Habari za Punde

Kamati Yambana Mvuna msitu wa Hifadhi

Na Haji Nassor, PEMBA

WAKAAZI wa kijiji cha Msiakwe Shehia ya Wambaa, wamemlalamikia mwananchi mwenzao Khamis Hamad kutokana na uvunaji wa misitu kwa maslahi yake, huku ikizingatiwa kuwa msitu huo ni wa hifadhi ya Kangaale.

Walisema kuwa licha ya kuonywa mara kadhaa mwananchi huyo kupitia vikao vya kamati ya Hifadhi, lakini amekua akijitoa mshipa wa fahamu na kuendelea kuvuna magogo mabichi na kisha kupiga mkaa.

Wakizungunza na waandishi wa habari katika ziara maalum, wananchi hao walisema Khamis Hamad amekua akiendelea na tabia yake ya kukata miti na magogo kisha kupiga mkaa na kutoa lugha zisizonzuri anapokatazwa.

Juzi kwenye kikao cha kamati ya Hifadhi ya Msitu huo, kilichofanyika Kituo cha Afya cha Wambaa, ambapo mwananchi huyo aliitwa alisema alikiri kuendesha hujuma hizo na kuomba msamaha.

Alisema kwa sasa anatarajia kuacha kazi hiyo lakini akaomba mbele ya Kamati hiyo kwamba, kuni korja 30 alizokushazikata aachiwe akauzi ili amalize matatizo yake ya kifamilia jambo ambalo halikukubaliwa na Kamati hiyo.

“Naomba radhi na sasa nimesikia na kutambua dhamira yenu ya kuhifadhi, lakini kwa haya magogo ambayo nimeshayakata naomba niachiwe maana nna matatizo yangu ya kifamilia, hivyo naomba niyakamilisha kisha sikati tena’’, alijitetea

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Makame Haji alisema kwa vile hilo sio kosa la mwanzo la kuitwa mbele ya kikao na kuomba radhi kisha kuendelea na hili huwezi kusamehewa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Haji Mohamed Ali alisema mtuhumiwa huyo hapaswi kusamehewa maana alishawahi kukamatwa na kutozwa faini ya shilingi 50,000/= na kulipa shilingi 30,000/= na bakaa kushindwa kuilipa.

Nae Katibu Mohamed Omar alisema kama akiachiwa itatoa fursa kwa wengine kuendesha hujuma hizo kwa vile wanajua kwamba unaitwa kwenye vikao na kupigwa faini ndogo na kuendelea na kazi.

Msitu wa Kangaale wenye ekari zaidi ya 150, kwa sasa unahifadhiwa na wanakijiji cha Msiakwe shehia ya Wambaa na Shehia ya Mgelema kutokana na utata wa umiliki wa Msitu huo huku juhudi za kutatua hilo zikiendelea.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.