Na Asya Hassan
PAZIA la mashindano ya Muungano kwa mchezo wa mpira wa wavu, linatarajiwa kufunguliwa leo katika uwanja wa Vyuo vya Mafunzo Kilimani mjijni Zanzibar.
Taarifa za Chama cha mchezo huo Zanzibar (ZAVA) zilizotolewa kwa vyombo vya habari na Msemaji wake Mwajuma Juma, zimefahamisha kuwa, jumla ya timu kumi zitatoana jasho kuwania ubingwa wa michuano hiyo.
Alieleza kuwa, mashindano hayo yatafungiliwa kwa pambano kati ya Magereza kutoka Dar es Salaam na Mafunzo ya Zanzibar.
Alisema kila upande kati ya Zanzibar na Tanzania Bara utawakilishwa na timu tano.
Alizitaja timu hizo za Bara kuwa ni pamoja na Magereza na Jeshi Stars zitakazokuwa na timu za wanaume na wanawake, sambamba na Mzinga ambayo itashirikisha wachezaji wanawake.
Kwa upande wa Zanzibar, alisema timu zitakazoshiriki ni Mafunzo, Zenj FM kwa wanaume na wanawake, Nyuki na Polisi.
Msemaji huyo alibainisha kuwa maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika ikiwa pamoja na kuwasili kwa timu kutoka Tanzania Bara.
Hata hivyo, Mwajuma alieleza kuwa, chama chake kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa wafadhili, ambapo hadi sasa hakuna mtu, taasisi wala kampuni yoyote iliyojitokeza kubeba gharama za uendeshaji wa mashindano hayo.
Kutokana na kukosa ufadhili, alisema bado chama chake hakina uhakika wa kupatikana kwa zawadi kwa ajili ya washindi wa ngarambe hizo.
No comments:
Post a Comment