Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Fatma Hamadi Rajabu amesema Serikali itaendelea kujali na kuthamini misaada inayotolewa na Taasisi binafsi.
Ameyasema hayo mara baada ya kukabidhi Pikipiki (Bodaboda) 13 kutoka Kampuni ya Adem Store ambazo ni kwa ajili ya Idara ya maendeleo ya Vijana Zanzibar.
Amesema Pikipiki hizo, zitasaidia kuondosha changamoto mbalimbali za usafiri, zinazojitokeza kwa Watendaji wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar ambapo zitatolewa kwa Wilaya zote za Zanzibar.
Aidha amesema, hatua hiyo ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwawezesha Vijana kiuchumi na kufanya kazi kwa Ufanisi.
Mbali na hayo amesema licha ya kuwa idara husika imehamishiwa Wizara nyengine, mchakato wa upatikanaji wa Pikipiki hizo, ulianzia katika Wizara ya Habari, hivyo kampuni imekabidhi kwa Wizara hiyo kabla ya kukamilishwa kwa taratibu za ugawaji.
Kwa upande wake, Ofisa Manunuzi wa Wizara hiyo, Asha Aboud Simai, amesema Wizara imekusudia kuhakikisha Vijana wanapata nyenzo za kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya Usafiri.
Hata hivyo amesema kuwa hatua hiyo, imeelezwa kuwa ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuwajengea uwezo Vijana wa kujiajiri na kupunguza changamoto ya ajira nchini.
Pikipiki hizo, zimetolewa na Kampuni ya Adem Store baada ya kushinda tenda ya kusambaza, zimegharimu zaidi ya sh. Milioni 57 na zinatarajia kutolewa kwa Wilaya za Unguja na Pemba.
Imetolewa na Kitendo cha Habari,
WHSUM.


No comments:
Post a Comment