Habari za Punde

Taarifa Fupi ya Dkt Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Wakati wa Mazungumzo na Waandishi wa Habari

TAARIFA FUPI YA MHESHIMIWA DKT. MWINYIHAJI MAKAME WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI WAKATI WA MAZUNGUMZO YA ANA KWA ANA NA WAANDISHI WA HABARI, TAREHE 13 FEBRUARI 2012.

1. Utangulizi

Kwa mara ya kwanza naanza kukutana na waandishi wa habari kuzungumza nao ana kwa ana juu ya mambo ya msingi yanayohusu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (ORMBLM). Utaratibu huu utakuwa endelevu ambapo kwa kupitia vyombo vya habari wananchi wataweza kupata taarifa mbali mbali zinazohusu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Taarifa hii fupi inaelezea juu ya muundo wa ORMBLM, majukumu yake ya msingi, malengo yake kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, utekelezaji kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka, mafanikio iliyoyapata tokea kuanza kwa awamu hii ya Saba, changamoto inazokabiliana nazo na namna ya Serikali ilivyojipanga kukabiliana na changamoto hizo.


2. Muundo wa ORMBLM

Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imeongezewa majukumu ya Serikali za Mitaa, Tawala za Mikoa, Idara Maalum pamoja na Wazanzibari waliopo nchi za nje (Diaspora). Hatua hii imekusudiwa kuongeza ufanisi na usimamizi mzuri wa shughuli za Serikali katika kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo ya haraka na endelevu..

Katika hali ya sasa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inatekeleza mipango na mikakati yake kupitia Idara na Vitengo kumi na moja (11) vifuatavyo:-

i) Ofisi ya Faragha ya Rais.
ii) Ofisi ya Baraza la Mapinduzi
iii) Idara ya Mipango, Sera na Utafiti.
iv) Idara ya Uendeshaji na Utumishi.
v) Idara ya Mawasiliano Ikulu.
vi) Kitengo cha Usalama wa Serikali (GSO).
vii) Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho.
viii) Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Shughuli za Wazanzibari Waliopo Nchi za Nje (DIASPORA).
ix) Idara ya Uratibu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
x) Idara ya Uratibu Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
xi) Ofisi ya Afisa Mdhamini.

3. Majukumu ya ORMBLM

Katika kutekeleza shughuli zake za kila siku, ORMBLM inamajukumu ya msingi ambayo huwa yanaekewa malengo ya muda mrefu na muda mfupi, Ofisi hii imeendelea na utekelezaji wa majukumu hayo kupitia malengo iliyojipangia ili kuweza kufikia azma yake ya kuendeleza utawala bora na kutoa huduma bora kwa jamii. Miongoni mwa majukumu yake ya kila siku ni pamoja na:-

a) Kuimarisha na kusimamia utekelezaji halisi wa Sera na Mipango ya Kisekta
b) Kusimamia, kuratibu na kuhakikisha kwamba shughuli zote za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi zinatekelezwa ipasavyo na kwa ufanisi.
c) Kuhakikisha kuwa jamii inaarifiwa ipasavyo shughuli mbali mbali zinazofanywa na Rais wa Zanzibar kupitia njia tofauti vikiwemo vyombo vya habari.
d) Kusimamia, kuziendeleza na kuratibu kazi za Idara Maalum za SMZ
e) Kuratibu ushirikiano wa kikanda na wa kimataifa, uhusiano wa kimataifa na mambo yanayohusu Wazanzibari wanaoishi nchi za nje.
f) Kusimamia na kuratibu utekelezaji wa majukumu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
g) Kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Usajili wa Vitambulisho vya Wazanzibari Wakaazi
h) Kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Usalama wa Serikali (GSO)

4. Malengo kwa Mwaka wa Fedha wa 2011/2012

Utekelezaji wa malengo kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha, ORMBLM umezingatia Mipango ya Kisekta iliyowekwa katika Dira 2020, Malengo ya Maendeleo ya Milenia, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUZA II) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010-2015. Aidha, vipaumbele vimewekwa katika mambo yafuatayo:-

a) Kuendeleza Umoja wa Kitaifa na mshikamano
b) Kuimarisha uwezo, utoaji wa huduma ikiwemo usafishaji wa miji na uendeshaji wa Serikali za Mitaa, Mikoa na Wilaya
c) Kuimarisha na kuongeza uwezo wa Idara Maalum za SMZ
d) Kuimarisha huduma bora katika Vyuo vya Mafunzo pamoja na kupunguza msongamano
e) Kuimarisha mfungamano wa Kikanda ili Wazanzibari waweze kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na Jumuiya za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Jumuiya nyengine za Kikanda.
f) Kuwashajihisha Wazanzibari wanaoishi nchi za nje katika kushiriki na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
g) Kutoa elimu ya kujikinga na Maambukizi ya UKIMWI na VVU.

Sambamba na malengo hayo, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inaendelea na utekelezaji wa Miradi 10 ya Maendeleo. Miradi hiyo ni:-

(i) Ukarabati wa Majengo ya Ikulu na Nyumba za Serikali
(ii) Uimarishaji wa Mawasiliano Ikulu
(iii) Marekebisho ya Serikali za Mitaa
(iv) Uendelezaji Vitambulisho
(v) Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja
(vi) Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja
(vii) Mradi wa Shamba la Mfano la Mbogamboga - Bambi
(viii) Ujenzi wa Makao Makuu ya Valantia
(ix) Ujenzi wa Hospitali Mpya ya Kikosi cha KMKM
(x) Ujenzi wa Chuo kipya cha Mafunzo Hanyegwa Mchana

Aidha, ORMBLM inatekeleza Mradi wa Mpango wa Kuimarisha Huduma za Miji Zanzibar (Zanzibar Urban Service Program - ZUSP), usimamizi wa mradi huu upo chini ya Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo. Mradi huu unalenga kukarabati na kutengeneza michirizi ya Maji ya mvua, hii itapelekea kupunguza athari za kimazingira na matatizo ya jamii katika maeneo. Taratibu za manunuzi tayari zimeshaanza kwa kutangaza zabuni na hatua za tathmini zinaendelea na tunatarajia kazi za ukarabati na ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua zitaanza mwishoni mwa mwaka huu.

5. Utekelezaji Halisi wa Malengo kwa Kipindi cha Julai – Disemba 2011

Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imeweza kutekeleza malengo yake ya nusu mwaka kama ilivyojipangia kwa kufanya matengenezo muhimu katika Ikulu zilizopo Unguja, Pemba na Dar e Salaam. Ofisi imeendelea kusimamia huduma za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar ili aweze kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

Katika kipindi Julai - Disemba, ORMBLM imeweza kuanzisha Website ambayo inatoa taarifa mbali mbali zinazotekelezwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar pamoja na idara na vitengo mbali mbali vya Ofisi hii. Aidha, Ofisi hii imenunua samani na vitendea kazi vikiwemo meza, viti, makabati, komputa, vespa, vifaa vya kuandikia. Aidha, wafanyakazi kutoka Idara tofauti wamejengewa uwezo kwa kupatiwa masomo ya muda mrefu na mfupi pamoja na kuwezeshwa kuhudhuria semina mbalimbali za kuimarisha uwezo wao wa utendaji kazi.

Katika juhudi za kukuza mashirikiano ya kikanda na kimataifa, Ofisi imeweza kuratibu shughuli mbali mbali ikiwemo kuhudhuria vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Aidha, utekelezaji wa Juhudi za kuwashirikisha Wanzanzibari wanaoishi nchi za nje (diaspora) nalo lilipewa kipaumbele.

6. Mafanikio kwa Kipindi cha Julai-Disemba 2011

Katika jitihada za utekelezaji wa majukumu ya msingi ya ORMBLM kwa kipindi cha miezi sita iliopita imepiga hatua na kuleta mafanikio yafuatayo:-

a) Kuandaa rasimu za awali za Mpango Mkakati wa ORMBL na ya Diaspora
b) Kuanzisha tovuti ya ORMBLM
c) Kutoa majarida mawili na kipeperushi kimoja
d) Kufuatilia utekelezaji wa ahadi za Rais
e) Kuanzishwa Mahkama ya Rufaa ya Idara za SMZ.
f) Kuanzisha utaratibu wa waandishi wa habari kuzungumza na Mheshimiwa Rais.
g) Kuimarisha Vyuo vya Mafunzo kiutendaji
h) Kuwepo kwa soko huru la bidhaa na huduma katika nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki
i) Wazanzibari wanaoishi nchi za nje (diaspora) wameanza kuchangia na kuekeza katika sekta za kijamii
j) Kuiwezesha Zanzibar kuandaa semina kuhusu fursa zitokanazo na Soko la Pamoja la Jumuia ya Afrika Mashariki
k) Uratibu wa tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa umeimarika
l) Ujenzi wa jengo jipya la Makao Makuu ya Valantia

7. Changamoto

Licha ya mafanikio yaliofikiwa bado ORMBLM inakabiliwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku, changamoto hizo ni pamoja na:-

a) Uhaba wa vitendea kazi (vyombo vya usafiri, kompyuta, mashine ya kuchapia, kurikodia na za vipaza sauti).
b) Uhaba wa watendaji wataalamu kulingana na kada zinazohitajika kwa baadhi ya Taasisi za ORMBLM.
c) Ukosefu wa nafasi za kufanyia kazi (office space)
d) Watumishi wa Serikali kutoelewa dhana na majukumu ya Kitengo cha Usalama wa Serikali ( GSO)
e) Ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya ulipaji kodi kwa wanajamii kunakopelekea lengo la makusanyo ya mapato kutofikiwa kama taasisi husika zinavyojipangia kwa baadhi ya Halmashauri za Wilaya na mabaraza ya miji.
f) Tabia walionayo wanajamii juu ya usafi wa mji kwamba wao hawahusiki na kubeza juhudi za watendaji.
g) Uelewa mdogo wa wananchi kupasha habari kwa haraka juu ya majanga yanapotokea pamoja na kutoa taarifa zisizo sahihi juu ya majanga hayo.
h) Mlundikano wa mahabusu.
i) Muingiliano wa majukumu baina ya Serikali za Mikoa na Wilaya kwa upande mmoja na Serikali za Mitaa.
j) Utata katika ukusanyaji mapato baina ya Taasisi za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

8. Mikakati ya Kukabiliana na Changamoto

a) Kuandaa vipaombele katika bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2012/2013
b) Kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR/UUB) kuajiri wafanyakazi wapya kwa mujibu wa mahitaji ya wataalamu hao (wataalamu hawa zaidi katika Mikoa, Wilaya na Halmashauri).
c) Kujenga jengo jipya katika eneo la Mazizini lenye ghorofa nane litakalotumiwa na ORMBLM na OR/UUB.
d) Kutoa elimu kwa watumishi kwa kutumia sheria mpya ya utumishi wa umma ya mwaka 2011
e) Kuendeleza mazungumzo na Bodi ya Mapato kuhusu kutoa elimu ya ulipaji kodi sambamba na kupatiwa wataalamu wa fani hio ili wafanye kazi katika Halmashauri na Mabaraza ya Miji.
f) Kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuweka mji safi pamoja na kuanzisha kanuni na taratibu za adhabu kwa wanaoharibu usafi wa mji
g) Kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia vipindi vya redio na TV juu ya umuhimu wa kuripoti taarifa za majanga yanapotokea kwa haraka na kwa usahihi. Aidha kufanya mazungumzo na Makampuni ya simu za mkononi ili kusajili simu zote kwa lengo la kudhibiti tabia ya kutoa taarifa za majanga ya uongo.
h) Kufanya mazungumzo na uongozi wa Mahkama kwa lengo la kuishauri kuendesha kesi kwa haraka na ikiwezekana watumie muda wa ziada katika kuendesha kesi hizo.
i) Kuandaa sera ya Serikali za mitaa na kuandaa sheria mpya itakayosimamia uendeshwaji wa Serikali za mitaa.
j) Kushirikisha vikundi vya jamii (CBO) na (NGOS) kutoka katika wadi zote katika kusaidia huduma za taka kutoka Majumbani hadi sehemu zilizotengwa
k) Kuangalia uwezekano wa kubinafsisha baadhi ya huduma za usafi kwa kutumia makampuni binafsi.
l) Kuanzisha mipango ya matumizi ya taka kwa kujenga “compost” na “Recycling plant” ili kupunguza gharama za utupaji taka kwa kuzingatia kuwa zaidi ya asilimia 86 ya taka hizo ni mboji (Organic).
m) Kutoa taaluma ya afya na usafi wa mji kwa jamii kupitia ZBC Redio na TV
n) Kuhamasisha vikundi vya jamii (CBO) katika kila wadi kwa mashirikiano na masheha na madiwani kufanya operesheni za mara kwa mara za usafi.
o) Manispaa kufanya operesheni maalum ya usafishaji mitaro yote ya mjini katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya mvua za Masika kuanza na kuandaa kikundi maalum cha dharura wakati wa msimu wa mvua za masika.
p) Kuandaa operesheni maalum ya kukamata waanyama wanaozurura ovyo mijini kwa mashirikiano na vikosi vya SMZ, Halmashauri na Manispaa
q) Kuunda kamati maalum ya wizara ikiongozwa na mkuu wa wilaya katika kutumia njia bora za busara za kudhibiti wanyama hao bila ya kuleta malumbano na wananchi

9. Hitimisho

Kimsingi huu ndio muonekano wa ORMBLM kuanzia muundo wa Ofisi, majukumu ya kila siku yanayotekelezwa, vipaumbele katika utekelezaji wa malengo, mafanikio yaliofikiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja sambamba na changamoto za kiutendaji pamoja na mikakati iliyowekwa inayolenga kukabiliana na changamoto hizo.

Ndugu waandishi wa habari asanteni kwa kunisikiliza


(Dkt. Mwinyihaji Makame)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.