Habari za Punde

Mhadhiri SUZA: Tafiti Ufunguo wa Maendeleo

Na Haji Nassor, Pemba

MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Mohamed Ali Shehe amesema Zanzibar haiwezi kuendelea kama suala la tafiti zinazofanywa hazikupewa kipaumbele na kuzitumia ipasavyo kama mataifa mengine yaliyoendelea ulimwenguni yafanyavyo.

Alisema nchi zote zilizoendelea kwanza huweka mbele suala la kuzifanyia kazi tafiti zinazofanywa ndani ya nchi zao kwa vile kupitia hizo ndio Serikali hugundua changamoto mbali mbali ambazo zinalikabili taifa na hatimae kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.


Mhadhiri huyo alitoa tamko hilo jana huko ukumbi wa mikutano wa TASAF mjini Chake chake Pemba alipotoa maelezo mafupi juu ya uzinduzi wa tume hiyo ya utafiti kwa Zanzibar mbele ya watendaji wakuu wa Serikali na jumuia za kiraia Kisiwani Pemba.

Alisema Zanzibar zipo tafiti kadhaa zilizofanywa na wasomi wa visiwa hivyo, lakini bado hazijatumiwa kama ndio njia sahihi ya kujiletea maendeleo na badala yake haziangaliwi kwa kina na kupoteza rasilimali muhimu.

“Wakati umefika sasa kuziona tafiti zilizofanywa zinaibuliwa na kuyatafutia ufumbuzi wa kina yale yaliyoonekana wakati watafiti na wasomi walipokuwa katika kazi hiyo”, alieleza Mhadhiri huyo.

Aidha amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga kiasi cha shilingi 19 bilioni kwa mwaka uliopita lakini hakuna kasi ya uombaji wa fedha hizo hasa kwa wasomi na watafiti kutoka Zanzibar.

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa alisema zipo tafiti kadhaa zilizofanywa Zanzibar, lakini nyingi zao zimekuwa zikiishia kwenye makabati jambo ambalo haliwezi kusaidia kusukuma mbele maendeleo nchini.

Hata hivyo alisema uhaba wa watafiti kwa baadhi ya wakati nao umekuwa ukichangia hata hizo tafiti chache zilizofanywa kutofanyiwa kazi ipasavyo na kutokuwepo mabadiliko kabla na baada ya tatifi zenyewe.

Aidha amewataka watendaji wakuu hao wa Serikali kuhakikisha wanatoa ushirikiano mkubwa wanapotokezea watafiti kupitia taasisi zao, ikiwa ni pamoja na kuwatoa wenye uwezo ili kuungana na wengine.

“Suala la utafiti ni pana na linahitaji ushirikiano kwa pande zote mbili kwa maana mfanyaji na mfanyiwa ili zipatikane taarifa za kweli”, alieleza Tindwa.

Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wanawake nao kujitokeza kwa wingi kufanya tafiti mbali mbali, kwa vile bado idadi yao ni kidogo hapa Zanzibar.

Tume hiyo ya utafiti Zanzibar inasimamiwa na SUZA, na iko chini ya ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.