Habari za Punde

Maofisa Wizara ya Habari Wapewa Changamoto Kuwa na Malengo Kwenye Semina Elekezi

Na Abdi Shamnah

MAOFISA Mipango kutoka Idara na Taaasisi zilizomo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, wametakiwa kuandaa malengo machache yalio bora, yenye uhalisia na kutekelezeka pale wanapoandaa taarifa za kila kipindi.

Changamoto hiyo imetolewa leo na Ofisa mkuu wa Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara hiyo, Thabit Ali wakati alipokuwa akiendesha mafunzo elekezi kwa Maofisa Mipango kutoka taasisi na Idara ziliomo katika Wizara hiyo, iliofanyika katika ukumbi wa Eacrotanal mjini hapa.


Mafunzo hayo ya siku moja, yameandaliwa na Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, kwa lengo la kuwaandaa vyema watendaji hao katika utekelezaji wa kazi zao, ikiwemo uandaaji wa malengo katika MTEF na Bajeti za kila mwaka.

Amesema maofisa hao ni wasaidizi muhimu katika Serikali, hivyo wana wajibu mkubwa wa kuandaa malengo machache yalio bora, yenye uhalisia na kutekelezeka na kuainisha aina ya shughuli zinazopasa kufanyika.
‘Sio vyema kuwa na malengo mengi kwa wakati mmoja kwani ni vigumu kutekelezeka’, alisema.

Aliwakumbusha umuhimu wa kuwa na malengo yenye shabaha maalum ili hatimae waweze kuyafanyia tathmin na kufahamu mafanikio yaliofikiwa.

Alifafanua kuwa malengo hayo yanapaswa kuwagusa moja kwa moja wananchi wote Unguja na Pemba, walio Mjini na vijijini ili waweze kufahamu uwepo wa taasisi hizo na juhudi zinazofanyika katika kuwaletea maendeleo.

Thabit alitoa wito kwa idara na taasisi hizo kuvitumia kikamilifu vyombo vya habari vya Redio TV na magazeti ili kutangaza malengo yao ili hatimae wananchi walio mjini na vijijini waelewe kinachofanywa na Serikali yao.
Katika hatua nyingine mkufunzi huyo alizishauri idara na taasisi zenye miradi kuwashajiisha wafadhili kusaidia, pale inapowezekana badala ya kuisubiri Serikali ambayo ina mambo mengi inayoshughulikia.

Wakichangia katika mafunzo hayo, baadhi ya washiriki walishauri kuwepo vitengo vya Uhusiano vitakavyokuwa na Bajeti ndani ya Idara na taasisi za Wizara hiyo, ili sekta ya habari iweze kutumika ipasavyo kutangaza sera mbali mbali na kushajiisha malengo yaliowekwa.

Wamesema ufinyu wa bajeti umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha utekelezaji wa malengo yanayowekwa, sambamba na fedha chache zinazopatikana kutumika kwa shughuli za kiutawala badala ya zile za kimaendeleo.

Mapema akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mipango, sera na Utafiti wa Wizara ya Habari, Utamaduni, utalii na Michezo, Mwita Mashaka, aliwataka watendaji hao kuitumia vyema fuersa hiyo kujenga uwezo ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao.

Alisema mafunzo hayo ni ukumbusho muhimu kwao ili kuondokana na kasoro mbali mbali ambazo zimekuwa zikijitokeza kila baada ya kipindi wakati wa kuandaa taarifa hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.