Habari za Punde

Machano Akabidhi Fedha Zote Mfuko wa Jimbo kwa Kamati

Na Khamis Mohammed

MWAKILISHI wa Jimbo la Chumbuni, Machano Othman Said, amewataka wanafunzi waliofuzu kuingia mchipuo na kidato cha tatu kujipanga vizuri kwa elimu ya juu zaidi katika kujenga mustakabala mwema wa kielimu katika maisha ya baadaye.

Hayo aliyaeleza wakati wa sherehe fupi za kuwapongeza wanafunzi 81 waliofanikiwa kuingia kidato cha tatu na wengine 17 waliofuzu mchipuo huko katika Skuli ya Mwembemakumbi, wilaya ya Mjini juzi.

Mwakilishi huyo ambaye pia ni Waziri asiye na Wizara Maalum wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema, vijana hao hao wana kila sababu ya kujivunia mafanikio hayo huku wakielewa kazi kubwa iliyopo mbele yao ya kupata elimu zaidi.

"Elimu ya kidato cha nne au cha sita hivi sasa haikidhi ushindani wa kielemu, tunatakiwa kufanya kazi kubwa zaidi na kufikia angalau shahada ya kwanza au pili".

"Hii ni kwa sababu hivi sasa tunaelekea katika ushindani wa soka huria la Afrika Mashariki ambalo litakuwa na ushindani mkubwa wa kielimu na ajira, hivyo elimu ndiyo itakayokufanyeni muingie katika ushindani huu".

"Nafsi za ajira zitakuwa kwa watu wote wa ukanda huu, Mganda, Mkenya, Mnyarwanda, Mrundi watakuja hapa kutafuta ajira, bila ya elimu ya ngazi ya juu, hatutaweza kumudu ushindani", alisema Mwakilishi huyo.

Hivyo, Mwakilishi huyo, aliwataka wanafunzi hao kuejiepusha na vishawishi ambavyo vitapelekea kuharibu malengo yao ya kielimu na kuharibikiwa kimaisha.

Wakati huo huo, Mwakilishi huyo, alikabidhi shilingi milioni 10 za mfuko wa maendeleo ya Jimbo kwa uongozi wa kamati ya maendeleo ya Jimbo la Chumbuni ikiwa ni katika kutekeleza kwa vitendo azma ya serikali kwa maendeleo ya wananchi wake majimboni.

Kati ya fedha hizo, shilingi milioni mbili na laki tano ni kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya Skuli ya Mwembemakumbi huku fedha nyengine zaidi ya shilingi milioni mbili ambazo zinatarajiwa kutumika kwa kuweka kifusi katika moja ya barabara ya jimbo hilo.

Fedha nyengine shilingi milioni tano zitatumika kulipia deni la uchimbaji wa kisima cha maji ambacho kitahudumia wananchi wa Jimbo hilo katika kukabiliana na tatizo la maji.

"Sisi viongozi wenu wa Jimbo mliotuchagua, tutahakikisha tunaendelea kusimamia maendeleo ya Jimbo na kuwatumikia wananchi wakati wote".

"Mimi kama Mwakilishi na wenzangu Mbunge na Madiwani, tutashirikiana kuhakikisha Jimbo hili linaondokana na kero zote zinazowakabili wananchi wetu".

Aidha Mwakilishi huyo aliahidi kuzitafutia ufumbuzi baadhi ya kero katika skuli hiyo ikiwemo ya ukosefu wa vikalio, ukosefu wa mashine ya fotokopi, udogo wa maabara na maktaba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.