WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetiliana saini ya mikataba na kampuni tatu zilizoshinda kandarasi ya ujenzi wa skuli tatu za sekondari katika mkoa wa mjini Magharibi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Abdulla Mzee Abdulla alitia saini hiyo katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Wizara hiyo Mazizini.
Baada ya kutiliana saini Naibu huyo alisema skuli hizo zitakazojengwa zitakuwa za kisasa na zitazingatia mahitaji yote ya elimu kwa wanafunzi.
Alisema kuwa skuli hizo zitakazojengwa ni pamoja na Kwamtipura ambapo itajengwa na kampuni ya M/S B.H.Ladwa ya Tanzania ambapo atajenga kwa thamani ya shilingi 1,880,800,000 bila ya ongezeko la VAT ambayo ni ni shilingi 338,544,000.
Kwa mujibu wa Naibu huyo kampuni itatakiwa imalize ujenzi huo, Aprili 2013, tayari kwa masomo.
Saini nyengine wizara hiyo ilitiliana na kampuni ya M/S Lukumbulu Investment Company Limited ya Tanzania, ambayo itajenga skuli ya sekondari ya Kiembesamaki.
Kampuni huyo itaijenga skuli hiyo kwa kiasi cha shilingi 2,148,973,400 bila ya ongezeko la thamani ya VAT, ambayo ni shilingi 386,815,212 na itajengwa kwa muda wa miezi 10 na inatarajiwa kukamilika Februari 2013.
Mkandarasi mwengine ni M/S Group Six International Limited ya China atajenga skuli mpya ya sekondari ya Mpendae kwa thamani ya shilingi 1,566,424,661 bila ya ongezeko la thamani ya VAT ambayo ni shilingi 281,956,439 na itajengwa kwa muda wa mwaka mmoja ambapo ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Aprili 2013.
Naibu huyo alisema kuwa majengo hayo yatakayojengwa yatakuwa ya ghorofa ambapo Kwamtipura litakuwa la ghorofa tatu, Kiembesamaki ghorofa mbili na Mpendae ghorofa moja ambapo kutakuwa na huduma zote muhimu kwa ajili ya skuli.
Alifahamisha kuwa skuli ya Kwamtipura na Kiembesamaki itakuwa na madarasa 24 na itachukuwa wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na skuli ya Mpendae itachukuwa wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Alisema kuwa ujenzi wa skuli zote hizo ni pesa zilizokopwa kutoka Benk ya Dunia ambapo zilikuwa Dola 42,000,000 ambapo pesa hizo zilikuwa katika miradi ya ujenzi wa skuli 19 ikiwa skuli 13 zishamalizika na skuli 3 zinaendelea na ujenzi ikiwa skuli 3 ndio hizi zinazotarajiwa kuanza ujenzi wake Aprili 23,2012.
Abdulla alisema kuwa ujenzi wa skuli zote hizo za kisasa unatokana na serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kupanua elimu ya sekondari kwa kupata majengo mapya na yanayozingatia huduma zote za elimu.
Alisema kuwa anataraji kwa wakandarasi hao kutoa kipaumbele kwa mafundi wa kujenga kuwa watatoka hapa hapa nchini kwani kunavijana wengi wanahitaji kazi hizo na sio kwenda kuwachukuwa vijana kutoka nje ya Zanzibar.
Hata hivyo aliwataka wakandarasi hao kwenda kujisajili katika Idara ya wakandarasi watakuwa hawawezi kuendelea na ujenzi wao kwa uhuru na pia aliwataka kujenga majengo yaliobora zaidi kwani washasoma majengo yaliojengwa na wenzao.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma alisema anasikitishwa kwa pale wanapokuja wakandarasi halafu wakawa wanajenga na ujenzi huo kuwa usifike mwisho na kuamua kuondoka na pesa na badala yake kubaki maboma ambayo hayawezi kuendelezwa kwa maendeleo yoyote ya nchi.
Alisema kuwa pia kunawakandarasi wengine huchukuwa wafanyakazi kutoka nje ikiwa pesa zinazokopwa ni za wananchi wanazolipa hivyo ni vizuri kwa wakandarasi hao wakaangalia nafasi kubwa kwa wanachi wa hapa.
No comments:
Post a Comment