Habari za Punde

Habari SC Zatinga Fainal ya NSSF Dar.



Soka yaitambia Uhuru, netiboli yairusha roho NSSF
Na Juma Mmanga, Dar es Salaam

TIMU za soka na netiboli za Habari SC, zimeingia fainali ya mashindano ya NSSF kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi katika michezo ya nusu fainali iliyochezwa jana katika viwanja vya TCC Chang’ombe.

Kinadada wa netiboli ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo, waliisanbaratisha timu ya NSSF wenyeji wa ngarambe hizo, mabao 34-13.

Wafungaji wa Habari katika mtanange huo, walikuwa Amina Khamis Fataki pamoja na pacha wake kimchezo Fatma Abdallah.


Kwa ushindi huo, timu ya Habari ambayo imeonesha uwezo mkubwa katika patashika hizo za mwaka huu, inasubiri kujua itapambana na timu gani katika fainali kati ya TBC Queens na Mwananchi wanaotarajiwa kuvaana leo katika nusu fainali ya pili.

Wakati hayo yakijiri kwa mchezo wa netiboli, kwa upande wa soka, timu ya Habari imeifanyia mauaji makubwa Uhuru Publications kwa kuitandika mabao 4-1 katika mchezo uliotawaliwa na vijana hao wa Zanzibar kwa kiasi kikubwa.
Mabao ya washindi yalifungwa na Amour Mussa na Yussuf Saleh ambapo kila mmoja aliingia nyavuni mara mbili.

Amour Mussa alianza kucheka na nyavu katika dakika ya 35, kwa bao safi lililodumu hadi wakati wa mapumiziko.

Naye Yussuf Saleh alionesha umahiri wake kwa kuiandikia Habari bao la pili katika dakika ya 55, kabla Amour Mussa kujiongezea bao la pili dakika ya 63 kabla Saleh kuhitimisha ushindi uo maridhawa kwa bao la dakika ya 65.

Sasa Habari SC itapambana na mshindi wa mchezo wa nusu fainali ya pili unaozikutanisha timu za TBC na waandaaji wa michuano hiyo NSSF zinazotajariwa kutiana mikononi leo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.