Joseph Ngilisho na Mahmoud Ahmad, ARUSHA
MAHAKAMA Kuu kanda ya Kaskazini jana imetengua kiti cha Ubunge katika jimbo la Arusha mjini, kilichokuwa kikikaliwa na Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema.
Mahakama hiyo imetengua matokeo ya kiti hicho kufuatia uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka juzi, baada ya kubaini kukiukwa sheria za uchaguzi pia mahakama hiyo ikimuamuru Lema kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua muda wa saa moja na robo kuanzia saa 3.10 hadi saa 4.15 za asubuhi ya jana, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Gabriel Rwakibarila alisema kuwa katika ya malalamiko kumi yaliyowasilishwa na upande wa walalamikaji, malalamiko mawili yametupwa huku malalamiko 8 yakimtia hatiani Lema.
Alisema kuwa mahakama baada ya kupitia malalamiko yote iliridhika kuwa katika mikutano 60 ya kampeni za Lema, matukio manane kati ya kumi yalikiuka maadili ya kampeni.
Alisema kutokana na hali hiyo, Mahakama imeridhika na ushahidi uliowasilishwa na hivyo kuamuru kubatilishwa kwa matokeo ya Ubunge yaliyompa nafasi ya kuchaguliwa kwa Godbless Lema.
Jaji Rwakibarila alisema kuwa malalamiko mawili ya udini na ukaazi yaliyowasilishwa na walalamikaji hayakuwa na tija hivyo mahakama imeamua kuyatupa.
Aidha malalamiko manane ya udhalilishaji wa kijinsia na kashfa, mahakama imeridhika kuwa Lema alikiuka sheria na kanuni za uchaguzi, hata hivyo Jaji huyo alieleza kuwa nafasi ya kukata rufaa kwa Lema iko wazi endapo hakuridhika na hukumu hiyo.
Awali kabla ya hukumu Jaji alitaja baadhi ya malalamiko kati ya manane ya udhalilishaji wa kijinsia na kashfa aliyoyatoa Lema wakati wa kuomba kura dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda Buriani.
Miongoni mwa maneno ambayo yaliwasilishwa mahakamani hapo ambayo Lema aliyatamka wakati wa kuomba kura ni pamoja na kuwaambia wananchi kuwa wakimchagua Dk. Batilda atahamia Zanzibar kwa mume wake na kulitelekeza jimbo.
Jaji Rwakibarila aliyataja malalamiko mengine kuwa, Dk. Batilda sio mwaminifu kwani ana mimba ya mzee wa Monguli (Edward Lowasa) na atazaa nje ya ndao, pia chungeni sana wanaovaa vilemba msije mkachagua al-Qaida, mila za kichaga na kiarusha ni mwiko kuongozwa na mwanamke, mkimchagua Dk. Batilda atafunga kituo cha radio cha Safina.
Kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2011 ilifunguliwa mwaka jana na wanachama watatu wa CCM, Musa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo dhidi ya Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema wakiitaka mahakama uibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mbunge huyo.
Katika kesi hiyo upande wa walalamikaji uliongozwa na Mawakili, Alute Mungwai na Akida Modest huku upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Method Kimomogolo na Juma Masanja ambaye ni wakili wa serikali mwandamizi kutoka mkoa wa Tabora.
Naye Lema alisema kuwa pamoja na kutenguliwa Ubunge wa jimbo la Arusha mjini bado yeye ndiye, mbunge na hata kama uchaguzi utarudiwa ni wazi kuwa yeye ndiye atakayeshinda ingawaje hizo ni mbinu za viongozi wa juu Taifa la Tanzania.
Aliongeza kuwa Mahakama kupitia kesi yake imeonesha wazi jinsi ambavyo wanavyobaka demokrasia na suala hilo litawapeleka watu katika misitu bila kupenda na pia nchi itaingia katika machafuko.
“Ninachoweza kusema nina moyo mkubwa sana kwani mimi nimepita katika mapito ya hali ya juu sana na pia aliyeniweka madarakani ni Mungu na wala sio hao viongozi wa ngazi za juu na ninapenda kuwatia moyo kuwa hii hukumu ya kutengenezwa kama siyo ya kutengenezwa imekuwaje kila kiongozi anajua hii hukumu kuanzia juzi na jana”, alisema Lema.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema kuwa hiki ni kipindi kigumu sana kwao na pia ni kipindi cha mpito, pamoja na kuweka jazba pembeni badala yake chama hicho kinatakiwa kuonesha dunia, mahakama jinsi haki inavyopatikana.
Mbowe alisema kuwa chama hicho hakiwezi kukataa ama kukuabali hukumu ya mahakama badala yake kinalenga kutafuta haki siku ya Jumamosi katika viwanja vya NMC jijini hapa ambapo pia watashahuriana kabla na kutoa tamko.
“Mimi naisheshimu sana mahakama kwa kuwa ina taratibu zake za msingi na kwa hali hiyo nawasihi sana wananchi kuwa watulivu kwa siku hizi mbili mpaka Jumamosi tutatoa hatma yetu kama tutakata rufaa au laa na baada ya kushahuriana na viongozi na wanasheria wetu wa chama”, alisema Mbowe.
Kwa upande wa walalamikaji, ambaye aliongea kwa niaba ya wenzake Happy Kivuyo alisema kuwa mahakama imefanya uamuzi wa hali ya juu sana na imeonesha haki kwa kuwa Lema alikuwa anatoa lugha za matusi na kuzalilisha sana.
“Napenda niwaambie wakazi wa mji wa Arusha kuwa malalamiko yetu hayakuwa ya kuchonga ila yalikuwa ni ya msingi wa hali ya juu sana na kwa hali hiyo mahakama imefanya uamuzi wa hali ya juu sana”, alisema Happy.
No comments:
Post a Comment