Na Madina Issa
JUMUIYA ya Zanzibar Outreach Program (ZOP) inayosaidia jamii matibabu ya macho, koo, masikio na Presha pia wamewapatia huduma hiyo wazee wa wanaoishi Welezo, hatua iliowapa faraja wazee hao.
Mmoja wa wazee hao Khatib Omar alimueleza mwandishi wa habari hizi kuwa wamefarijika, kwa kupata huduma za madaktari hao kwa kuwa ni jambo la nadra kwao.
Alisema baada ya kupata taarifa za kuwepo madaktari hao, wazee hao walipongeza hatua hiyo na kuamini maradhi yao ya muda mrefu yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi kwa kupungua au kuondoka kabisa.
"Leo hii tumefarijika sana ndugu yangu kwa kupata matibabu kutoka kwa madaktari hawa kwani hivi sasa ni muda mrefu tumekua hatujapata matibabu ya aina yoyote, "alifahamisha mzee huyo.
Hivyo, amewataka madaktari hao wasisite kuwatembelea kila baada ya muda iliwafahamu matatizo yao na kuyapatia ufumbuzi.
Mapema Sister Calista Urassa anayewahudumia wazee hao alisema wamefarajika na ujio wa madaktari hao kwa kuwapatia huduma nzuri wazee hao, kwani wamekuwa wakisumbuliwa na maradhi tofauti.
Hata hivyo, amewataka madaktari hao waendeleze utaratibu wa kwenda kuwapatia huduma wazee hao ili matatizo yao yaweze kubainika mapema
Wakitoa shukurani kwa wazee hao Katibu wa Jumuiya ya ZOP, Dk.Naufali Kassim Muhammed aliahidi kuwa hiyo haitakuwa safari ya mwisho kwenye kituo hicho.
Mapema Mkurugenzi wa Bodi ya Goza ya Marekani, Antje Fleischer kwa kushirikiana na Mario Muellel walisema wao wapo kwa lengo la kuwasaidia wazanzibar wote wenye matatizo hususani ya ugonjwa wa aina tofauti kwenye visiwa vya Zanzibar.
Akitoa tathmini ya matibabu hayo, Dk. Salum Omar Mbarouk kutoka OPD Mnazimmoja alisema waliopatiwa tiba hiyo ni wazee 38 wakiwemo wanaume 30 na wanawake wanane.
No comments:
Post a Comment