UTANGULIZI
1. Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu, likae
kama Kamati kwa madhumuni ya kupokea, kujadili, kuzingatia na hatimae
kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
2. Mheshimiwa
Spika, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi
wa Rehema kwa kutujaalia uzima na afya njema na kuweza kukutana
hapa katika kikao hiki muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Aidha, nachukua fursa hii adhimu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa
kutuongoza, kutuelekeza na kusimamia ipasavyo utekelezaji wa majukumu ya
Serikali kama ilivyoainishwa katika miongozo iliomo katika Mipango Mikuu ya
Kitaifa, Kimataifa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 -2015.
3. Mheshimiwa
Spika, ni dhahiri juhudi zake anazozichukua katika kulitumikia
Taifa na kuweza kutenga muda maalum wa kukutana na watendaji ili kupitia
mipango ya utekelezaji wa bajeti ya kila Wizara bila ya kuchoka tena kwa
uadilifu, umahiri na umakini mkubwa umeleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji
ndani ya Serikali. Hakika changamoto anazotupa zimetufanya tuwe na mtizamo mpya
katika upangaji na utekelezaji wa kazi zetu. Hatua hii imeleta uwazi, ubunifu na
uwajibikaji katika kusimamia maadili ya matumizi ya fedha za umma. Namuomba Mwenyezi
Mungu ampe umri mrefu na afya njema ili aweze kuiongoza vema nchi yetu.
4. Mheshimiwa
Spika, nawapongeza Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad
Makamo wa Kwanza wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi Makamo wa Pili wa
Rais kwa kumsaidia kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar katika
utekelezaji wa kazi zake. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza
la Mapinduzi kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuitumikia nchi yetu.
5. Mheshimiwa Spika, naomba
kukupongeza wewe binafsi, Naibu wako na Wenyeviti kwa kuliongoza vizuri Baraza
letu. Umahiri wako katika kutuongoza umepelekea kukua na kuimarika kwa
demokrasia na mijadala iliyo wazi, inayosisimua na inayovutia wananchi wetu. Hali
hii imejenga imani kubwa ya wananchi kwa chombo chao cha kutunga Sheria pia
kujenga imani na viongozi waliowachagua.
6. Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya kipekee natoa pongezi maalumu kwa
Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi zinazofanya kazi na Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Kamati hizo ni Kamati ya Kusimamia Ofisi za
Viongozi Wakuu wa Kitaifa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Hamza Hassan Juma,
Mwakilishi wa kuchaguliwa na wananchi wa Jimbo la Kwamtipura ambae pia ni
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi. Vile vile
Kamati ya Kusimamia Hesabu za Serikali (PAC) inayoongozwa na Mheshimiwa Omar
Ali Shehe, Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake. Ushauri na miongozo yao mizuri
imesaidia sana katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku na
tunawaahidi kuwa tutaendelea kutoa ushirikiano wetu kwao. Naomba pia
kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la wawakilishi ambao kwa namna
moja au nyengine wamekuwa wakifanya kazi na Wizara zetu.
7. Mheshimiwa
Spika, Hotuba yangu hii inalenga kutoa maelezo ya kina ya
utekelezaji wa malengo ya bajeti ya mwaka 2011/2012. Aidha, nitaeleza pia muelekeo
wa vipaumbele vya bajeti na malengo yatakayotekelezwa na Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika mwaka ujao wa fedha 2012/2013.
8. Mheshimiwa
Spika, utekelezaji wa malengo ya bajeti kwa kipindi
cha Julai- Machi 2011/2012 kwa Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi umezingatia
vipaumbele vilivyowekwa katika malengo ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Sambamba na malengo hayo, Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar ilitekeleza miradi kumi ya maendeleo.
Miradi hiyo ni kama ifuatayo:-
i.
Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya
Ikulu na Nyumba za Serikali (State Lodges)
ii.
Kuimarisha Mawasiliano Ikulu
iii.
Mageuzi ya Serikali za Mitaa
iv.
Uendelezaji Vitambulisho
v.
Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa Kaskazini Unguja
vi.
Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa Kusini Unguja
vii.
Shamba la Mfano la Mbogamboga-Bambi
viii.
Ujenzi wa Makao Makuu ya Valantia
ix.
Ujenzi wa Hospitali mpya ya Kikosi cha
Kuzuia Magendo (KMKM)
x.
Ujenzi wa Chuo Kipya cha Mafunzo Hanyegwa
Mchana
9. Mheshimiwa Spika, Aidha,
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ilitekeleza Mradi wa Mpango wa
Kuimarisha Huduma za Miji Zanzibar (Zanzibar Urban Service Programme ZUSP).
Usimamizi wa utawala na fedha wa mradi huu upo chini ya Ofisi ya Rais, Fedha,
Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
10. Mheshimiwa
Spika, matayarisho ya bajeti ya Ofisi ya Rais
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa Mwaka wa fedha 2012/2013,
yamezingatia mipango ya kisekta iliyowekwa katika Dira 2020 (Vision 2020), malengo
ya maendeleo ya Milenia, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA
II) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala cha CCM ya 2010 – 2015 pamoja na
vipaumbele ambavyo vimewekwa ili kutatua changamoto mbali mbali. Kwa ujumla, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inalenga
kutekeleza vipaumbele katika mambo yafuatayo:-
i)
Kuendeleza umoja wa kitaifa na
mshikamano.
ii)
Kusimamia utekelezaji wa miundo ya
utumishi na uhakiki wa kazi kwa watendaji.
iii)
Kuendelea kuimarisha makaazi na nyumba
za Ikulu.
iv)
Kuendelea kuimarisha mawasiliano na
utoaji wa habari.
v)
Kuendelea na jitihada za kufanya
Mageuzi ya Serikali za Mitaa ikiwemo kufanya mapitio ya mipaka ya maeneo pamoja
na kusimamia utungaji wa Sheria kama inavyoelekezwa na matamko ya Sera ya
Serikali za Mitaa.
vi)
Kuimarisha
uwezo na utoaji wa huduma ikiwemo usafi hasa mijini.
vii)
Kuendelea
kuimarisha na kuongeza uwezo wa Idara Maalum za SMZ ikiwemo kuimarisha haki za
binadamu kwa wanafunzi waliopo Chuo cha Mafunzo na kujenga Chuo kipya Hanyegwa
Mchana.
viii) Mafunzo kwa wafanyakazi juu ya haja ya kubadilika
kiutendaji na kufahamu dhamana walizonazo hasa katika mazingira wanayofanyia
kazi.
ix)
Kuimarisha
tafiti kwa lengo la kupata taarifa zitakazowezesha kupanga mipango kulingana na
matokeo ya tafiti hizo.
x)
Kuendelea
kuimarisha mfungamano wa Kikanda ili Wazanzibari waweze kuzitumia fursa za
kiuchumi zinazotokana na Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Jumuiya
ya Afrika ya Mashariki pamoja na Jumuiya nyengine za Kikanda.
xi)
Kuwashajihisha
Wazanzibari wanaoishi nchi za nje kushiriki na kuchangia maendeleo ya kijamii
na kiuchumi ya nchi yao.
xii)
Kutoa elimu
kuhusu masuala mtambuka (cross cutting issues) yakiwemo huduma za watu wenye
ulemavu, kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI na VVU.
xiii) Kwa kusaidiana na vyombo vyengine vya Kitaifa,
kuimarisha ulinzi na usimamizi madhubuti wa mipaka yetu pamoja na kudhibiti
magendo na uharamia.
11. Mheshimiwa
Spika, sambamba na malengo na vipaumbele vya
jumla, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi itatekeleza
jumla ya miradi minane ya maendeleo iliyopo hapa chini:-
i)
Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya
Ikulu na Nyumba za Serikali (State Lodges)
ii)
Mradi wa Kuimarisha Mawasiliano -
Ikulu
iii)
Mradi wa Mageuzi ya Serikali za Mitaa
iv)
Mradi wa Kuimarisha Kiwanda cha Ushoni
Zanzibar Quality Tailoring cha Idara Maalum za SMZ
v)
Ujenzi wa
Hospitali ya KMKM
vi)
Ujenzi wa
Makao Makuu ya Kikosi cha Valantia
vii)
Mradi wa
Shamba la Mfano la Mboga Mboga JKU
viii) Ujenzi wa Chuo kipya cha Mafunzo Hanyegwa Mchana
12. Mheshimiwa
Spika, kwa muda mrefu Serikali ilikuwa katika mchakato wa
kuandaa Sera ya Serikali za Mitaa ambayo ndiyo muongozo wa utekelezaji wa
Mageuzi ya Serikali za Mitaa, napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba Sera
hiyo sasa imekamilika. Utaratibu wa maandalizi ya Sera hii, umefuata hatua
kadhaa zikiwemo, (a) Mapitio ya taarifa na Sera mbali mbali zikiwemo tafiti
zilizofanywa juu ya mageuzi ya Serikali za Mitaa Zanzibar, (b) Mapitio ya MKUZA
na DIRA ya Maendeleo ya 2020, (c) Mapitio ya Sheria mbali mbali zinazohusu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (d) Kufanya mapitio ya muundo wa Serikali
za Mitaa (e) Mahojiano na baadhi ya watendaji na (f) Mikutano ya Wadau Unguja na
Pemba kikiwemo kikao cha Makatibu Wakuu na
Kamati ya Uongozi ya Wizara na hatimae kupitishwa rasmi na Baraza la
Mapinduzi.Sera hii inakwenda sambamba na
utekelezaji wa maazimio ya kupeleka madaraka kwa wananchi. Aidha, Sera ya
Serikali za Mitaa inatoa Mamlaka na nguvu za Utawala katika Serikali za Mitaa
na inalenga kutoa msukumo maalumu wa kuishirikisha jamii katika mipango ya kujiletea
maendeleo kutoka katika ngazi ya chini kwa misingi ya ushirikishwaji.
13. Mheshimiwa
Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naliomba Baraza lako
Tukufu liniruhusu kuwasilisha utekelezaji wa malengo ya bajeti ya mwaka wa
fedha 2011/2012 pamoja na mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 kwa Idara
na Taasisi zote zilizo chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi.
MUUNDO WA OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI
WA BARAZA LA MAPINDUZI
14. Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inajumuisha Ofisi, Idara, Vitengo
na Taasisi zifuatazo:-
a)
Ofisi ya
Faragha ya Rais
b)
Ofisi ya
Baraza la Mapinduzi
c)
Idara ya
Mipango, Sera na Utafiti
d)
Idara ya
Uendeshaji na Utumishi
e)
Idara ya
Mawasiliano Ikulu
f)
Kitengo cha
Usalama wa Serikali (GSO)
g)
Ofisi ya
Afisa Mdhamini Pemba
h)
Ofisi ya
Usajili na Kadi za Utambulisho
i)
Idara ya
Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Shughuli za Wazanzibari wanaoishi Nchi
za Nje
j)
Idara ya
Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (inajumuisha Serikali za Mikoa,
Wilaya na Serikali za Mitaa)
k)
Idara ya
Uratibu wa Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (inajumuisha Idara
Maalum za SMZ).
OFISI YA FARAGHA YA RAIS
15. Mheshimiwa
Spika, Ofisi ya
Faragha ya Rais inashughulikia kuratibu shughuli za kila siku za Mheshimiwa
Rais wa Zanzibar, kusimamia ratiba za kazi, kuweka kumbukumbu za mazungumzo
yanayofanyika na kutayarisha muhtasari wa ripoti. Kadhalika, Ofisi hii inasimamia
upatikanaji wa huduma zote za Mheshimiwa Rais na kushughulikia utunzaji na
matengenezo ya nyumba zote za Ikulu.
16. Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Ofisi
ya Faragha ya Rais iliidhinishiwa TZS 520 milioni kwa kazi za kawaida na hadi
kufikia mwezi Machi 2012, Ofisi hii iliingiziwa TZS 466.3 milioni sawa na
asilimia 89.7 ya makadirio ya matumizi.
17. Mheshimiwa
Spika, Ofisi ya Faragha ya Rais imetekeleza
vyema mujukumu na malengo yake kwa kuratibu ziara za Mheshimiwa Rais ambapo alikutana
na wananchi, viongozi wa Mikoa, Wilaya na baadhi ya Taasisi za Serikali. Kwenye
ziara hizo, Mheshimiwa Rais alishuhudia hatua mbali mbali za maendeleo na
alielezwa changamoto na hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana nazo. Miongoni
mwa Taasisi alizozitembelea ni Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Shirika
la Utangazaji Zanzibar, Mamlaka ya Maji (ZAWA) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Zanzibar. Katika Taasisi zote hizo alizozitembelea aliridhishwa na juhudi
zinazochukuliwa na Taasisi hizo na wananchi katika kujiletea maendeleo na kutoa
maelekezo ya namna ya kuimarisha huduma kwa wananchi.
18. Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa ziara za Mikoa, Ofisi
ya Faragha ya Rais iliratibu ziara hizo kwa kushirikiana na uongozi wa Mikoa.
Katika kila Mkoa, Mheshimiwa Rais alipokea taarifa za utekelezaji na kupata
ufafanuzi wa baadhi ya mambo muhimu. Aidha, Mheshimiwa Rais alikagua miradi ya
maendeleo ikiwemo ya Serikali na iliyoanzishwa na wananchi wenyewe. Katika
ziara hizo aliwasisitiza viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kwamba
wanatatua wenyewe migogoro ya ardhi iliyopo na kuepukana na kuanzisha migogoro
mipya ya ardhi.
19. Mheshimiwa
Spika, mambo mengine yaliyojitokeza ni pamoja
na vitendo vya uharibifu wa mazingira na udhalilishaji wa kijinsia ambapo Mikoa
yote imeagizwa kuandaa mikakati ya kuvidhibiti vitendo hivyo haraka
iwezekanavyo. Kwa ujumla ziara hizi zimeonesha mafanikio makubwa na
kuwafurahisha wananchi, ambapo walipata fursa za kuainisha matatizo yao na
kupatiwa ufumbuzi wa papo kwa papo. Kadhalika, ziara hizi zimesaidia kuongeza
ukaribu kati ya wananchi na Serikali yao na pia kuhuisha matumaini yao katika
kujiletea maendeleo na kuendeleza hali ya amani na utulivu.
20. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka huu wa fedha 2011/2012,
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alifanya ziara
katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (Ras el Khaimah, Sharjah na Dubai). Mheshimiwa
Rais wa Zanzibar na ujumbe wake walikutana na Mtawala wa Ras el Khaimah Sheikh
Saud Saqr Al Qasimi na Mtawala wa Sharjah Sheikh Dkt. Sultan bin Mohammed Al
Qasimi. Serikali ya Ras el Khaimah na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetia
saini mkataba wa makubaliano (MOU) katika Nyanja kadhaa za kiuchumi na
maendeleo ya jamii. Kadhalika, Hospitali Kuu ya Ras el Khaimah imetiliana saini
(MOU) na Wizara Afya ya Zanzibar kwa lengo la kushirikiana katika matibabu ya
maradhi ya kisukari, figo, moyo na saratani. Sharjah nayo imekubali kimsingi
kuisaidia Zanzibar katika utafiti wa maji yaliotuwama chini ya ardhi. Kwa jumla
ziara ya Mheshimiwa Rais katika Falme za Kiarabu imefungua milango mipya ya
ushirikiano katika nyanja zote muhimu na
itasaidia kuongeza kasi ya maendeleo ya Zanzibar.
21. Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha ushirikiano wa
kimataifa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar
amekutana na Viongozi na Mabalozi mbali mbali wakiwemo mwana wa Malkia wa
Uingereza Mheshimiwa Prince Charles na mkewe Camilla Parker Bowles, Naibu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Dkt Asha Rose Migiro, Waziri
anaeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa wa Finland Mheshimiwa Heldi Hantaka na
Waziri wa Afya wa Norway Mheshimiwa Anne-Grete Strom-Erichsen.Viongozi wote hao
walimueleza Mheshimiwa Rais namna
walivyofurahishwa na maendeleo ya Zanzibar pamoja na hali ya amani na utulivu.
Viongozi wengine mashuhuri waliokutana na Mheshimiwa Rais wanaonekana katika Kiambatanisho
Namba 1.
22. Mheshimiwa
Spika, mbali na mafanikio hayo, Ofisi ya
Faragha ya Rais pia imetekeleza malengo yake mengine kama ifuatavyo:-
a)
Kufanya
matengenezo ya sehemu ya kufulia na varanda katika Ikulu Kuu ya Mnazi mmoja
pamoja na kufanya matengenezo ya kawaida Ikulu ya Chake Chake ikiwa ni pamoja
na kuweka vipoza hewa.
b)
Ofisi
imewaongezea uwezo wa kiutendaji wafanyakazi wake watano (5) kwa kuwapatia
mafunzo na kuwalipia ada na vifaa vya masomo katika nyanja za menejimenti na
huduma za chakula na vinywaji katika Chuo cha Maendeleo ya Utalii
Maruhubi.
c)
Ofisi
imeifanyia matengenezo makubwa maktaba ya Mheshimiwa Rais. Maktaba hiyo imo
katika hatua za mwisho za ujenzi.
d)
Ofisi
imenunua vifaa mbali mbali vya kazi za kila siku za ofisi ikiwa ni pamoja na
vifaa vya kuandikia, majalada, magazeti, kompyuta sita (6) pamoja na
uchapishaji wa kadi na vitabu vya hotuba mbali mbali za Mheshimiwa Rais.
e)
Ofisi
imetoa huduma zote muhimu kwa wageni wa Mheshimiwa Rais pamoja na kufanikisha
sherehe mbali mbali zinazofanyika Ikulu.
23. Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013,
Ofisi ya Faragha ya Rais imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
a)
Kuendelea
kuimarisha shughuli za kila siku za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi.
b)
Kuimarisha
mazingira ya wafanyakazi (Work environment) na kununua vitendea kazi.
c)
Kuendeleza
matunzo ya nyumba za Ikulu na vifaa vinavyostahiki.
d) Kuwajengea uwezo wa kiutendaji
wafanyakazi wa Ofisi ya Faragha ya Rais.
24. Mheshimiwa
Spika, ili Ofisi ya Faragha ya Rais iweze
kutekekeza majukumu na malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/13,
naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 1,908.3 milioni kwa matumizi ya
kazi za kawaida.
OFISI YA BARAZA LA MAPINDUZI
25.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Baraza la Mapinduzi inayoongozwa na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi imepewa uwezo wa Kikatiba na Kisheria wa
kuratibu na kusimamia shughuli zote za Baraza la Mapinduzi na Kamati zake mbali
mbali ikiwa ni pamoja na Kamati ya Kitaalamu ya Makatibu Wakuu wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (Inter-Ministerial Technical Committee).
26.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Baraza la Mapinduzi, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 iliidhinishiwa
TZS 836 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na hadi kufikia Machi 2012,
Ofisi ya Baraza la Mapinduzi iliingiziwa TZS 644 milioni sawa na asilimia 77.0
ya makadirio ya matumizi ya kawaida na kutekeleza yafuatayo:-
a) Imeandaa
vikao 25 vya Baraza la Mapinduzi na vikao 21 vya Kamati ya Makatibu Wakuu na
kujadili nyaraka mbali mbali zikiwemo Sera na Miswada ya Sheria (Viambatanisho
2 na 3) vinatoa ufafanuzi zaidi.
b) Imeratibu
na kusimamia vikao 8 vya Kamati Maalum ya Baraza la Mapinduzi, Kamati ya Fedha,
Uchumi na Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati nyenginezo zilizopewa majukumu
maalum ya kuyafanyia kazi.
c) Imeratibu
mikutano 48 ya pamoja kati ya Mheshmiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi na Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
d) Imenunua
meza na viti vipya pamoja na kufunga mtambo wa sauti katika ukumbi wa Vikao vya
Baraza la Mapinduzi.
e) Imefanya
matengenezo makubwa katika Ofisi zake ziliopo katika Jumba la wananchi,
Forodhani ikiwa ni pamoja na kutengeneza chumba madhubuti (strong room) kwa
ajili ya kuhifadhia kumbukumbu muhimu na kutengeneza Ofisi tatu za Mawaziri
wasio na Wizara Maalum.
f)
Imehifadhi kumbukumbu za zamani za
Baraza la Mapinduzi ili kuzinusuru kuharibika kwa kuzitengenezea vitabu pamoja
na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu hizo kwa njia ya elektroniki.
g) Imewapatia
wafanyakazi wake watatu mafunzo ya muda mrefu katika fani za utawala, usimamizi
wa fedha na uandishi wa sheria.
h) Imeandaa
mafunzo maalumu kwa wafanyakazi wake kuhusu mbinu na mikakati ya kupambana na
maambukizi mapya ya UKIMWI.
27.
Mheshimiwa
Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Baraza la Mapinduzi inakusudia kutekeleza
malengo yafuatayo:-
a)
Kuhakikisha kuwa Baraza la Mapinduzi
na Kamati ya Makatibu Wakuu wanatekeleza ipasavyo majukumu yao ya kikatiba na
kisheria.
b)
Kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi
kwa Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi na watumishi wa Ofisi ya Baraza la Mapinduzi.
c)
Kuwajengea uwezo watumishi ili waweze
kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
d)
Kutunza na kuhifadhi nyaraka na
kumbukumbu muhimu za Ofisi
e) Kuongeza ufanisi kazini ikiwemo
kuwapatia watendaji stahili zao
f)
Kutathmini
utendaji na uwajibikaji wa Serikali.
28.
Mheshimiwa
Spika, ili
Ofisi ya Baraza la Mapinduzi iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 1,362
milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.
IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI
29. Mheshimiwa
Spika, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ina jukumu la
kuandaa na kusimamia utayarishaji wa Sera, Sheria, Mipango na kufanya utafiti
na tathmini kwa miradi ya maendeleo. Aidha, ina jukumu la kufuatilia, kukusanya
na kuchambua takwimu zitakazosaidia kufanya tathmini na kupanga mipango ya
maendeleo. Vile vile, Idara inaratibu utekelezaji wa DIRA 2020, MKUZA II,
Mageuzi Makuu (Core Reforms), Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Chama Tawala ya mwaka
2010 - 2015 na mipango mengine mikuu ya Kitaifa na Kimataifa. Jukumu jengine ni
kuratibu kazi za kuandaa ripoti za utekelezaji wa Bajeti na Mipango ya
Maendeleo.
30.
Mheshimiwa Spika, Idara
ya Mipango Sera na Utafiti, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 iliidhinishiwa TZS 240
milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na hadi kufikia Machi 2012, Idara hii iliingiziwa
TZS 158.5 milioni sawa na asilimia 66.0 ya makadirio ya matumizi ya kawaida na
kutekeleza yafuatayo:-
a)
Imetoa elimu
ya uibuaji na uimarishaji wa miradi kwa maofisa 25 wa miradi.
b)
Imenunua samani
pamoja na kukusanya vitabu kwa ajili ya kitengo cha nyaraka (Documentation
Centre).
c)
Imeanzisha
tovuti (Website) ya Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kutayarisha Barua Pepe rasmi (Official E-mail
Address) za maafisa wote na watendaji wengine.
d)
Imeanzisha
kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) na kukipatia samani
na vitendea kazi vikiwemo kompyuta tatu, 3G computer modem, anti virus software
na vifaa vya kuhifadhia kumbukumbu.
e)
Imewajengea
uwezo watendaji wake kwa kufanya ziara za kujifunza katika Ofisi za Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zilizopo Dodoma na Dar es
Salaam. Aidha, wafanyakazi watatu wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi, kati ya
wiki mbili hadi nne katika fani za uchambuzi wa Sera, kufanya ufuatiliaji na
tathmini kwa kuangalia matokeo pamoja na uwajibikaji katika bajeti, sambamba na
kuendesha semina mbili kwa Maafisa Mipango 52 wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Unguja na Pemba ili waweze
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na namna bora ya kuandika ripoti za
utekelezaji.
f)
Imefanya mapitio ya Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
g)
Imenunua vitendea kazi vikiwemo kompyuta nne, fotokopi kubwa
moja, skana moja, na samani za Ofisi zikiwemo meza na viti.
h) Imeandaa
ripoti za utekelezaji wa malengo ya bajeti ya mwaka 2011/2012, utekelezaji wa
miradi ya maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala cha CCM ya mwaka
2010-2015.
i)
Imeratibu utekelezaji wa miradi 10 ya
maendeleo inayotekelezwa na Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa
kuitembelea na kufanya tathmini juu ya utekelezaji wake na kujua hatua iliyofikia.
j)
Kwa kushirikiana na Idara ya Utumishi
na Uendeshaji, imetoa mafunzo juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI na
VVU kwa watendaji 34.
UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO KWA
MWAKA 2011/2012
31.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi iliidhinishiwa kutekeleza miradi 9 ya maendeleo na fedha zilizotengwa
kwa miradi hiyo ni TZS 1,930.0 milioni. Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
imeratibu utekelezaji wa miradi hiyo kwa ufanisi mkubwa. Naomba kuitaja miradi
hiyo kama ifuatavyo:-
i)
Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Ikulu na Nyumba za
Serikali (State Lodges)
ii)
Kuimarisha Mawasiliano Ikulu
iii)
Mageuzi ya Serikali za Mitaa
iv)
Uendelezaji Vitambulisho
v)
Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja
vi)
Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja
vii)
Shamba la Mfano la Mboga Mboga Bambi
viii)
Ujenzi wa Makao Makuu ya Valantia
ix)
Ujenzi wa Hospitali mpya ya Kikosi cha KMKM
Mradi
wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Ikulu na Nyumba za Serikali
32.
Mheshimiwa
Spika, Mradi
wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Ikulu na Nyumba za Serikali uliidhinishiwa
TZS 300 milioni na hadi kufikia mwezi Machi 2012, mradi huu umeingiziwa TZS 300
milioni sawa na asilimia 100.0 ya makadirio ya matumizi na kutekeleza
yafuatayo:-
a) Kukamilisha
matengenezo ya Ikulu ndogo ya Migombani kwa kuweka grill za chuma sehemu 16
eneo la pwani, kutengeneza msingi
unaopokea maji ya mvua mbele ya Geti kuu, kujenga ukuta mpya sehemu ya kufulia,
kuweka paa, kutengeneza mageti matatu, kulipa gharama za matengenezo ya waya na
vioo vya madirisha, kulipa gharama za
uwekaji wa viegesho vya gari (car parking shades), kulipa gharama za
matengenezo ya Msikiti, kulipia gharama za matengenezo ya jiko la nje pamoja na
kujenga ukuta (fence) sehemu ya pembeni ya eneo la nyumba ya Migombani.
b) Kulifanyia ukarabati jengo la Ikulu Kuu (Mnazi Mmoja)
kwa kutia
rangi ukuta na kutengeneza sehemu ya vyoo.
c) Kuanza ujenzi wa nyumba ya Ikulu ndogo ya Laibon
Dar-es-salaam kwa kufanya marekebisho ya jikoni na kuweka makabati
ya aluminium, kugharamia uwekaji wa mtambo wa Intercom na kulipa gharama za
kutengeneza na kufunga viegesho vya gari (car parking shades).
Mradi
wa Kuimarisha Mawasiliano – Ikulu
33.
Mheshimiwa
Spika,
mradi wa Kuimarisha Mawasiliano - Ikulu uliidhinishiwa TZS 100 milioni na hadi
kufikia mwezi Machi 2012, fedha zilizoingizwa ni TZS 100 milioni sawa na
asilimia 100 ya makadirio ya matumizi. Fedha zote zimetumika kwa kununulia gari
la mawasiliano aina ya Toyota VX na vifaa vyake vikiwemo mabomba, inverter,
wireless microphones na amplifier.
Mradi
wa Mageuzi ya Serikali za Mitaa
34.
Mheshimiwa
Spika,
Mradi wa Mageuzi ya Serikali za Mitaa uliidhinishiwa TZS 150 milioni na hadi
kufikia mwezi Machi 2012, fedha zilizoingizwa ni TZS 86.3 milioni sawa na
asilimia 57.5 na kutekeleza yafuatayo:-
a)
Sera ya Serikali za Mitaa imekamilika. Viliandaliwa jumla ya vikao
kumi vya wadau wa sera wakiwemo Makatibu wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya,
Madiwani, Wenyeviti wa Halmashauri na Mabaraza ya Miji, Maofisa wa wizara za
SMZ na Taasisi zisizo za kiserikali (NGO’S) kwa kukusanya maoni ambayo
yalisaidia sana katika kukamilisha sera hiyo.
b)
Imeandaa hadidu rejea za kutayarisha Mpango Mkakati.
c)
Imeandaa madodoso ya kufanya utafiti unaolenga ukusanyaji wa
mapato na uwezo wa kiutendaji katika Serikali za Mitaa.
35.
Mheshimiwa
Spika, utekelezaji
wa miradi mingine sita (6) niliyoitaja awali nitaitolea maelezo yake katika
Idara husika.
36.
Mheshimiwa
Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ya Mipango Sera na Utafiti imekusudia
kutekeleza malengo yafuatayo:-
a)
Kuimarisha uwezo
wa Idara katika kupanga, kuandaa na kuchambua Sera, kufanya tafiti pamoja na
kuratibu shughuli za mipango na bajeti za Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi.
b)
Kufanya uchambuzi
wa Sera ya Serikali za Mitaa ili iweze kutekelezeka na kufanya uchambuzi wa
Mpango Mkakati wa Chuo cha Mafunzo na kuhakikisha utekelezaji wake.
c)
Kuandaa utafiti unaolenga kutanua wigo katika
ukusanyaji wa Mapato kutoka Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Idara ya
Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
d)
Kuratibu na
kuandaa ripoti za utekelezaji wa malengo ya bajeti pamoja na Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2010-2015.
e)
Kuandaa mfumo
shirikishi wa ufuatiliaji na tathmini kwa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
f)
Kuimarisha uwezo wa watendaji kitaaluma.
g) Kuimarisha na kutunza kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEKNOHAMA).
h) Kuongeza ufanisi kazini ikiwemo
kuwapatia watendaji stahili zao, kununua vitendea kazi vya kisasa vya Ofisini
na samani.
MIRADI YA MAENDELEO ITAKAYOTEKELEZWA
KWA MWAKA 2012/2013
37.
Mheshimiwa
Spika,
kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi itatekeleza
miradi ifuatayo:-
i)
Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya
Ikulu na Nyumba za Serikali (State Lodges)
ii)
Mradi wa Kuimarisha Mawasiliano -
Ikulu
iii)
Mradi wa Mageuzi ya Serikali za Mitaa
iv)
Mradi wa Kuimarisha Kiwanda cha Ushoni
cha “Zanzibar Quality Tailoring” cha Idara Maalum za SMZ
Mradi
wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Ikulu na Nyumba za Serikali (State Lodges)
38.
Mheshimiwa
Spika, Mradi
wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Ikulu na Nyumba za Serikali utatekeleza
malengo yafuatayo:-
a) Kujenga nyumba mbili za
wafanyakazi na walinzi ndani ya eneo la Ikulu ndogo ya Laibon Dar es Salaam.
b) Kuezeka nyumba ya Ikulu
ndogo ya Mkoani na kutengeneza kibanda cha walinzi.
c) Kuanza ukarabati mkubwa
wa nyumba tatu za Ikulu ya Chake Chake.
d) Kukamilisha ujenzi wa
nyumba ya Serikali ya mapumziko Micheweni.
Mradi wa
Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Ikulu na Nyumba za Serikali unakadiria
kutumia TZS 400 milioni.
Mradi
wa Mawasiliano – Ikulu
39.
Mheshimiwa
Spika, Mradi
wa Mawasiliano – Ikulu utatekeleza malengo yafuatayo:-
a)
Kufanya
matengenezo ya chumba kwa ajili ya utayarishaji wa vipindi
b)
Kununua vifaa
vya kisasa kwa ajili ya kurikodia sauti na picha
c)
Kununua
mashine za kufanyia uhariri wa vipindi
Mradi wa Mawasiliano - Ikulu unakadiria
kutumia TZS 100 milioni.
Mradi wa Mageuzi
ya Serikali za Mitaa
40.
Mheshimiwa
Spika, Mradi
wa Mageuzi ya Serikali za Mitaa utatekeleza malengo yafuatayo:-
a)
Kupitia na kuunda mipaka mipya ya Mamlaka ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa
b)
Kusambaza na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Serikali za Mitaa
c)
Kuunda vikundi kazi vitakavyotumika katika kupitia mfumo wa Kodi
na Mapato wa Serikali za Mitaa na Muundo wa Serikali za Mitaa na Utawala.
d)
Kupitia na kufanya marekebisho ya Sheria Namba 1 ya mwaka 1998, ya
Mamlaka ya Utawala wa Mikoa na Sheria Namba. 3 na 4 ya mwaka 1995 ya Serikali
za Mitaa
Mradi wa Mageuzi ya Serikali za
Mitaa unakadiria kutumia TZS 150 milioni.
Mradi
wa Kuimarisha Kiwanda cha Ushoni cha “Zanzibar Quality Tailoring” cha Idara
Maalum za SMZ
41.
Mheshimiwa
Spika, Mradi
mpya wa Kukiimarisha Kiwanda cha Ushoni “Zanzibar Quality Tailoring” cha Idara
Maalum za SMZ unakusudia kukipa uwezo kiwanda hicho kwa kununua vifaa vya
kisasa vikiwemo vyarahani na mashine za kufumia. Mradi huu utakapokamilika
unategemewa kushona aina zote za Sare za Idara Maalum za SMZ na kuondokana na
utaratibu wa kuagizia vifaa hivyo kutoka nje.
Mradi wa Kuimarisha Kiwanda cha
Ushoni cha Idara Maalum za SMZ unakadiria kutumia TZS 256 milioni.
42.
Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
iweze
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba
Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 466.9 milioni kwa matumizi ya kazi za
kawaida na TZS 906 milioni kwa matumizi ya
kazi za maendeleo.
IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI
43.
Mheshimiwa
Spika, Idara
ya Uendeshaji na Utumishi ina jukumu la kusimamia shughuli za Utawala na
Utumishi zikiwemo kusimamia Sheria na Kanuni za Utumishi kwa wafanyakazi,
kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi, kusimamia Sheria ya Ununuzi na
uondoaji wa mali chakavu za Serikali, kuwaendeleza wafanyakazi kielimu pamoja
na kusimamia maslahi yao.
44.
Mheshimiwa Spika, Idara
ya Uendeshaji na Utumishi, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 iliidhinishiwa TZS
1,858.5 milioni kwa kazi za kawaida. Fedha hizi zilitumika pia kwa kulipia
mishahara ya Ofisi ya Faragha ya Rais, Idara ya Mawasiliano – Ikulu, Idara ya
Uendeshaji na Utumishi, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti na Idara ya Uratibu
wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Hadi kufikia mwezi Machi 2012, Idara
hii iliingiziwa TZS 1,810.4 milioni sawa na asilimia 97.4 ya makadirio ya
matumizi ya kawaida na kutekeleza yafuatayo:-
a) Idara
imenunua zana na samani za Ofisi zikiwemo Kompyuta sita, Vespa moja, meza 13, viti 19, makabati mawili, mafriji
manne, Mafeni manne, Vipoza hewa (Air Candition) vitano, fotokopi mashine moja
pamoja na kufanya matengenezo ya Ofisi na matengenezo ya magari.
b) Idara
imesimamia maslahi ya wafanyakazi wakiwa kazini na baada ya kustaafu kwa
kuwalipa maslahi yao.
c) Idara
imeendesha vikao sita vya Bodi ya Zabuni na vikao vitatu vya Kamati ya Ukaguzi
wa ndani
d) Idara
imewajengea uwezo wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi
sita na mafunzo ya muda mfupi wafanyakazi watatu. Aidha Idara imetoa taaluma ya
kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI kwa wafanyakazi 38 wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi sambamba
na kutoa taaluma inayohusu maadili ya kazi na utunzaji wa siri za ofisi kwa watendaji
45 wa kada ya masjala. Idara pia imeratibu mafunzo kwa watendaji wa Idara zote
zilizo chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
e) Idara
imetoa motisha kwa wafanyakazi kwa kuwapatia malipo baada ya saa za kazi kwa wafanyakazi
28, sare kwa wafanyakazi 26 pamoja na kutoa zawadi kwa wafanyakazi bora watatu.
f)
Idara imeweka mfumo bora wa usimamizi na
utoaji wa taarifa katika uwajibikaji kazini kwa kuendesha semina ya uandaaji wa
taarifa za kiutumishi na Sheria ya Utumishi
wa Umma kwa Maofisa Utumishi 35 wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
kwa Unguja na Pemba.
g) Idara
imefanya uhakiki wa mahitaji ya mafunzo ya wafanyakazi pamoja na kuandaa mpango
wa mafunzo hayo. Kazi hiyo ipo katika hatua za mwisho kukamilika.
h) Idara
imepitia majukumu ya kazi ya wafanyakazi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na
kuyagawa majukumu hayo kwa wafanyakazi.
45.
Mheshimiwa
Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ya Uendeshaji na Utumishi imekusudia kutekeleza
malengo yafuatayo:-
a) Kuongeza ufanisi kazini ikiwemo
kuwapatia wafanyakazi stahili zao, kununua vitendea kazi vya kisasa na samani.
b) Kusimamia
sheria ya manunuzi pamoja na kuratibu vikao vya kamati ya ukaguzi wa ndani.
c) Kuwaendeleza
wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi 3 katika ngazi za
Shahada ya Uzamili, Shahada na Stashahada katika fani za Uongozi, Utawala na
Uhasibu. Muda mfupi wafanyakazi 2 katika fani za Udereva, na Katibu Mukhtasi. Aidha,
Mfanyakazi mmoja kujifunza lugha ya alama.
d) Kuanda
Mafunzo ya Maadili na Kazi za Ofisi ya Rais (Ikulu).
e) Kusimamia
upatikanaji wa Hati Miliki za Majengo yote ya Ikulu na Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
f)
Kutoa taaluma katika masuala mtambuka
ikiwemo kujikinga na maambukizo mapya ya UKIMWI na huduma za watu wenye ulemavu.
g) Kuandaa
mpango wa matumizi ya Rasilimali watu pamoja na kupitia muundo wa Utumishi na
kupandisha daraja watumishi (scheme of services).
h) Kufanya
uhakiki wa kazi na kutoa nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi
i)
Kukamilisha kufanya uhakiki wa
mahitaji ya mafunzo na kuandaa mpango wa mafunzo.
46.
Mheshimiwa Spika, ili Idara
ya Uendeshaji na Utumishi iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa mwaka
wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 1,247.3 milioni
kwa matumizi ya kazi za kawaida.
IDARA YA MAWASILIANO – IKULU
47.
Mheshimiwa
Spika, Idara
ya Mawasiliano Ikulu ina jukumu la kutoa, kuratibu na kupokea taarifa za
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuhusu
utekelezaji wa Sera na Mipango ya Serikali inayolenga kuwaletea maendeleo
wananchi. Aidha, Idara hii ina jukumu la kuthibitisha na kuhakikisha kuwa taarifa
zote za Mheshimiwa Rais zinazotolewa kwa wananchi na wadau wengine ni sahihi na
zinatolewa kwa wakati muafaka.
48.
Mheshimiwa
Spika, majukumu
mengine ni kutambua fursa ambazo zinaweza kutumika ili kuimarisha mawasiliano
baina ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Taasisi za
Serikali na wananchi pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wanaarifiwa kila hatua
za yale yote yaliyoahidiwa kwao na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi. Lengo ni kuweka taswira nzuri baina ya Mheshimiwa Rais wa
Zanzibar, wananchi na washirika wengine wa maendeleo. Aidha, Idara ya
Mawasiliano ina jukumu la kuandaa utaratibu utakaomuwezesha Mheshimiwa Rais
kukutana na kuzungumza na wahariri na waandishi wa habari juu ya mambo
yanayohusu Zanzibar na maendeleo yake na kwa mnasaba huo huzungumza na wananchi
kila baada ya miezi mitatu.
49.
Mheshimiwa
Spika, Idara
ya Mawasiliano Ikulu, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 iliidhinishiwa TZS 80.7
milioni kwa kazi za kawaida na hadi kufikia mwezi Machi 2012, Idara hii
iliingiziwa TZS 53.7 milioni sawa na asilimia 66.5 ya makadirio ya matumizi ya
kawaida na kutekeleza yafuatayo:-
a) Imeandaa
vipindi 25 vya televisheni kuhusu utekelezaji wa
ahadi za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kama
zilivyoelezwa kwenye Ilani ya Chama Tawala cha CCM pamoja na ahadi alizotoa
wakati wa ziara za Mikoani.
b) Imetoa
mafunzo kwa maafisa mawasiliano wa Wizara na Taasisi za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar. Mafunzo hayo yaliyotolewa ni juu ya wajibu wa maafisa mawasiliano
katika kutoa taarifa za Serikali kwa wananchi.
c) Imewapatia
mafunzo wafanyakazi watatu ambapo mfanyakazi mmoja anasomea fani ya ukatibu muhtasi,
mmoja kujifunza programu maalum ya uhifadhi wa taarifa kwenye Kompyuta na
mfanyakazi mwengine anasomea taaluma ya kazi kwa Vijana katika Chuo cha Mwalimu
Nyerere Tawi la Zanzibar.
d) Imechapisha
matoleo matatu ya majarida ya Ikulu na toleo moja la kipeperushi lenye ujumbe wa
mambo kumi ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa na watendaji pamoja na wananchi.
e) Imetembelea
na kukutana na wakuu na waandishi wa vyombo mbali mbali vya ndani na nje ya
Zanzibar kwa lengo la kuimarisha mawasiliano.
f)
Imenunua vitendea kazi vikiwemo vifaa
vya kuandikia, seti ya kompyuta na vifaa vya kutengenezea gari.
50.
Mheshimiwa
Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ya Mawasiliano Ikulu imekusudia kutekeleza
malengo yafuatayo:-
a) Kulinda
na kuendeleza taswira ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa kutoa habari sahihi na kwa wakati.
b) Kuratibu
mikutano ya Mheshimiwa Rais na Vyombo vya Habari.
c) Kuwajengea
uwezo wafanyakazi watatu kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi.
d) Kuwaendeleza
wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi wawili katika ngazi
za Shahada na Cheti katika fani za Teknolojia ya Habari na Programu ya Kazi kwa
Vijana. Muda mfupi mfanyakazi mmoja katika program maalum ya kuchambua habari
za Magazeti.
e) Kuongeza
ufanisi kazini ikiwemo kuwapatia watendaji stahili zao, kununua vitendea kazi
vya kisasa na samani.
51.
Mheshimiwa
Spika,
ili Idara ya Mawasiliano Ikulu iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 174.9
milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.
KITENGO CHA USALAMA WA SERIKALI (GSO)
ZANZIBAR
52.
Mheshimiwa
Spika, Kitengo
cha Usalama wa Serikali (GSO) Zanzibar kimeanzishwa kwa Sheria Namba 3/1983 na
kinatekeleza majukumu yake sambamba na Sheria ya Utumishi wa Umma “Public
Service Act No. 2/2011”. Sheria hizi zimeainisha majukumu ya Kitengo cha
Usalama wa Serikali kuwa ni udhibiti wa shughuli za Usalama wa Serikali na
Utumishi wa Umma.
53.
Mheshimiwa
Spika, Kitengo
cha Usalama wa Serikali (GSO) Zanzibar, kwa mwaka wa fedha 2011/2012
kiliidhinishiwa TZS 49.8 milioni kwa kazi za kawaida na hadi kufikia mwezi Machi
2012, kitengo hiki kiliingiziwa TZS 27.5 milioni sawa na asilimia 55.2 ya
makadirio ya matumizi ya kazi za kawaida na kutekeleza yafuatayo:-
a)
Kimefanya
upekuzi kwa watumishi 554 kutoka katika Taasisi mbali mbali za Serikali na
kutoa ushauri unaofaa baada ya upekuzi huo.
b)
Kimekagua
jumla ya Taasisi 12 za Serikali katika kuangalia utunzaji wa siri za Serikali
(idadi ya Taasisi zilizokaguliwa zinaonekana katika Kiambatanisho Namba 5).
c)
Kimeweza
kufanya ukaguzi wa Taasisi 12 zenye vituo muhimu katika kuangalia usalama wa
vituo hivyo na kupendekeza njia bora za kudumisha usalama.
d)
Kitengo
kilitoa mafunzo ya Usalama na kuwaelimisha watumishi wa Taasisi nane ambazo
zipo katika Kiambatanisho Namba 6.
54.
Mheshimiwa
Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Kitengo cha Usalama wa Serikali (GSO) kimekusudia
kutekeleza malengo yafuatayo:-
a)
Kufanya upekuzi wa awali na upekuzi endelevu kwa watumishi 500 wa
Serikali.
b)
Kuendeleza ushirikiano na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na
Utawala Bora katika kusimamia kanuni za utumishi na kuhakikisha zinatekelezwa
hususan zile zinazogusa usalama wa mali na nyaraka za serikali.
c)
Kuendelea kushirikiana na Maafisa Usalama wa Taasisi za Serikali
katika kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa sheria zinazohusu utunzaji wa
siri za Serikali.
d)
Kuweka mazingira bora ya kazi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa
wananchi.
55.
Mheshimiwa
Spika, ili
Kitengo cha Usalama wa Serikali (GSO) kiweze kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe
TZS 54.9 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.
OFISI
YA AFISA MDHAMINI – PEMBA
56.
Mheshimiwa
Spika, Ofisi
ya Afisa Mdhamini Pemba ina jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli za utawala
na huduma za Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi zinazofanyika
Pemba. Aidha, Ofisi hii inaratibu ziara za Viongozi Wakuu wa Kitaifa na
Kimataifa wanaotembelea Pemba. Majukumu mengine ni pamoja na kuratibu usimamizi
wa nyumba za Ikulu. Vile vile, Ofisi ya Afisa Mdhamini inaratibu shughuli za
Idara Maalum za SMZ pamoja na Mamlaka za Serikali za Mikoa na Serikali za Mitaa
kwa upande wa Pemba.
57.
Mheshimiwa
Spika, Ofisi
ya Afisa Mdhamini Pemba, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 iliidhinishiwa TZS 365.5
milioni kwa kazi za kawaida na hadi kufikia mwezi Machi 2012, Ofisi hii
iliingiziwa TZS 322.5 milioni sawa na asilimia 88.2 ya makadirio ya matumizi ya
kawaida na kutekeleza yafuatayo:-
a) Imeratibu
ziara sita za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
na ziara moja ya Mheshimiwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kisiwani Pemba.
b) Imewapatia
nafasi za mafunzo wafanyakazi sita, wanne katika ngazi ya stashahada, wawili
katika ngazi ya cheti na mfanyakazi mmoja amepatiwa mafunzo ya muda mfupi
Tanzania Bara.
c) Imetoa mafunzo kwa wafanyakazi 50 juu ya umuhimu
wakupima VVU ili kujua afya zao, kubadili tabia na kuacha unyanyapaa kwa
wafanyakazi wanaoishi na VVU na UKIMWI.
d) Wafanyakazi
16 wamepatiwa mafunzo ya siku mbili (2) juu ya umuhimu wa Daftari la kudumu la
mali za Serikali (Fixed Asset Register).
e) Imefanya
ukarabati wa jengo la Ofisi ya Afisa ya Mdhamini na imenunua vitendea kazi
vikiwemo vespa moja, kompyuta mbili na samani.
58.
Mheshimiwa
Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Afisa Mdhamini Pemba imekusudia kutekeleza
malengo yafuatayo:-
a)
Kuratibu, kusimamia na kufuatilia
utekelezaji wa shughuli zote za Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa upande wa Pemba ikiwemo ziara za Viongozi Wakuu.
b)
Kuwajengea uwezo wa kitaaluma
wafanyakazi saba kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika kiwango na
fani tofauti.
c)
Kufanya matengenezo madogo ya jengo la
Ofisi ya Afisa Mdhamini Pemba.
d)
Kuratibu mafunzo ya kujenga uwezo wa Taasisi
za Mabaraza ya Miji na Halmashauri katika kuzidi kuinua kiwango cha ukusanyaji
mapato na uibuaji wa miradi ya jamii.
e)
Kuendelea kuwajengea uelewa
wafanyakazi juu hatua za mapambano ya UKIMWI, utunzaji mazingira na uimarishaji
wa utawala bora sehemu za kazi.
f)
Kuongeza ufanisi kazini ikiwemo
kuwapatia wafanyakazi stahili zao, kununua vitendea kazi vya kisasa na samani.
59.
Mheshimiwa
Spika, ili
Ofisi ya Afisa Mdhamini Pemba iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 462.4
milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida zikijumuisha TZS 115.7 kwa ajili ya ruzuku
za Halmashauri za Pemba.
OFISI YA USAJILI NA KADI ZA
UTAMBULISHO
60.
Mheshimiwa
Spika, Ofisi
ya Usajili na Kadi za Utambulisho imeanzishwa rasmi mwaka 2005 chini ya Sheria
Namba 7/2005 ikiwa na wajibu wa kuwasajili na kuwapatia vitambulisho
Wazanzibari wakaazi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Aidha, Ofisi ina wajibu
wa kutunza taarifa zote za wananchi zilizokusanywa kwa ajili hiyo.
61.
Mheshimiwa
Spika, Ofisi
ya Usajili na Kadi za Utambulisho, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 iliidhinishiwa
TZS 1,248 milioni kwa kazi za kawaida na TZS 150 milioni kwa kazi za maendeleo
na hadi kufikia mwezi Machi 2012, Ofisi hii iliingiziwa TZS 886.9 milioni sawa
na asilimia 71.1 ya makadirio ya matumizi ya kazi za kawaida na TZS 150 milioni
sawa na asilimia 100 kwa kazi za maendeleo na kutekeleza yafuatayo:-
a) Imesajili
Wazanzibari wakaazi 10,578 waliotimiza masharti ya usajili na kutengeneza upya
vitambulisho 3,932 ambavyo vimemaliza muda wake wa matumizi na kuvigawa kwa
wahusika.
b) Imetengeneza
vitambulisho 10,393 vya wafanyakazi wa Serikali na Taasisi zake ambazo
zimewasilisha taarifa za wafanyakazi kwa kutengenezewa vitambulisho.
c) Imeandaa
Rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Usajili Namba 7 ya 2005 ili kuruhusu utoaji
wa vitambulisho vya wageni wanaoishi nchini, rasimu hiyo tayari imeshapita
Baraza la Mapinduzi na inasubiri kuwasilishwa kwenye Baraza lako Tukufu. Taratibu
zote za kiutendaji zimekamilika ikiwa ni pamoja na mfumo wa utengenezaji wa
vitambulisho hivyo, pamoja na fomu za maombi ya usajili.
d) Ofisi
imerusha hewani jumla ya vipindi 18 kupitia Shirika la Utangazaji la ZBC, juu
ya kuelimisha matumizi bora ya kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi.
e) Imeendelea
kuwajengea uwezo wafanyakazi 9 kwa kuwasomesha katika viwango vya Cheti na
Stashahada pamoja na Shahada ndani na nje ya nchi.
f)
Imenunua Kompyuta 7 mpya kwa
kubadilisha za zamani zilizokwisha muda wake.
62.
Mheshimiwa
Spika, shughuli
nyengine zilizofanywa na Ofisi ya Usajili na Kadi za
Utambulisho ni kufanyiwa ukaguzi wa kimataifa kwa mara ya sita juu ya muundo,
mfumo na taratibu zake za kiutendaji na imethibitishwa kuwa inaendelea kufanya
kazi zake kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vilivyowekwa na International Standard Organisation na IQ Net. Aidha, imekarabati vyumba viwili
katika jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Kati ili Ofisi yake ya Tunguu iweze
kuhamia Dunga kuondosha usumbufu wa kufuata huduma Tunguu katika jengo la Mkuu
wa Mkoa wa Kusini Unguja.
63.
Mheshimiwa
Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho imekusudia
kutekeleza malengo yafuatayo:-
a) Kuendelea
kuwasajili Wazanzibari Wakaazi 10,500 wanaotimiza masharti ya usajili na
kuwapatia Vitambulisho.
b) Kuendelea
kutengeneza vitambulisho vipya kwa ajili ya kubadilisha vitambulisho
vilivyomaliza muda wake wa matumizi. Pia kuwabadilishia vitambulisho vipya vya Wazanzibari
Wakaazi walioomba kufanya mabadiliko halali ya taarifa zao binafsi na
waliopoteza.
c) Kuendelea
kubadilisha na kutengeneza vitambulisho vya wafanyakazi wa Wizara, Idara na Taasisi
za Serikali kwa kuzingatia muundo mpya wa Mawizara ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
d) Kuanza
kutoa vitambulisho maalum kwa wageni wanaoishi nchini kwa ruhusa maalum
(Residence Permit) na kutunza taarifa zilizokusanywa kwa ajili hiyo katika
database ya Serikali mara baada ya marekebisho ya Sheria ya usajili Namba
7/2005 kupitishwa na Baraza la Wawakilishi.
e) Kuendelea
kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi bora na sahihi ya vitambulisho vya
Mzanzibari Mkaazi kama ambavyo sera inavyoelekeza.
f)
Kuendelea kuwajengea uwezo kielimu wafanyakazi
wa Ofisi.
g)
Kuendelea kununua malighafi za
utengenezaji wa vitambulisho sambamba na kubadilisha mitambo iliyochakaa na
kwisha muda wake zikiwemo seti za kupigia picha (Kits).
h) Kuongeza ufanisi kazini ikiwemo
kuwapatia wafanyakazi stahili zao
64.
Mheshimiwa
Spika, ili
Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho iweze kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe
TZS 1,593 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.
No comments:
Post a Comment