Na Haji Nassor, Pemba
UONGOZI wa klabu ya soka ya Hard Rock inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kisiwani Pemba, umewaomba radhi wapenzi wake kwa kushindwa kuingia Ligi Kuu ya Zanzibar msimu ujao.
Hard Rock imesema kuwa, haikuwa dhamira yake kuwaangusha wapenzi wake, bali hali hiyo ilitokana na makosa madogo yaliyojitokeza siku ya mchezo wao wa mwisho na timu ya Bandari kutoka Unguja ambapo zilitoka sare ya bao 1-1.
Matokeo hayo yaliiwezesha Bandari kukata tiketi ya ligi kuu msimu ujao, ikizingatiwa kuwa ilishinda pambano la kwanza kisiwani Unguja kwa mabao 2-1, na hivyo kupata ushindi wa jumla wa mabao 3-2.
Akizungumza kwa masikitiko, Kocha Mkuu wa Hard Rock Asaa Khamis, alisema mchezo wa mpira wa miguu ni wa makosa, na hivyo wapinzani wao waliwahi kutumia fursa pale timu yake ilipoteleza na kupoteza udhibiti wa mchezo huo uliochezwa uwanja wa Gombani Pemba.
Hata hivyo, amewaomba mashabiki wao, wasahau matokeo hayo, na badala yake sasa waanze kuzungumzia msimu ujao ambao amewahakikishia kuwa watajipanga vyema ili waweze kupanda ngazi hiyo mwakani.
Baada ya Bandari kufanikiwa kupanda daraja la Ligi Kuu, imeungana na timu za Mtende Rangers pamoja na Duma inayomiikiwa na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment