Habari za Punde

Azma ya Serikali Kukuza Kilimo ipo Palepale - Maalim Seif


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wakulima wa bonde la mpunga Cheju wakati wa ziara yake katika bonde hilop jana. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim.

Mkulima wa mpunga katika bonde la Cheju Bi Siame Ali akitoa maoni yake kuhusiana na kufeli kwa kilimo hicho mwaka huu mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad (hayupo pichani) kufuatia ziara ya kiongozi huyo katika bonde hilo.

Mkulima wa mpunga katika bonde la Cheju Bw. Kheir Kombo akitoa maoni yake kuhusiana na kufeli kwa kilimo hicho mwaka huu mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad (hayupo pichani) kufuatia ziara ya kiongozi huyo katika bonde hilo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim akitoa ufafanuzi juu ya masuala mbali mbali yaliyoulizwa na wakulima wa mpunga katika bonde la Cheju mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wakulima wa bonde la mpunga Cheju wakati wa ziara yake katika bonde hilo jana. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim na wa pili kushoto ni kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Abdallah Mwinyi Khamis. (Picha, Salmin Said, OMKR). 

Na Hassan Hamad OMKR

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad azma ya Serikali ya kukuza kilimo iko pale pale na wala haitorudi nyuma, licha ya changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Amesema Serikali inawategemea sana wakulima hasa wa mpunga na kwamba mafanikio yao yanaisaidia serikali katika kukabiliana na ugumu wa maisha na kunyanyua kipato cha wananchi. 

Maalim Seif alitoa changamoto hiyo jana alipotembelea mabonde ya mpunga huko Cheju Mkoa wa Kusini Unguja kuangalia maendeleo ya kilimo hicho kwa msimu huu, ambapo kwa kiasi kikubwa kilimo cha juu cha kutegemea mvua hakikuleta mafanikio mazuri katika eneo hilo. 


Amefahamisha kuwa lengo la serikali ni kuongeza uzalishaji wa mpunga ili kupunguza uagiziaji wa zao hilo muhimu zaidi la chakula kwa Zanzibar kutoka nchi za nje. Ameseongeza kuwa katika kufikia malengo hayo serikali imepanga kununua matrekta mapya ishirini ambayo kwa kushirikiana na yale mengine ambayo yalitengenezwa msimu uliopita, yatapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa matrekta Unguja na Pemba. 

Hatua nyengine zilizochukuliwa katika kukuza kilimo cha mpunga ni pamoja na kupunguzwa kwa bei za pembejeo kwa wakulima ambapo kwa msimu uliopita mbolea kipolo kimoja kiliuzwa kwa shilingi elfu kumi kutosha shilingi elfu sitini, dawa ya magugu lita moja iliuzwa kwa shilingi elfu sita kutoka shilingi 26 elfu na mia tano, huku gharama za uchimbuaji ziliwa shilingi elfu 16 kwa ekari moja kutoka shilingi 64 elfu. 

Amewataka wakulima wa mpunga kuitumia fursa hiyo kuendeleza kilimo hicho kwa lengo la kuongeza tija na kupunguza umaskini wa kipato unaowakabili wananchi wengi wa Zanzibar. Amesema mbali na hilo, serikali pia inaendelea kufanya utafiti ili kupata mbegu bora zaidi ambazo zitaendana na mazingira na hali ya hewa ya Zanzibar. 

Katika hatua nyengine, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema Serikali inafanya tathmini ili kuweza kuwafidia wakulima wa mpunga katika bonde la Cheju ambao kilimo chao kiliathirika kutokana na sababu mbali mbali. 

Amesema licha ya serikali pamoja na wakulima kufanya juhudi kubwa katika kukiendeleza kilimo cha mpunga mwaka huu, lakini hali haikuwa nzuri kwa kilimo cha juu katika maeneo ya Cheju, hali inayoifanya serikali kufikiria namna ya kuwafidia wakulima hao, ili waweze kukabiliana na athari hizo. 

Ameutaka uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili kuharakisha tathmini hiyo, ili kuzipa nafasi mamlaka zinazohusika kuweza kuchukua hatua kwa muda muafaka. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Bw. Affan Othman Maalim akizungumzia kuhusu mafanikio duni ya kilimo hicho katika bonde la Cheju msimu huu kumetokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamepelekea mvua kutonyesha kwa wakati na kwa kiwango kisichotarajiwa. 

Ameitaja sababu nyengine kuwa ni usimamizi mbovu wa baadhi ya jumuiya zilizokuwa zikisimamia kilimo hicho ambazo baadhi yao hazikuwa waaminifu. Affan amefahamisha kuwa tayari Wizara yake imeshajiandaa kikamilifu kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo, na kwamba maandilizi ya kazi hiyo yataanza mapema zaidi, ili kutoa fursa kwa wakulima kufikiwa na huduma kwa muda unaostahiki. 

Ametoa wito kwa wakulima kuweka utaratibu wa kuorodhesha majina yao na maeneo wanayohitaji kuchimbuliwa, ili kuondosha usumbufu wakatika kazi ya uchimbuaji na uburugaji inapoanza.

Kwa upande wao wakulima wa bonde hilo wameiomba serikali kuanza maandilizi mapema kwa ajili ya msimu ujao, sambamba na kuwasogezea pembejeo za kilimo karibu ili waweze kuzitumia kwa wakati. Pia wameiomba serikali kuzifanyanyia matengenezo barabara katika mabonde hayo, ili ziweze kupitika wakati wote na kurahisisha usafirishaji wa mazao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.