Habari za Punde

Madaktari, Wauguzi Wasaidieni Wagonjwa


Na Haji Nassor, Pemba

MADAKTARI katika hospitali ya Chake chake Pemba, wametakiwa kuimarisha huduma nyakati za usiku na kuacha tabia ya kuchapa usingizi ili kuepusha vifo kwa wagonjwa.

Ofisa Mdhamini wa wizara ya Afya Pemba, Mkasha Hija Mkasha alieleza hayo kenye hafla ya kukabidhiwa vifaa mbali mbali kwa ajili ya wagonjwa ikiwa ni pamoja na magodoro yaliyotolewa na mbunge mstaafu wa Jimbo la Chonga Hemed Mohamed Hemed.

Mkasha alisema kuwa pindi madaktari wa zamu za usiku wakiendelea kuuchapa usingizi, wanaweza kusababisha vifo visivyotarajiwa kwa wagonjwa, ambao wanahitaji kupitiwa saa 24 wanapokuwa wadoni.

Alieleza kuwa kitaratibu, daktari hasa anaeingia zamu ya usiku hatakiwa kulala na badala yake awe macho saa zote, kwani lolote linaweza kutokezea kwa wagonjwa na kuhitaji msaada wa dharura.

“Madaktari hasa mnaoingia zamu usiku, acheni tabia ya kuchapa usingizi, na badala yake muwapitie mara kwa mara wagonjwa wetu, ili kuwapa huduma stahiki”, alieleza Mkasha.

Akizungumzia kuhusu msaada huo wa magoro, aliwataka madaktari kuhakikisha hawayachukui majumbani, kwani yameletwa hapo kwa ajili wagonjwa na sio wao.

Alisema ni vyema msaada huo wakautunza na kuuenzi ,ili wafaidike wagonjwa mbali mbali, wanaofika hospitalini hapo na endapo wataanza kugawanana lengo halitofikiwa.

Aliongeza kuwa wodi za watoto, wanaume na wodi ya wagonjwa kifua kikuu (TB), ndizo ambazo zitafaidika na msaada huo ili kuimarisha huduma ya malazi kwa wagonjwa hao.

Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Mbunge huyo Mstaafu wa Jimbo la Chonga Hemed Mohamed Hemed, alisema safari yake yote ya alipokuwa Mbunge, ilikuwa ni kilio katika hospitali hiyo ya Chake chake.

Alifafanua alikuwa anamuomba Mwenyeenzi Mungu, kabla ya kufika mbele ya haki, awe tayari ameshafanikiwa kupata msaada huo kwa ajili ya wagonjwa wanaolazwa.

Msaada aliokabidhi Mbunge huyo Mstaafu ni pamoja na magodoro madogo 100, Mashuka 100 na mito 200, ukiwa na thamani ya shilingi 8.5 milion ,ambapo vitagawiwa kwenye wodi tofauti .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.