Na Salum Vuai, Maelezo
MAADHIMISHO ya sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day) hapa Zanzibar, yanatarajiwa kuanza kesho kwa shughuli mbalimbali.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) Khamis Mwinyi Mohammed, alisema tayari kamati nne zimeundwa kushughulikia maadhimisho hayo.
Katika mkutabno wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake Kikwajuni, Katibu huyo alizitaja kamati hizo kuwa ni ile ya fedha,maandamano, maonesho na michezo, ambazo zimeanza kazi tangu Machi 15.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na shirikisho hilo, maadhmisho hayo yataanza kwa ufunguzi wa tamasha la michezo litakalofunguliwa na waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo.
Aidha tarehe 27 mpaka 30, Aprili, kutakuwa na usafishaji mazingira katika maeneo kadhaa utakaohusisha wanachama wa vyama vya wafanyakazi na viongozi wao.
Mohammed aliyataja maeneo ambayo yatafanyiwa usafi kuwa ni hospitali ya Mnazimmoja, nyumba za wazee Sebleni, hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongochekundu pamoja na ofisi za ZATUC Kikwajuni.
Katibu huyo alisema maonesho ya bidhaa mbalimbali yataanza Aprili 29 na kumalizika Mei 2, yatakayofanyika viwanja vya nje Amaan, ambapo yanatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.
Katibu huyo alisema kilele cha sherehe hizo kitafanyika Mei Mosi kwenye uwanja wa Amaan ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amepangwa kuwa mgeni rasmi.
Kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu, Mohammed alisema itakuwa “Mfumko wa bei, kodi kubwa na mishahara duni ni pigo kwa wafanyakazi”.
Aliwaomba wafanyakazi, wanachama wa ZATUC na wananchi wote kwa jumla, kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo.
No comments:
Post a Comment