Wizara yafafanua agizo kusitishwa malipo ya uzazi
Na Salum Vuai, Maelezo
WIZARA ya Afya Zanzibar, imewashauri wananchi kuendelea kuvuta subira wakati wizara hiyo ikijiandaa kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, la kutaka kusitishwa kwa ada kwa akinamama wajawazito.
Dk. Shein alitoa agizo la kusitishwa kwa michango hiyo ya shilingi 40,000 anazotozwa mama mmoja ambaye huzalishwa kwa njia ya upasuaji, wakati akifanya majumuisho ya ziara yake ya Mkoa wa Kusini Unguja, katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar kuliopo Tunguu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu waziri wa Afya Dk. Sira Ubwa Mamboya alisema wizara imefarijika na agizo hilo, kwani yamekuwepo malalamiko na lawama nyingi juu ya utaratibu huo wa kuwatoza malipo kinamama hao.
Dk. Sira alilazimika kutoa ufafanuzi huo, kutokana na kubainika kuwepo kwa baadhi wananchi kukataa kulipa fedha wanazotozwa kwa sasa, kufuatia tamko hilo la Rais.
Hata hivyo, alisema kwa sasa utaratibu huo hauwezi kutekelezeka mara moja, hadi bajeti ya wizara kwa mwaka 2012/13 itakapopitishwa katika kikao cha bajeti kinachotarajiwa kuanza mwezi ujao.
Alifahamisha kuwa, wizara yake iko katika mchakato wa maandalizi ya kuanza utaratibu huo, kwani katika bajeti inayomalizika, hakuna makisio ya kufidia gharama hizo.
"Inawezekana baadhi ya wananchi wamemfahamu vibaya Rais, ni kweli hata sisi hatupendi kuwalipisha, lakini kutokana na hali halisi, tunawaomba wavumilie hadi baadhi ya mambo yatakapowekwa sawa ikiwemo kupitishwa kwa bajeti ijayo", alifafanua Dk. Sira.
Alitaja miongoni mwa mambo muhimu kabla kuanza kwa utaratibu wa kutoa huduma bila malipo kwa wananchi, kuwa ni pamoja na wizara yake kuandaa na kutangaza zabuni ya kuleta vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya huduma hizo za uzazi salama kwa kinamama wajawazito.
Naibu Waziri huyo alisema, wizara yake imeshauriana na Rais kuhusu hali hiyo, na kuongeza kuwa pamoja na wananchi kutokutozwa ada yoyote, bado serikali itakuwa ikigharamika kwani ndiyo itakayolipia gharama hizo.
"Tumelazimika kutoa ufafanuzi huu kwa sababu wakunga na wauguzi wetu wanapata shida kwani wananchi wamefahamu kuwa ada hizo zimeshafutwa tangu Rais alipotoa kauli hiyo kule Tunguu, tunawasihi wawe na subira kwa sasa na tutakapokuwa tayari tutawatangazia rasmi", alisisitiza Dk. Sira.
Akizungumzia hali halisi katika wodi ya wazazi hospitali kuu ya Mnazimmoja, Dk. Sira alisema kwa kawaida, wodi hiyo hupokea kinamama 40 wanaokwenda kujifungua, ambapo kati ya hao, takriban wanane kati yao hulazimika kufanyiwa upasuaji.
Kinamama hao wanaojifungua kwa upasuaji hutozwa shilingi 40,000, huku wale wasiohitaji kupasuliwa, hutakiwa kununua vifaa vyao kwa gharama zao wenyewe.
No comments:
Post a Comment