Habari za Punde

Zanzibar ID ya Kwanza kwa Ubora Afrika

Na Mwantanga Ame

SHIRIKA la kusimamia Viwango na Usalama la Kimataifa, limesema serikali ya Zanzibar, kipindi cha miaka sita mfululizo ni ya kwanza katika bara la Afrika, kuweza kuzalishalisha vitambulisho vya ukaazi viliyo na ubora wa kimataifa duniani.

Wakala wa Ukaguzi wa Kimataifa juu ya uthibitisho wa Viwango na Usalama kutoka nchini Israel, walieleza hayo jana huko Zanzibar Beach Resort, baada ya kukamilisha ukaguzi wa ndani ya Idara hiyo inayozalisha vitambusho vya Mzanzibari mkaazi.


Wakaguzi hao walieleza Zanzibar inastahiki kupata vyeti viwili vya ubora cha ISO 9001 na ISO 27001 kwa vile imeweza kuzalisha vitambulisho kwa viwango vya kimataifa na usalama duniani.

Avraham Rost, Wakala wa Shirika hilo kutoka nchini Israel, alisema Zanzibar, kwa bara la Afrika, ni ya kwanza kukidhi ubora wa kimataifa katika uzalishaji wa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi ikilinganishwa na mataifa mengine yenye kutoa huduma hiyo kimataifa kupungua hadhi yake siku hadi siku.

Alisema hadhi hiyo Zanzibar, inaipata baada ya taasisi yao kuridhika na shughuli zinavyoendeshwa ndani ya Idara hiyo kwani imeweza kuimarisha uzalishaji wa viwango pamoja na kusimamia usalama wa ndani wa mfumo wa utoaji vitambulisho.

Kutokana na mafanikio hayo Mkaguzi huyo, aliuomba uongozi wa Idara hiyo kuhakikisha anaendeleza ushirikiano na wafanyakazi ili kuweza kulinda mfumo wa ubora na usalama katika kuzalisha vitambulisho.

Nae Mkaguzi wa Usalama na Viwango, Merav Vered,
alisema Zanzibar kwa kiasi kikubwa inastahili kupewa sifa kwa vile imemudu kukabiliana na mabadiliko iliyoyatoa kwa wakati, kwa kukifanya kituo chake cha vitambulisho kuwa na mfumo bora wa matumizi ya teknolojia ya kisasa.

Alisema mpango wa serikali wa kuunganishwa katika mkonga wa taifa, taasisi yao ina imani kubwa utaweza kuimarisha zaidi hadhi ya uzalishaji na usalama wa vitambulisho vinavyotolewa na kituo hicho kuwa bora zaidi.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya serikali mgeni rasmi katika ripoti hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Maulid Salum alisema serikali ya Zanzibar imefarajika kuona inaendelea kuwa ni ya kwanza kwa bara la Afrika kuwa na vitambulisho na Idara inayotoa huduma zake kimataifa.

Alisema hivi sasa serikali imo katika matayarisho ya kuingia katika mkonga wa kitaifa ambao utaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa jambo ambalo litaongeza ufaniki katika kituo hicho.

Nae, Mkurugenzi wa Idara hiyo, Mohammed Juma Ame, akitoa shukrani zake alisema Idara yao itahakikisha inaendeleza sifa hiyo kwa kuongeza ushirikiano na watendaji wa taasisi hiyo.

Alisema, wamefurahia kuona wakaguzi hao kuweza kutogundua kasoro hata moja licha ya kuwataka kufanya mabadiliko ndani ya mfumo wa uzalishaji wa vitambulisho na Usalama katika kipindi kifupi huku ukiwa na masharti magumu.

Akizungumzia juu ya kuja kwa vitambulisho vya Taifa, Mkurugenzi huyo, alisema bado hadhi ya vitambulisho vya Mzanzibar itaendelea kuwa juu kwani matumizi yake yatazidi katika mambo ya Zanzibar.

Alisema vitambulisho vya Mzanzibari vitabakia kwa vile Zanzibar bado ni nchi yenye mamlaka yake, kama ilivyo katika uhalali wa kuwa na bendera yake, wimbo wa taifa na muhuri wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.