Ramadhan Makame na Madina Issa
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Kamisheni ya Utalii Zanzibar itekeleza wajibu wake wa msingi ambao ni kukuza utalii nchini utakaoongeza pato la nchi, badala wafanyakazi wake kugombania safari za nje.
Wajumbe hao walieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi liliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar walipokuwa wakichangia mswada wa mabadiliko ya sheria ya Kamisheni ya utalii.
Akichangia mswada huo, Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alisema kamisheni hiyo ina wajibu mkubwa wa kukuza utalii jambo ambalo halijafanyika kama inavyotakiwa.
Alisema inashangaza kuona viongozi wa kamisheni hiyo kutofanya wajibu wake na badala yake wamekuwa wakigombania safari za nje hadi kufikia hatua ya kununiana.
“Kamisheni ya Utalii ibadilike ifanye kazi yake ya kukuza utalii na sio kugombaniana safari za nje na kufikia hatua ya kununiana”, alisema Jussa.
Aidha alisema Zanzibar inapaswa kubadilika kwa kukaribisha watalii wa daraja la juu kuliko ilivyo hivi sasa kukumbatia watalii wa daraja la chini ambao mchango wao katika pato la nchi umekuwa mdogo.
Akizungumzia suala la kuvuja kwa mapato ya utalii, alisema ni vyema utitiri wa taasisi zinazokusanya mapato ukaondolewa na kuwepo taasisi moja, ambayo itasaidia kutovuja mapato hayo kama ilivyo hivi sasa.
Mwakilishi huyo alipendekeza pawepo utaratibu mahususi ambao utahakikisha utalii unawanufaisha Wazanzibari kiajira kwani hivi sasa zaidi ya asilimia 80 ya walioajiriwa si Wazanzibari.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma alisema Zanzibar haijanufaika na utalii kama nchi nyengine za visiwa vinavyofanana na Zanzibar kama Seychelles na Mauritius.
Alisema tatizo kubwa liliopo ni kutokuwepo kwa udhibiti wa wageni jambo linalofanya ajira nyingi hata zile zinazoweza kufanywa na vijana wa Zanzibar kuchukuliwa na watu wa nje.
“Suala la ajira tuliwekee mikakati, tujue tuna hoteli ngapi lakini pia nafasi za ajira wapewe Wazanzibari, haiwezekani ajira zifanywe kiholela, mikataba hamna watu wanafukuzwa kazini kama kuku, hii haikubaliki”, alisema.
Mwakilishi huyo alisema utalii umekuwa ukiharibu maadili hasa Nungwi, kwani huwekwa ngoma ufukweni wakati wa usiku (full moon), ambapo mchezo na mavazi yanayovaliwa hayalingani na maadili ya Zanzibar.
Naye Subeit Khamis Faki (Micheweni), alisema Wazanzibari wenyewe ndio wanaosababisha watalii wavunje mila na utamaduni wa visiwa hivi, kwani hawawasisitizi kufuata sheria zilizopo hasa mavazi.
Aidha Mwakilishi huyo wa Micheweni alilalamikia tatizo la vitambulisho vya Uzanzibari kutolewa ovyo kwa wageni jambo linalowasababishia kupata vyeti vya kuzaliwa na kukomba kazi kwenye sekta ya utalii.
“Kwa nini mtu kaja Zanzibar kwa ajili ya ulinzi tu halafu apewe kitambulisho cha Mzanzibari, naomba tuangalie leo na kesho haiwezekani mambo haya kuachiliwa yanaweza kutuletea athari hapo baadae”, alisema Subeit.
Kwa upande wake Mgeni Hassan Juma (Viti Maalum) alisema isikubalike na wasiruhusiwe wawekezaji kujenga ufukweni kwani ni kinyume na sheria na wasiogopwe lazima waelezwe katika kuifuata sheria.
Alishangazwa kufumbiwa macho suala la udhalilishajwi na unyanyaswaji wanayofanyiwa wafanyakazi wa hoteli za kitalii hasa wanawake, unaofanywa na wageni.
Mswada huo uliwasilishwa juzi na waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdillahi Jihad Hassan kwa niaba ya waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo.
No comments:
Post a Comment