Habari za Punde

Atajwa Kumrubuni Mchezaji Akane Usajili Wake

Na Ameir Khalid
MJUMBE mmoja wa Kamati Tendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa, amehusishwa na madai ya kumshawishi na kumrubuni mchezaji Othman Khamis Abeid wa timu ya Idumu SC ya Unguja Ukuu Tindini, ili akane kuwa hakusaini fomu ya uhamisho pamoja na usajili.

Mjumbe huyo (jina tunalo), ametajwa kuhusika na kitendo hicho kilichoifanya ZFA iinyang'anye ushindi timu ya Idumu na kuamuru mchezo kati yake na Bweleo SC urudiwe, kutokana na utashi binafsi.

Katika mchezo huo uliopigwa Mei 15, 2012, katika uwanja wa Mao Dzedong Idumu ilishinda kwa mabao 2-1, na kukata tiketi ya timu nne bora zitakazocheza fainali za ligi daraja la pili Taifa huku Bweleo ikitupwa nje.

Idumu imekata rufaa katika Kamati ya Rufaa na Usuluhishi ya ZFA kupitia barua yake hiyo ya Mei 24, ambayo pamoja na mambo mengine, ilimtaja mjumbe huyo maarufu katika medani ya soka Zanzibar, Tanzania na Afrika Mashariki, kuwa alimshawishi mchezaji huyo aliyelalamikiwa kuwa usajili wake haukufuata taratibu.

Katika barua yake ya rufaa iliyosainiwa na Katibu wake Mkuu, Idumu imepinga uamuzi wa Kamati Tendaji ya ZFA Taifa wa kuipokonya ushindi na kuamua mchezo huo urejewe, kwa madai kuwa hatua hiyo haikuzingatia haki bali ilisukumwa na utashi na upenzi kwa baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na mjumbe huyo aliyetajwa kumshawishi mchezaji Othman Khamis Abeid.

"Katika kikao cha kusikiliza lalamiko la timu ya Bweleo dhidi ya timu ya Idumu cha Jumanne, tarehe 22 Mei,2012, mchezaji wetu Othman Khamis Abeid alimtaja na kuthibitisha mbele ya kikao kuwa mjumbe huyo alimshawishi na hata kutaka kumrubuni kwa kiasi chochote cha fedha, ili mradi tu aseme "amesaini leseni tu na lakini hakusaini fomu ya uhamisho wala usajili", ilisema sehemu ya barua hiyo.

Uongozi wa Idumu umesema hilo peke yake ni kosa la jinai kwa kiongozi wa ngazi ya juu katika michezo kumfundisha kijana kupinda sheria na kanuni za michezo kwa makusudi, na baadae kiongozi huyohuyo ashiriki katika kikao cha kutoa maamuzi dhidi ya Idumu SC, na kusema haki haingeweza kupatikana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.