Habari za Punde

Meli ya Kitalii Yatia Nanga Pemba

Yatoka Afrika Kusini moja kwa moja

Na Haji Nassor, Pemba

HATIMAE bandari ya Mkoani Pemba kwa mara ya kwanza tokea kujengwa kwake, jana ilianza kupokea meli kubwa ya kitalii ikitokea Afrika Kusini ikiwa na watalii 58 ambao wanatokea Marekani na Uingereza kwa ziara ya siku moja kisiwani humo.

Mwandishi wetu aliekuwepo bandarini hapo alishuhudia meli hiyo Clipper Odyssey yenye namba za usajili IMO 8800195 ikiwasili bandarini hapo majira ya saa 12:50 asubuhi, ikiongozwa na kapteni wa shrika la bandari Zanzibar Makame Hassan ambapo baadae watalii hao wakaanza ziara yao katika maeneo mbali mbali ya kihistoria ya Kisiwani Pemba.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi bandarini hapo, Meneja wa Kampuni ya Sewe travel ya Chake chake ambayo ndioa waratibu wa ziara hiyo, Peter Molnar alisema kampuni yake ilifanya kazi kubwa hadi kufanikiwa kuwaleta watalii hao wakiwa na usafiri huo wa moja kwa moja.

Peter alisema, azma ya kampuni yake ni kuhakikisha wanaleta zaidi watalii kwa kutumia usafiri huo hasa kwa vile bandari ya Mkoani ina uwezo wa kupokea meli kubwa jambo ambalo wengi hawakulifikiria.

“Tutafanya tena juhudi za kuleta watalii hapa Pemba kwenye Kisiwa kizuri kwa shughuli za kitalii, kwa vile meli kubwa zinafunga bila ya tabu na gati ina uwezo wa kufunga”,alisema Meneja huyo.

Kwa upande wake Kapteni Makame Hassan kutoka Makao makuu ya shirika la bandari Zanzibar, ambae alisaidiana na nahodha wa meli hiyo kuingiza bandarini hapo, alisema meli hiyo ya kitalii ni ya kwanza kufunga bandari ya Mkoani.

Alieleza kuwa gati ya Mkoani ina uwezo wa kufunga meli yenye uzito wa tani hadi 9000 ambapo meli hiyo ina uzito wa tani 5218, na gati hiyo ina urefu wa mita 117 na meli hiyo yenyewe ikiwa na urefu wa mita 103 ambapo ilikuja na mabaharia 78.

Nae Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Pemba, Hamad Salim alisema, wakati umefika kwa wafanyabiashara wakubwa kuitumia bandari ya Mkoani kwa kupakulia bidhaa zao mbali mbali, kwa vile hilo linawezekana.

Kuhusua maghala alieleza yapo ya kutosha ya kuhifadhia bidhaa hizo na Shirika la Bandari litaendelea kuyaimarisha licha kwamba baadhi ya bidhaa zinapokuja huja kwenye makontena maalumu.

“Sisi kama shirika la bandari hatujakaa kimya juu ya kuimarisha maghala ya kuhifadhia bidhaa za wafanyabiahara wetu wanaotumia bandarai hii”,alieleza Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo amesema juhudi za kuifanyia matengenezo badari hiyo ili kuondoa tatizo la kutuama maji zimefikia pahala pazuri na wanatarajia kabla ya mvua za masika kuanza iwe zoezi hilo limekamilika.

Watalii hao 58 mara watakapomaliza ziara yao kwa kutwa moja Kisiwani Pemba wanatarajiwa kurudi kwa kupitia Unguja na kisha kuendelea na ziara yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.