Habari za Punde

Qatar Air Ways Yanukia Kutua Zanzibar

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utalii Zanzibar Alhalil Mirza akizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali kuhusiana na safari yake ya kikazi nchini Ujerumani.Hafla iliofanyika huko ofisini kwake Amani Mjini Zanzibar.

PICHA NA YUSSUF SIMAI MAELEZO ZANZIBAR
Na Mwantanga Ame

IDADI ya watalii Zanzibar, inatarajiwa kuongezeka hasa baada shirika la ndege la Qatar ‘Qatar Air Ways’ kukubaliwa ndege zake kushuka kwenye ardhi ya Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Ali Khalil Mirza aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya kuelezea ziara waliyoifanya watendaji wa SMZ na wafanyabiashara walioshiriki katika maonyesho ya Biashara nchini Ujerumani.

Mkurugenzi huyo alisema tayari kumekuwa na mazungumzo katika hatua za mwisho kuwapo makubaliano na shirika la ndege la Qatar, ambalo litatua moja kwa moja hapa Zanzibar.


Alisema kuja kwa shirika hilo litaweza kuongeza idadi ya watalii waingiao nchini kwa mfumo wa mtalii mmoja mmoja badala ya kuendelea kuingiza watalii kwa makundi.

Alisema shirika hilo baada ya kukamilisha taratibu zake linatarajiwa kuanza safari zake kuanzia mwezi Julai ama Septemba mwaka huu.

Alisema pia shirika hilo litaanzisha safari ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki ikiwa pamoja na kutumiwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.

Eneo jengine ambalo ziara hiyo wameweza kufaidika nalo alisema linalohusu mazungumzo na shirika la ndege la Air RABIA, ambalo limekuwa likifanya safari zake katika mataifa ya Misri, kutokana na hivi sasa kukabiliwa na machafuko ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Alisema baada ya mazungumzo hayo wanatarajia kupata jibu katika maonyesho ya utalii yajayo yatayofanyika nchini Dubai.

Aidha, alisema katika ziara hiyo pia Zanzibar itaweza kufaidika na huduma za utembezaji wa watalii baada ya kuwapo kwa mkataba uliosainiwa kati ya Chama cha Waongozaji Watalii Zanzibar na Chama cha Waongozaji Watalii wa Ujerumani.

Akizungumzia juu ya idadi ya watalii walioingia Zanzibar hadi hivi sasa alisema tayari wamefikia 175,067, kiwango ambacho hakijaingiza watalii wanaotoka Tanzania bara, ambao idadi hiyo inaweza kuongezeka kufikia watalii 215,000 hadi 220,000.

Akiendelea alisema mashirika ya ndege ambayo yamekuwa yakileta watalii kwa wingi hadi sasa ni matatu likiwemo la Kenya Air Ways (KQ), Ethiopian Air Line na Oman Air huku kukiwa na chata nane ikiwemo ya Italia na Ubelgiji.

Kutokana na mafanikio hayo Mkurugenzi huyo alisema hivi sasa taasisi hiyo imo katika kutekeleza mkakati wa utalii kwa wote kwa kuhakikisha inayaimarisha majengo ya historia ili watalii waingiao nchini waweze kusoma mazingira mbali mbali ya maisha ya watu wa Zanzibar.

Aidha, Mkurugenzi huyo, alisema wanalazimika kujiandaa na hilo kutokana na kutafuta mbinu zitazoweza kuyaingia masoko ya utalii yaliopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC, Kaskazini mwa Asia ikiwemo China na utalii wa ndani.

Alisema mbali ya mipango hiyo pia Kamisheni hiyo imo kuwaandalia mazingira mazuri mapapasi kwa kuhakikisha wanaotaka kufanya kazi hiyo wanapewa elimu pamoja na kuwa na vitambulisho maalum baada ya kuridhiwa na Chama cha Watembeza wataliii Zanzibar (ZATO) na vyombo vya sheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.