Habari za Punde

Bilioni 6.6 Kujenga Barabara Arusha

Na Joseph Ngilisho, Arusha

MKOA wa Arusha utatumia zaidi ya shilingi bilioni 6.6 kugharamia utekelezaji wa miradi ya barabara mwaka wa fedha 2011/12.

Hayo yamesemwa na Meneja wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Arusha, Deusdedit Kakoko, katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi.


Mhandisi Kakoko amesema kiasi cha shilingi bilioni 2.9 zitatumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya barabara kuu zenye urefu wa kilomita 402.51

Aidha amesema Tanroads itatekeleza miradi 72 ya madaraja katika barabara kuu yenye thamani ya shilingi milioni 357.97.

Mbali na kazi hizo Mhandisi Kakoko, amesema Tanroads itatekeleza miradi ya barabara za mkoa zenye urefu wa kilomita 640.75 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 2.94.

Amesema TANROADS inatarajia kufanyia ukarabati madaraja 36 yaliyoko katika barabara za Mkoa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 359.

Kuhusu utekelezaji wa mpango wa Maendeleo, Mhandisi Kakoko amesema zaidi ya shilingi milioni 638 zitatumika kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi 10 ya barabara zenye urefu wa kilomita 43.3

Amefafanua kuwa mpaka Septemba 2011 mikataba ya kazi ipatayo 24 kati ya 40 imenunuliwa na makandarasi Mkoani Arusha yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.4

Kati ya mikataba hiyo, 14 ni ya barabara kuu yenye thamani ya shilingi bilioni 1.8 na 13 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.7 ni ya barabara za mkoa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.