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili muweze kuwa na idadi ndogo ya watoto ambao mtaweza kuwatunza bila matatizo”, alisisitiza Mama Asha.
Alisema ni vyema kabla ya kuamua kupata watoto ni vyema pakawepo na matayarisho ya kuzaa watoto hao kwa madai kuwa watoto hupatikana kwa ushirikiano kati ya mume na mke na wala siyo vinginevyo.
“Ningewaomba wanawake wenzangu hebu kuanzia sasa turudi kwa Mwenyezi Muungu kwa kuanza na kuwathamini watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kujenga utamaduni wa kuwajali na hata kuwasaidia”, alisema.
Aidha alifahamisha kuwa wakati umefika kwa wanawake nchini kujenga utamaduni wa kuwajali pia watu wenye matatizo badala ya kuendelea kuweka mbele maslahi yao binafsi.
Katika risala ya kikundi cha Mke mwema iliyosomwa kwa mgeni rasmi na katibu wa kikundi hicho, Asimwe Kalumanzila ilieleza matatizo yanayokikabili kikundi hicho kuwa ni pamoja na kutopatiwa usajili wa kudumu.
Kutokana na kuunga mkono jitihada za wanakikundi hao, mke wa makamu wa Rais huyo alichangia shilingi 300,000 kwa ajili ya kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuahidi shilingi 200,000 kwa ajili ya kwenda kusajili kikundi cha Mke mwema.
No comments:
Post a Comment