Habari za Punde

Mchango wa Walimu ni Muhimu kwa Maendeleo

Na Khamis Amani

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema maendeleo yoyote ya nchi yamo mikononi mwa walimu kutokana na kile wanachokiandaa mapema.

Serikali imefahamisha kuwa, walimu ndio wadau wakuu wa maendeleo kutokana na dhima kubwa waliyoichukuwa ambayo ndiyo inayopelekea taifa kukua kimaendeleo.

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamadi, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na walimu wa skuli mbali mbali zilizomo ndani ya mkoa wa Kaskazini Unguja.


Alisema, walimu wana dhamana kubwa katika nchi na ni jukumu lao kuandaa mazingira mazuri ya ufundishaji kwa manufaa ya ustawishaji wa nchi.

"Tukumbuke kuwa tumekubali kubeba dhima kubwa kwa maslahi ya serikali, lazima tufanye kazi kama tulivyojikubalisha kwani nyinyi ndio chanzo kikuu cha maendeleo ya nchi", alisema Naibu Waziri.

"Hakuna tunda lolote lisilotokana na ualimu iwe madaktari, mainjinia, wataalamu wa kilimo sasa ikiwa hamjitumi ipasavyo katika kazi zenu vipi mtaisadia serikali katika suala zima la maendeleo", aliongeza.

Naibu Waziri aliwataka walimu kutokuwa na khiyana katika kazi kazi za ufundishaji kwa kuwapa wanafunzi elimu itakayowasaidia katika maisha yao, kama na wao walivyopatiwa na walimu wao walipokuwa wanafunzi na hatimae kufikia hapo walipofikia.

Alifahamisha kuwa, suala la ualimu ni zito na si kwa serikali peke yake bali hata kesho mbele ya Mwenyezi Mungu, ambapo kila mmoja ataulizwa jinsi alivyoitoa neema hiyo.

Hivyo aliwataka walimu kutumia neema hiyo kwa kutoa elimu bora ili waweze kuisaidia nchi kupata vizazi vilivyo na elimu katika nyanja mbali mbali za kiuchumi.

Sambamba na agizo hilo, Naibu Waziri aliwataka walimu hao kujituma na kuachana na kufanya kazi kwa mazowea, kwani hawawezi kujenga nchi bila ya kuwa na wasomi jambo ambalo linahitaji umakini wa hali ya juu ulio mikononi mwao.

Aidha aliwataka Walimu Wakuu kusimamia ipasavyo majukumu yao na kuondokana na tabia ya muhali kwani hivi sasa hali ya nchi imekuwa mbaya sana kielimu.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alipata nafasi ya kukagua kazi za walimu kupitia wanafunzi wao na kujionea hali halisi ya maendeleo na matatizo yaliyojitokeza.

Baadhi ya matatizo yaliyojitokeza, walimu wengi wamekuwa na tabia ya kutopitia kazi walizozitoa kwa wanafunzi pamoja na kutosomeshwa kwa muda, hali ambayo Naibu Waziri hiyo ameikemea kwa kusema kuwa haimjengi mwanafunzi kwa kutojulikana uwezo wake wa kile alichofundishwa.

Naibu Waziri katika ziara hiyo alifuatana na Mkurugenzi wa Maandalizi Msingi Uledi Juma Wadi, Mkurugenzi Taasisi ya Elimu Suleiman Yahya Ame, pamoja na Maafisa mbali mbali wa Wizara ya Elimu, Elimu wilaya ya Kaskazini 'A' na Kaskazini 'B' na mkoa wa Kusini Unguja.

Baadhi ya skuli zilizotembelewa na Naibu Waziri huyo ni skuli ya sekondari ya Matemwe, skuli ya msingi na sekondari ya Pwani Mchangani, skuli ya Kiwengwa sekondari na msingi, skuli ya Kinyasini sekondari pamoja na skuli ya sekondari ya Mahonda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.