Habari za Punde

Huduma za mawasiliano zipanuliwe vijijini

Na Fatuma Kitima, DAR ES SALAAM
SERIKALI kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaangalia njia itakayotumika kuhakikisha huduma ya mawasiliano inapatikana katika maeneo mbali mbali nchini hasa katika maeneo vijijjini.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Prof. John Nkoma alieleza hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya kusherekea siku ya Mawasiliano Duniani.

Prof. Nkoma alisema kuwa mawasiliano yamekuwa kwa kiasi kikubwa ingawa bado baadhi ya maeneo hasa vijini bado kuna changamoto ya kupatikana kwa huduma hiyo kwa uhakika.

Alifahamisha kuwa asilimia 70 ya watu wanaoishi maeneo ya vijijini hawana huduma ya mawasiliano, jambo ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi ili uwepo usawa wa kupatikana kwa haki hiyo.

“Maendeleo yasiwe maeneo ya mijini tu, bali yaende hata maeneo ya vijijini”, alisema Prof.Nkoma katika hafla hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano (WMST), Clarence Ichwekeleza alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuzisajili simu zao kwani zoezi hilo lina umuhimu mkubwa.

Clarence alisema kuwa kusajili simu ni muhimu kwani inasaidia pindi unapoipoteza kupata vitu muhimu vilivyomo ndani ya simu hiyo.

Hata hivyo alisema kuwa mawasiliano yameongezeka kwa kiwango kikubwa kwa kuwa wakati huu watu wanatumia muda mfupi kupata huduma za benki kutumia simu zao za mikononi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.