Habari za Punde

Waziri: Msifiche Takwimu Mnazozikusanya

Na Salum Vuai, Maelezo

OFISI ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, imeshauriwa kuanzisha kitengo cha habari na mawasiliano, ili takwimu inazozizalisha ziweze kuzifikia sekta za umma kwa ajili ya kuzifanyia kazi.

Ushauri huo umetolewwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee katika mkutano wake na wafanyakazi wa ofisi hiyo ulifanyika hoteli ya Bwawani.

Waziri huyo alisema, kuzalisha takwimu pekee hakutoshi kama zitakuwa hazitumiwi na watu wanaopaswa kuzitumia kwa manufaa ya umma.

Ili hilo liwezekane, alisisitiza kuwepo ushirikiano wa kutosha kati ya watendaji wa ofisi ya takwimu na sekta za serikali ambako ndiko takwimu hizo zinakohitajika kwa ajili ya kupanga mambo mbalimbali ya maendeleo.

"Tumekuwa tukifanya 'surveys' nyingi na za aina mbalimbali, lakini tunapaswa kuwaelimisha watumiaji ili wazijue takwimu za tafiti tunazofanya ili waweze kuzitumia, vyenginevyo kazi yetu haitakuwa na faida yoyote", alifafanua.

Aidha, alihimiza matumizi ya vyombo vya habari katika kuelimisha jamii juu ya kazi zifanywazo na Ofisi ya Mtawimu Mkuu wa Serikali, ambavyo vipo kuuhudumia umma.

Akitoa mfano, alisema umuhimu wa takwimu za vifo ni kuionesha Wizara ya Afya iwapo watu wengi wanakufa kwa maradhi yanayofanana katika eneo moja, ili iweze kujipanga katika kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

Waziri huyo alielezea pia umuhimu wa kusambaza elimu kuhusu zoezi la sensa ya watu inayotarajiwa ufanyika Tanzania nzima mwezi wa Agosti mwaka huu, ili wananchi wajue kinachoendelea na hivyo kujiweka tayari kwa ajili ya kuhesabiwa.

Alisema kuwa muda uliobaki kabla kufanyika kwa sensa hiyo ni mdogo, hivyo iko haja kuanza maandalizi sasa kwa lengo la kuifanya jamii itambue umuhimu wa sensa hiyo na lini itafanyika, ili kwa wale ambao hawatakuwa na dharura kubwa wabaki majumbani kusubiri watakwimu.

Mzee pia alisisitiza haja kwa ofisi hiyo kuweka mkazo katika kuwaendeleza wafanyakazi wake ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na pia kuchukua nafasi za watakwimu wakongwe wanaomaliza muda wao wa utumishi au wale wanaohamishiwa katika sekta nyengine.

"Viongozi msiwe wachoyo, wachieni vijana wakasome, mtu asiseme 'mimi kiongozi sina hata diploma', vipi nimpeleke mtu akachukue 'master' au PHD, lazima tujiandae kuzalisha damu mpya ya watakwimu", alisisitiza Waziri huyo.

Nao wafanyakazi wa ofisi hiyo walimuomba waziri huyo atumie nafasi yake kukutana na wenzake wa wizara nyengine, ili kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utendaji wao.

Walizitaja baadhi ya changamoto wanazopambana nazo, ni pamoja na kutothaminiwa katika baadhi ya ofisi, wakidai pia hunyimwa posho na semina za mafunzo, licha ya kufanya kazi pamoja na wadau wa ofisi hizo.

Aidha walisema kumekuwa na upotoshaji wa takwimu zinazotolewa na baadhi ya taasisi, kwani vyanzo hivyo hutoa idadi isiyolingana hasa katika sekta ya utalii, ambapo Idara ya Uhamiaji na Kamisheni zimekuwa na takwimu zinazogongana.

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mohammed Hafidh, alisema ofisi yake inajitahidi kuwasomesha watendaji wake kadiri inavyowezekana, na kwamba sasa idadi kubwa wako masomoni nsa wengine wamesharudi.

Aidha alisema Ofisi yake kwa kushirikiana na Bodi, wameandaa mfumo wa mishahara na maslahi mengine kwa ajili ya wafanyakazi wake ili kuwaongezea ari ya kuwajibika kama inavyotakiwa.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.