Habari za Punde

Maalim Seif Avitembelea Vyombo vya Habari vya Serikali

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Yussuf Omar Chunda (katikati) akitoa ufafanuzi juu ya shughuli zinazofanywa na Idara hiyo, wakati Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipofanya ziara ya kutembelea Idara hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad aliangalia usanifu wa gazeti la Zanzibar leo wakati alipotembelea shirika la magazeti ya Serikali Zanzibar huko Rahaleo ikiwa ni mfululizo wa ziara zake katika taasisi za Serikali.

Na Hassan Hamad OMKR

Tume ya utangazaji Zanzibar inakusudia kufanya mazungumzo na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ili kujadiliana juu ya haja ya kuweka udhibiti wa kuingizwa bidhaa zinazotumia mfumo wa analog kwa vile vifaa na bidhaa hizo hazitotumika tena ifikapo mwaka 2013.

Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw, Chande Omar ameeleza hayo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad aliyefika katika ofisi za tume hiyo kuangalia maendeleo yake na changamoto inazo kabiliana nazo.


Bw. Chande amesema wakati nchi za Afrika Mashariki na Kati zikijiandaa kuachana na mfumo wa analog ifikapo Disemba mwaka huu, hakuna budi kwa bidhaa hizo kuwekewa udhibiti wa kuingia nchini, ili kuepusha mrundikano wa vifaa hivyo wakati muda wake wa matumizi utakapomalizika.

Amesema uchunguzi unaonesha kuwa licha ya vifaa hivyo kukaribia kumaliza matumizi yake, bado vimekuwa vikiingizwa kwa wingi nchini, hali inayopelekea pia uchafuzi wa mazingira.

Hata hivyo Bw. Chande amesema changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni namna ya kuibadilisha jamii kuweza kutumia vifaa vya dijital kutoka analog ikizingatiwa kuwa mfumo huo unahitaji kuwa na ving’amuzi ambavyo ni ghali.

Tume hiyo pamoja na mambo mengine ina jukumu la kutoa leseni na mawimbi ya matangazo kwa vituo vyote vya radio na televisheni ambapo hadi kufikia sasa jumla ya radio 23 zimepewa leseni za kurusha matangazo pamoja na televisheni 7 zikiwemo za serikali na binafsi.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kwa upande wake amesisitiza haja ya kuwaelimisha wafanyabiashara juu ya muda wa matumizi kwa vifaa vya analog, ili kuanza kuweka kipaumbele kwa vifaa vya dijital.

Maalim Seif ambaye pia alifanya ziara katika vyombo vya habari vya serikali vikiwemo ZBC Radio na Televisheni, Shirika la magazeti ya serikali na mitambo ya kurushia matangazo ya vituo hivyo iliyoko Bungi, Dole na Masingini pamoja na chuo cha uandishi wa habari Vuga, amesema vyombo vya habari ni muhimu kutokana na umuhimu wa taaluma hiyo katika kuwapasha habari wananchi.

Hivyo amewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa kujiamini na kulinda maadili ya kazi hiyo ili kuepusha migogoro katika jamii.

“Hivi sasa maadili kwa waandishi yamepotea, ni vyema kuwafunza waandishi hawa juu ya kufuata maalidili yao na waweze kuyafanyia kazi”, alisisitiza Maalim Seif wakati alipotembelea chuo cha habari Vuga kilicho chini ya mkurugenzi wake Bw. Saleh Yussuf Mnemo.

Ametoa changamoto kwa chuo kicho kutafuta eneo ili kujenga chuo kipya kinachokwenda na wakati na kuondokana na uhaba wa eneo la kufanyia sughuli zao.

Katika shirika la magazeti ya serikali, Mhariri mtendaji wa shirika hilo Bw. Abdulla Muhammed amesema shirika hilo lina mpango wa kuanzisha gazeti jengine ambalo kwa kuanzia litakuwa likichapishwa kila wiki.

Amesema hatua hiyo inakuja kutokana na gazeti moja kutokidhi haja ya kuwapasha habari wananchi, na kwamba gazeti hilo litatoa kipaumbele kwa sekta ya utalii na michezo ambazo bado hazijapewa umuhimu unaostahiki.

Bw,. Abdulla amesema shirika hilo linakabiliwa na changamoto tofauti zikiwemo baadhi ya taasisi za serikali kushindwa kulipa madeni yao magazeti na kuamua kuzuia kuzisambazia magazeti hadi hapo zinatakapojirekebisha.

Makamu wa Kwanza wa Rais aliunga mkono wazo hilo la kuzuiliwa kwa taasisi hizo kupelekewa magazeti ili kulinda mapato ya shirika.

Amelihimiza shirika hilo kuharakisha juhudi za kupata mtambo wa kuchapia magazeti ya serikali ili kuepusha usumbufu unaojitokeza ambapo kwa sasa gazeti la Zanzibar Leo linachapishwa mjini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.