Na Mwantanga Ame
KAMATI Teule ya Baraza la Wawakilishi, imefikia asilimia 80 ya kulichunguza Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), baada ya kuwahoji watendaji wa shirika hilo.
Kamati ilipewa kazi hiyo baada ya Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Hija Hassan Hija, kuwasilisha hoja binafsi ya kuliomba Baraza hilo kukubali kuunda kamati teule ya kulichunguza.
Hoja hiyo ilikubaliwa na Baraza hilo na kuamua kuitumia Kamati Teule, kuifanya kazi hiyo na baada ya kukamilisha kuiwasilisha katika Baraza la Wawakilishi kikao kijacho baada ya mjadala wa kujadili bajeti za mawizara ya serikali kumalizika.
Hoja iliyowasilishwa na Mwakilishi huyo ilihusu madai ya kuwapo kwa malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi wa Zanzibar wanaolalamikia kuunganishiwa huduma ya umeme wakipewa usumbufu huku wamiliki wa mahoteli, makampuni ya simu mabenki na minara wakiunganishiwa huduma hiyo mara moja.
Aidha eneo jengine alilitaja kuwa baya zaidi ni kuwepo kwa muda mrefu wanaopewa wananchi huku wakipandishiwa gharama kubwa wawekezaji wakipewa gharama ndogo.
Hoja hiyo ilidai inasikitishwa na kuona fedha wanazotoa wawekezaji hao haziingii katika mapato ya shirika hilo, na zile zinazotolewa na wamiliki wa mahoteli zikiingia mifukoni mwa baadhi ya watendaji.
Madai mengine ambayo yaliwasilishwa katika hoja hiyo, ni kudaiwa kwa shirika hilo limekuwa likitoa ajira kwa upendeleo kati ya wananchi wa Unguja na Pemba.
Aidha hoja hiyo pia imedai kuwa shirika hilo limeingia katika mikataba mingi ambayo inaonekana kutokuwa na tija ikiwemo ya ununuzi wa majenereta 32 yalionunuliwa baada ya Zanzibar kuingia katika kiza.
Suala jengine ambalo lilitajwa ndani ya hoja hiyo ni kufanyiwa uchunguzi juu ya deni la Zanzibar linalodaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuona kama kuna maslahi ya kuwapo kwa deni hilo na athari zake na taratibu za uuzwaji wa mali za shirika kama zinafuata sheria.
Hoja hiyo Mwakilishi huyo alidai aliiwasilisha kwa kutumia kanuni ya 27 (1) (m), 27 (3) 48 (1), na 49 (1) za kanuni za Baraza la Wawakilishi kuwa anaomba kutoa hoja kuwa baraza hilo liridhie kuunda Kamati Teule kwa mujibu wa kanuni 117 ya kanuni ya Baraza (toleo la @011) ili kuchunguza Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).
Kutokana na kuridhiwa huko Mwenyekiti wa kamati hiyo Omar Ali Shehe, aliliambia Zanzibar Leo jana, tayari kazi ya kulichunguza shirika hilo imefikia asilimia 80 baada ya kuwahoji watendaji mbali mbali wa Shirika hilo.
Alisema waliokwishafikishwa mbele ya Kamati hiyo ni pamoja na watendaji wanaoziongoza idara mbali mbali za Shirika hilo, wahasibu, washika fedha, Wafanyakazi wa vitengo tofauti vikiwemo vya ufundi pamoja usimamizi wa miradi.
Aidha, Mwenyekiti huyo ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake, alisema mahojiano wanayokusudia kuyafanya hivi sasa ni pamoja na Meneja Mkuu wa Shirika hilo na viongozi na Wajumbe wa Bodi ya Shirika.
Alisema hivi sasa wamelazimika kusitisha mahojiano hayo kutokana na kamati yao kuhusika na kuipitisha bajeti ya serikali na baada ya kumaliza kazi hiyo wataendelea na kazi hiyo.
Alisema asilimia kubwa ya mahojiano hayo yamekwenda vizuri kati ya watendaji walioitwa mbele ya kamati hiyo kutakiwa kutoa maelezo yao kwa vielelezo vya msingi.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisema muhtasari wa ripoti hiyo ya uchunguzi bado ni siri na itapokamilika itawasilishwa mbele ya Baraza la Wawakilishi ili waweze kuijadili.
Wajumbe wanaounda kamti ya uchunguzi huo ni Makamu Mwenyekiti wa PAC, Fatma Mbarouk Said, Mwakilishi wa Chonga, Abdalla Juma Abdalla, Farida Amour Mohammed, Viti Maalum, Mbarouk Wadi Mussa Mtando wa Mkwajuni, Mohammed Mbwana Hamad, Shadya, Mohammed Suleiman, Shamsi Vuai Nahodha, Othman Ali Haji, Abdalla Ali Suleiman na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Kitaifa Hija Hassan Hija.
No comments:
Post a Comment