Habari za Punde

Dk. Shein apangua Mawaziri : Shamuhuna apelekwa Elimu, Shaaban Ardhi

Nyanga aenda Kilimo, Jihad Mifugo

Mbarouk apewa Habari, Mansoor hana wizara maalum

Na Mwandishi wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mabadiliko ya kuwabadilisha wizara baadhi ya Mawaziri.

Katika mabadiliko hayo, Dk. Shein amemteua Ramadhan Abdalla Shaaban kuwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, kuchukua nafasi Ali Juma Shamuhuna.

Kabla ya mabadiliko hayo, Waziri Shaaban alikuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.

Waziri Shamuhuna ameteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, wizara ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Waziri Shaaban.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Dk. Shein amemteua Suleiman Othman Nyanga kuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili kuchukua nafasi ya Mansoor Yussuf Himid ambae sasa anakuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiyekuwa na wizara maalum.

Kabla ya mabadiliko hayo, Nyanga alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiyekuwa na Wizara maalum.

Aidha Dk. Shein amembadili wizara aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilah Jihad Hassan ambae sasa anakuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Said Ali Mbarouk sasa anakuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo.

Katika uteuzi mwengine, Dk. Shein amemteua Sheha Mohammed Sheha kuwa mshauri wa Rais Pemba.

Uteuzi huo umeanza tarehe 2 Aprili 2012.

7 comments:

  1. Ni jambo jema lkn. Kwa kweli wizara ya Ardhi Makaazi, Maji na Nishati bado haijapata mtu madhubuti, hii ni wizara nyeti na yenye kuamua hatma yetu kama waz'bari(hakuna Z'bar bila ya ardhi)

    Wahadimu tunahitaji kuelimishwa kuhusu umuhimu wa ardhi, Ardhi inasimamiwa vibaya,inajengwa ovyo: maeneo ya kilimo mfano Mwera, Fuoni kianga n.k yanajengwa majumba yale ya uwanda eti ndio yanakhuishwa(watu wanapanda miti).

    Serikali kwa nia njema imepima viwanja Tunguu, wahadimu wamegawana kumi kumi na uwezo wa kuvijenga hawana! matokeo yake vijana wananunua maeneo ya kilimo ili kujenga, Tunguu imebaki vile vile zaidi ya miaka 5 sasa.

    ReplyDelete
  2. shamuhuni ni mbadhirifu ameshauza maeeneo yote na fukwezote tunaomba chombo cha sheriya kimdhibiti kwa ubadhirifu ufisadi siyo kumbadilishiya wizara muda wakulindana umekusha

    ReplyDelete
  3. Ni kipindi cha mwaka na miezi mitatu takriban tokea mawaziri walipoteuliwa kushika nyadhifa zao.

    Ni wakati muwafaka kupima utendaji wao na jinsi walivyokabiliana na changamoto zilizojitokeza.

    Katika mabadiliko ni vyema Mheshimiwa Rais angeliingiza japo sura moja mpya katika safu ya Mawaziri kuangalia utendaji wake kuliko kuwazungusha waliopo.

    Kipindi cha kupimana kimepita kilichobaki ni kuwajibika na Mhe Rais asiishie Mawaziri tu ...

    Big Up Mr President

    ReplyDelete
  4. Unayosema mchangiaji wa pili ni kweli lkn. Huyo jamaa ni 'noma' fitna yake kubwa hakuna anaeiweza! huyo sio mtu wa kumchukulia hatua kienyeji.
    Tazama mwenyewe, kila awamu yumo, akiachwa kidogo anarudishwa asije akaharibu!

    Mm naskitika kwamba mawaziri wa wizara hii hawafanyi kazi zao, kwa mfano: sasa hivi, inasemekana tume ya UHAULISHAJI imemaliza muda wake karibia mwezi wa tatu sasa na hii huchaguliwa na Mh.Rais baada ya kushauriana na Mh.Waziri na hadi hii leo waziri hajafanya kazi yake!

    Kwa maana hiyo sasa hivi Z'bar huwezi kuuza wala kununua shamba, kiwanja au nyumba kwa 'document' halali na SMZ inaendelea kukosa mapato!
    Au na hili ndugu zangu ,ni tatizo la muungano kama anavyosema ustadh FARID wa UWAMSHO?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shamhuna kinachomsaidia ni Udonge wake na sio kingine. Maraisi wengi huhise kuwa wanahitaji kulipa fadhila za watu wa Donge kwa kubakia kuichagua CCM. Sasa kila Raisi anakuwa hana hila isipokuwa kumpa nafasi. Lakini mara watu wa Donge watakapoacha kumchagua kuwa mwakilishi wao basi utakuwa ndio mwisho wa kupata nafasi za juu.

      Lakini naihurumia Wizara ya Elimu. Hii wizara pia ni nyeti na ni muhimu kwa kutuletea wataalamu lakini maskini mara nyingi wizara hii haipewi mtu mathubuti. Sijui kama tutafika kwa mwendo huu wa kulindana na kutokuwa serio.us katika teuzi hizi

      Delete
  5. huyo mzee mnaemuongelea ni noma huyo...ardhi yetu ya Zanzibar takriban yote wamegawana yeye na mafisadi wenzake na Rais Dk sheni kwa hili tunakuomba ulifuatilie kuwa akina Shamhuna na wenzake waanze kurejesha ardhi za wa Zanzibari wanyonge.
    Niliomba kiwanja kule Tunguu tokea 2004 na kufuata utaratibu na sheria ki serikali lakini hadi hii leo bado kiwanja sijapata huko Tunguu.

    Nasikia vimetolewa kwa wakumbwa wa SMZ na familia zao tu mpaka watoto wadogo wameandikishwa wakati hata miaka 18 hawajafika.

    wakati kuna Wa Zanzibari wengi tu walitaka kujenga huko tuwe na mji mpya na sisi lakini viwanja hawakupata.

    MAFISADI WOTE HAPA ZANZIBAR WANA MWISHO WAO NA M/MUNGU YUPO PAMOJA NA SISI MPAKA KIELEWEKE.

    Tembeleeni website hii Skyscrapercity/westland kenya, kigali rwanda, luanda Angola,Addis Ababa, Khartoom Sudan... muone wenzetu walivyozidi kuendelea kujenga miji mipya kila leo nchi zao sasa hivi utadhania uko Mtoni.

    ReplyDelete
  6. Matatizo ya namna hii(ukosefu wa viwanja vilivyopimwa)yamesababisha watu wenye uwezo, kujenga vighorofa katikati ya mitaa ya 'uswahilini' mfano, Jang'ombe kwa chimbeni,M/ladu ,Mikunguni,Magomeni,mitaa ya kwaboko n.k.

    Sijui watu wa mipango miji hawapo au sheria ndio zinaruhusu? Mimi naamini kama si roho mbaya za Wahadimu sasa hivi Tunguu ingekua inanh'ara!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.