Habari za Punde

Iran Kusaidia Sekta ya habari, utalii, michezo Zanzibar

Na Mwandishi wetu

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Kiislam ya Iran, zimeunda timu ya watu wanne kufanya mapendekezo ya maeneo ambayo pande mbili hizo zitashirikiana katika sekta ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo.

Timu hiyo inajumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Dk.Ali Mwinyikai na Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho Dk.Amina Ameir Issa, ambao watasaidiana na maofisa wawili wa Iran katika kukamilisha waraka wa ushirikiano huo (MOU).


Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara ambayo imefanywa na Balozi wa Iran nchini Tanzania Morahhed Ahom, aliyemtembelea Waziri wa Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk ofisini kwake Kikwajuni mjini Zanzibar kuzungumzia masuala mbalimbali ya nchi hizo.

Morahhed amesema kwa vile Zanzibar na Iran ni nchi ambazo zina uhusiano wa muda mrefu hivyo kuna kila sababu ya Iran kuisaidia Zanzibar katika mambo ambayo yamo ndani ya uwezo wao.

Miongoni mwa mambo ambayo Iran imeahidi kuyafanyia kazi ni pamoja na kusaidia ukarabati wa magofu ya Zanzibar ambayo yamekuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka pande zote za dunia.

Kwenye suala la Michezo Morahhed amesema Nchi yake iko tayari kusaidia sekta hiyo katika fani za ukocha wa michezo mbali mbali ikiwemo mpira wa miguu, ambapo kwa kuanzia itasaidia mipira 100 ya soka ili iweze kugaiwa maskulini.

Aidha ameahidi kutoa nafasi mbili za masomo kwa maofisa wa sekta za wizara hiyo ambao wataenda kusomea taaluma ya Urithi na Utamaduni katika Jamhuri ya Kiislam ya Iran, pamoja na wahandishi wa Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), kwenda kujifunza teknolojia ya digitali.

Balozi Morahhed alitoa maelezo hayo kufuatia kuombwa na Waziri wa Habari,Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk, wakati wa mazungumzo yao.

Pamoja na mambo hayo Waziri Mbarouk pia aliiomba nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kusaidia kupatikana mtambo wa kuchapishia magazeti kwa ajili ya Shirika la Magazeti la Zanzibar ‘Zanzibar Leo’, linalochapisha magazeti yake Dar es Salaam kutokana na kutokuwepo mitambo ya kuchapishia magazeti Zanzibar.

Waziri huyo memshukuru Balozi huyo kwa ahadi zake na mashirikiano makubwa ambayo yamekuwa yakifanywa baina ya nchi hizo mbili.

Waziri Mbarouk amesema Zanzibar na Iran ni nchi ambazo zina asili na udugu mmoja hivyo kuna kila haja kuendeleza mashirikiano miongoni mwa nchi hizo mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.