Habari za Punde

Polisi wafukuwa kichanga kilichonyofolewa pua
Wachukua sampuli za DNA

Na Haji Nassor, PEMBA
JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba jana limeufukuwa mwili wa mtoto Arafa Haji Silima mwenye umri wa mwezi mmoja na siku tatu kwa ajili ya kupata vipimo vya vinasaba ‘DNA’ ili kuunganishwa na mtuhumiwa aliekutwa na damu inayodhaniwa kuwa ni marehemu huyo.

Zoezi hilo ambalo liliongozwa na Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Mkoa wa Kusini Pemba Mohamed Sheihan Mohamed, madaktari, Ofisi ya Mufti, Idara ya Mkurugenzi wa Mashitaka, pamoja na ndugu na jamaa wa marehemu, lilifanyikana majira ya saa 6:00 mchana eneo alilozikwa marehemu huyo.

Akizungumza mara baada ya madaktari wa hospitali ya Chake chake kufanikiwa kuchukua maji maji (cerium) toka kwa marehemu huyo, Mkuu huyo wa upelelezi na Makosa ya Jinai, alisema walilazimika kuufukua mwili huo ili waweze kupata maji hayo yatakayotumika kuunganishwa na uchunguzi wa vinasaba.

Alisema kuwa maji maji hayo ambayo yatasafirisha hadi hospitali ya Muhimbili kwa ajili uchunguzi, matokeo yake yatawasaidia katika kugundua iwapo mtuhumiwa wanaemshikilia (hakumtaja jina) alihusika, kwa vile awali walimkamata akiwa na damu inayodaiwa kuwa ni ya kichanga hicho kilichonyofolewa pua.

“Tumelazimika kuufukua mwili wa marehemu ili kuoanisha na ile damu ambayo tayari tunayo, na lengo ni kujua tunaemshikilia akiwa na damu ndie aliyehusika kupoteza maisha ya kichanga kwa kunyofoa pua yake’’, alieleza Mkuu huyo.

Alisema kuwa matokeo hayo wanatarajia kuyapata baada ya mwezi mmoja, ili kuendelea na kesi ambapo hadi jana mtuhumiwa huyo alikuwa yuko ndani akiendelea kuhojiwa na jeshi la Polisi.

Kwa upande wake Mwanasheria Dhamana kutoka Idara ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba, Mgeni Jailani Jecha alisema kitendo walichokifanya polisi cha kuufukua mwili wa marehemu ni sahihi kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai namba 7 ya mwaka 2004.

Alieleza kuwa sheria hiyo inawapa mamlaka Polisi, kuufukua mwili wa marehemu, kwa ajili kuunganisha ushahidi ambao tayari muhiska ameshazikwa kwa taratibu zote za imani husika.

Nae Kaimu Katibu wa Mufti Pemba, Abrahaman Abdalllah Naaman, alisema kwa mujibu wa sheria ya dini ya kiislamu, yapo mambo manne makubwa, ambayo maiti anapaswa afukuliwe kisha azikwe iwapo yatajitokeza.

Aliyataja kuwa ni pamoja na kuzikwa akiwa mjamzito na kuna shaka na kulichomo tumboni kikohai, maiti kuzikwa na mali mfano pete, kukosa kuoshwa, pamoja na kukosa kuelekezwa kibla.

‘‘Hayo ni makubwa, lakini hata yako mengine madogo madogo kwa mfano hata mamlaka husika kama vile serikali wanapaswa kumfukua maiti iwapo kuna jambo wanataka kuliweka sawa’’,alizidi kufafanua Katibu huyo.

Juzi mareheumu huyo kabla ya kuzikwa, alikumbwa na mkasa wa kunyofolewa pua na mtu asiejulikana wakati akiwa ndani mwao amelala huko Wesha wilaya ya Chake Chake Kisiwani Pemba, huku Jeshi la Polisi likiendelea kumshikilia mtu mmoja kwa mahojiani.

Taarifa zilizopatikana kutoka kijijini hapo zinaeleza kuwa tukio hilo lilichukuliwa kama la kimazingara kutokana eneo amabalo alikuwa amelazwa mtoto huyo na kunyofolewa pua hapakuwa na damu.

Hili ni tukio la mwanzo kubwa katika kipindi cha miaka 10 kuwahi kutokezea la kufukuliwa maiti na Jeshi la Polisi kwa kutaka kuchukua ushahidi wa aina hii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.