Habari za Punde

Jaji Mkuu asema Mrundikano wa Mahabusu Kuondoshwa

Na Maulid Kipevu, PEMBA

JAJI MKUU wa Zanzibar, Omar Othman Makungu amesema idara ya Mahakama imo katika mikakati ili tatizo la mrundikano wa Mahabusu katika Vyuo vya Mafunzo linakwisha katika kipindi kifupi kijacho.

Amesema kumekuwa na Mahabusu wengi katika Vyuo vya Mafunzo jambo ambalo linaipa mzigo Serikali kutokana na sababu ambazo zinaweza kupatiwa ufumbuzi wake.

Jaji Makungu amesema hayo katika ziara yake ya kutembelea Vyuo vya Mafunzo kuona hali halisi ilivyo na kuyatafutia ufumbuzi ikiwemo kuona mazingira wanayoishi Wanafunzi wa Vyuo hivyo.

Akijibu hoja ya kuchelewa kwa kesi na Mwenendo wa kesi (Proceeding) Mahakamani, baada ya kumalizika kwa kesi na kuendelea kwake Mahakamani, Jaji Mkuu amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na ameahidi kulitafutia ufumbuzi ili haki iweze kupatikana hasa kwa wale wanafunzi wanaotumikia adhabu za vifungo Gerezani.

Kuhusu shutuma za Rushwa kwa watendaji wa mahakama amesema kuwa kwa sasa hatomshamilia Mtendaji yeyote wa chombo hicho atakaetajwa kuhusika na rushwa na tayari ameanza kuchukua hatua kwa baadhi yao.

Jaji Mkuu alitembelea vyuo vya mafunzo Wete, Kengeja, Tungamaa na Kangagani ambapo alikutana na kuzungumza na Mahabusu na wanafunzi wa vyuo hivyo vya Mafunzo.

Aidha katika ziara hiyo Jaji Makungu, ameahidi kuzipeleka Serikalini matatizo ambayo ameyabaini ili serikali iweze kuyafanyia kazi ikiwemo maombi ya mafunzo ya amali kwa wafungwa na kufikiriwa kupatiwa mitaji mara baada ya kumaliza vifungo vyao ili kuweza kumudu ugumu wa maisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.