Habari za Punde

RC: Wanafunzi Zanzibar Oneni Aibu Kufeli Kiswahili

Na Salum Vuai, Maelezo

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis, amewataka wanafunzi wa skuli za Zanzibar waone aibu kufeli mitihani ya lugha ya Kiswahili, na badala yake wafanye bidii kuisoma ili waweze kuifahamu kikamilifu.

Wito huo aliutoa jana katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Zanzibar yaliyofanyika kwenye ukumbi wa EACROTANAL, na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wasomi wa vyuo, wasanii na sekta nyengine tafauti.


Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa, inasikitisha sana kuona wanafunzi wengi wa Zanzibar hufeli mitihani ya Kiswahili kwa asilimia kubwa kuanzia skuli za msingi, sekondari hadi elimu ya juu.

"Jambo hili linaleta huzuni kwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili. Nafahamu kuwa jitihada kubwa inafanywa na BAKIZA kutoa vipindi vya Kiswahili katika redio, TV na Redio za ZBC".

Alisema ni wajibu wa kila mwanafunzi kuvitumia vipindi hivyo na vyengine ili kuhakikisha wanafunzi wa Zanzibar wanaongoza katika somo hilo.

Aidha aliishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kuhamasisha matumizi ya kamusi la Kiswahili Fasaha hasa katika skuli na vyuo, kwani kamusi hilo limejaa maneno ya Kiswahili yaliyotafsiriwa vizuri na kusheheni utamaduni wa Mswahili.

Khamis alitumia fursa hiyo kuwahimiza Waswahili kuuenzi utamaduni wao kwa kutumia zaidi Kiswahili katika kila eneo linalohitajika, na kuhamasisha wengine kufanya hivyo na kuepuka kutumia lugha ya kigeni mbele ya wenyeji wa Kiswahili.

Kwa upande wa wasanii wa mashairi ya nyimbo, Mkuu huyo wa Mkoa aliwashauri kuiga utunzi wa washairi wa zamani ambao tungo zao zilitumia lugha iliyofumbwa, kwa pia kutumia maneno teule na yasiyokirihisha kusikiliza mbele ya watu wengine.

Alisema watunzi hao wakongwe, walichangia kwa kiasi kikubwa kuendeleza ubunifu wa kifasihi kwa wasanii chipukizi, na hivyo kuipa hadhi inayostahili lugha ya Kiswahili.

Alilipongeza na kulishauri Baraza la Kiswahili Zanzibar ambalo ndilo linaloandaa na kusimamia maadhimisho ya siku hiyo, kuendelea na juhudi za kuwaendeleza waandishi chipukizi wa mashairi na kuwahamasisha kupenda kuandika kwa kutumia lugha teule yenye tamathali za semi na mafumbo.

Mapema Katibu Mtendaji wa BAKIZA, Khadija Bakari Juma, alisema miongoni mwa mikakati yao katika kukiendeleza Kiswahili, ni kutembelea maskuli kwa lengo la kushajiisha walimu na wanafunzi kufahamu na kutumia lugha fasaha katika masomo yao.

Aidha alisema BAKIZA inakaribisha maoni na ushauri wa watu wote yenye lengo la kukiimarisha Kiswahili ili kiandikwe na kuzungumzwa vizuri na kuepuka upotoshaji wa maneno.

Katika maadhimisho hayo, kulisomwa makala zinazoelezea wasifu na jitihada za wasanii watatu waliochangia kwa njia tafauti kuiendeleza lugha hiyo, ambao ni marehemu Bakari Abeid Ali, Iddi Abdallah Farahan na Issa Haji Pandu 'Matona'.

Aidha washindi watatu wa shindano la utunzi wa mashairi walizawadiwa fedha taslimu katika hafla hiyo ambayo pia ilipambwa kwa nyimbo za wanafunzi kutoka Uroa Wilaya ya Kati pamoja na zoezi la chemsha bongo lililohusisha wanafunzi wanane kutoka skuli za sekondari za Mkoa wa Mjini Magharibi.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na watendaji wakuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, akiwemo Naibu Waziri Bihindi Hamad Khamis, Katibu Mkuu Dk. Ali Mwinyikai na Naibu wake Issa Mlingoti Ali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.