Habari za Punde

Hotuba ya Bajeti ya Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baaza la Mapinduzi - 3


BARAZA LA MJI WETE


1.                Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Baraza la Mji la Wete lililenga kukusanya TZS 45.6 millioni kupitia vyanzo vyake na hadi kufikia mwezi Machi 2012, Baraza limekusanya TZS 48.4 millioni sawa na asilimia 106 ya makadirio ya mapato na kutekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Baraza limetengeneza Ukumbi wa Mikutano wa Jamhuri Hall kwa kutia plasta, rangi, umeme, mafeni na vigae vya sakafuni.
b)       Limeendelea kuimarisha miradi ya jamii kwa kusaidia vifaa vya ujenzi na maji katika wadi 7, Kipangani, Selemu, Jadida, Utaani, limbani, Kizimbani na Bopwe venye thamani ya TZS. 15 milioni. 

2.                   Mheshimiwa Spika, shughuli nyengine iliyotekelezwa na Baraza ni kushughulikia kazi za matengenezo ya Soko la samaki Bandarini kwa kuunga maji, kutia rangi na umeme.

3.                   Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Baraza la Mji la Wete inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Kukusanya jumla ya TZS 50 milioni kutoka katika vyanzo vyake vya mapato
b)       Kuengeza ujazo wa kifusi katika kituo cha kuegesha gari Wete
c)       Kuendelea na ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano (Jamuhuri Hall)
d)       Ukarabati wa barabara kutoka chinjioni mpaka Bandarini.
e)       Kuendeleza huduma za usafi katika eneo la Baraza la Mji wa Wete.

HALMASHAURI YA WILAYA YA WETE


4.                   Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Wete kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 ililenga kukusanya TZS 40 milioni kutokana na vyanzo vyake vya mapato na hadi kufikia mwezi Machi 2012, Halmashauri ya Wilaya ya Wete imekusanya TZS. 59.2 milioni sawa na asilimia 148 ya  makadirio na kutekeleza yafuatayo:-

a)       Imekamilisha ujenzi wa Msingi wa Ofisi ya Halmashauri, jumla ya TZS 15.8 milioni zimetumika.
a)       Halmashauri imetoa msaada wa vifaa vya ujenzi katika Skuli za Maziwani, Mchangamdogo, Kojani, Daya, Ukunjwi, Mjini Kiuyu, Ole msingi, Pandani msingi, Bwagamoyo na Fundo. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Wete imejenga vyoo vya bei nafuu Mchangamdogo na imetoa elimu ya Afya na kununua vifaa vya usafi Kojani vyenye thamani ya TZS 5 milioni.

5.                Mheshimiwa Spika, shughuli nyengine iliyotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Wete ni kusaidia wananchi waliopata maafa kwa kuunguliwa moto nyumba zao katika maeneo ya Ole na Mzambarau Takao ambapo TZS 330,000 zimetumika.

6.                Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Halmashauri ya Wilaya ya Wete inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Kukusanya jumla ya TZS 75 milioni kutoka katika vyanzo vyake vya mapato
b)       Ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri wa Wilaya ya Wete iliyoko Bahanasa.
c)       Kusaidia huduma za Afya na Mazingira kwa kutoa mafunzo katika Wilaya ndogo, Kojani.
d)       Kusaidia vifaa vya ujenzi wa madarasa ya Skuli katika Wadi.
e)       Kununua pikipiki itakayoimarisha shughuli za ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato.

HALMASHAURI YA WILAYA YA MICHEWENI


7.                Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni katika mwaka wa fedha 2011/2012 ililenga kukusanya TZS 30 milioni kupitia vyanzo vyake vya mapato na hadi kufikia mwezi Machi 2012, imekusanya TZS 60 milioni sawa na asilimia 200 ya makadirio ya mwaka na kutekeleza yafuatayo:-

a)       Imeezeka na kupiga plasta Chinjio la Mziwanda, imejenga choo Konde Mjini, imesaidia matofali Skuli ya Sekondari Micheweni na imeanza msingi wa Skuli ya Msingi Mawe Matatu Makangale.
b)       Imenunua vitendea kazi zikiwemo Vespa mbili.

8.                Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

a)      Kukusanya TZS 77 milioni kutoka katika vyanzo vyake vya mapato.
b)      Kujenga ukumbi wa mikutano Micheweni kuanzia msingi hadi sehemu ya linta.
c)      Kusaidia miradi ya jamii, wanafunzi na majanga.
d)      Kusaidia ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa kituo cha Afya cha Simai katika eneo la Machengwe.
e)      Kusaidia kazi za kusambaza mabomba ya maji kijiji cha Kikunguni na Kibubunzi.
f)        Kuongeza ufanisi kazini ikiwemo kuwapatia wafanyakazi stahili zao, kununua vitendea kazi vya kisasa na samani.

IDARA YA URATIBU IDARA MAALUM ZA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR


9.                Mheshimiwa Spika, Idara hii ina wajibu wa kusimamia na kuratibu kazi zote za Idara Maalum za SMZ ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sera, Sheria na kanuni za Idara Maalum za SMZ, kusimamia vikao vya Tume ya Utumishi pamoja na Mahkama ya Rufaa za Idara Maalum ya SMZ. Aidha, inasimamia majukumu ya Kisera ya kuoanisha miundo ya kiutumishi, maslahi ya maafisa na wapiganaji, kuwajengea uwezo wa kitaaluma na kuratibu masuala ya michezo na utamaduni ndani ya Idara Maalum za SMZ.

10.            Mheshimiwa Spika, Idara ya Uratibu Idara Maalum za SMZ, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 iliidhinishiwa TZS 145 milioni kwa kazi za kawaida na hadi kufikia mwezi Machi 2012, Idara hii iliingiziwa TZS 84.1 milioni sawa na asilimia 58 ya makadirio ya matumizi ya kawaida na kutekeleza yafuatayo:-

a)       Imefuatilia kwa karibu shughuli zote za maendeleo na za kawaida zilizotekelezwa na Idara Maalum za SMZ.
b)       Imefanikisha vikao vitatu vya Tume ya Utumishi ya Idara Maalum za SMZ.
c)       Imefanikisha Vikao vitatu vya Mahkama ya Rufaa ya Idara Maalum ya SMZ.
d)       Idara imewajengea uwezo wafanyakazi wake wawili kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi
e)       Imenunua vitendea kazi vipya ili kuboresha ufanisi kazini.

11.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/1013, Idara ya Uratibu wa Idara Maalum za SMZ imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Kuendelea kusimamia na kuratibu kazi za kawaida na miradi mitano ya maendeleo itakayotekelezwa Idara Maalum za SMZ.
b)       Kufanikisha vikao vitano vya Tume ya Utumishi ya Idara Maalum za SMZ.
c)       Kufanikisha vikao vitano vya Mahkama ya Rufaa ya Idara Maalum za SMZ.
d)       Kufanya mapitio ya Sera, Sheria na kanuni za Idara Maalum za SMZ.
e)       Kuandaa mipango ya Rasilimali watu na kupitia miundo ya utumishi pamoja na kupandisha vyeo kwa Wapiganaji.
f)        Kuwajengea uwezo wa kitaaluma wafanyakazi wa Idara katika ngazi ya Shahada ya Pili, Cheti na mafunzo ya muda mfupi.
g)       Kukijengea uwezo wa uzalishaji Kiwanda cha Ushoni cha Idara Maalum za SMZ
h)       Kuhamasisha shughuli za michezo na utamaduni ndani ya Idara Maalum za SMZ

12.            Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Uratibu wa Idara Maalum za SMZ iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 200 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.

 

KIKOSI MAALUM CHA KUZUIA MAGENDO (KMKM)


13.            Mheshimiwa Spika, Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) kimeanzishwa kwa Sheria Namba 1/2003 na kina jukumu la ulinzi na kupambana na shughuli za magendo na uvuvi haramu katika bahari ya Zanzibar.

14.            Mheshimiwa Spika, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kiliidhinishiwa TZS 6,887 milioni kwa kazi za kawaida na hadi kufikia mwezi Machi 2012, Kikosi kiliingiziwa TZS 6,082.9 milioni sawa na asilimia 88.3 ya makadirio ya matumizi ya kawaida na TZS 200 milioni sawa na asilimia 100 kwa matumizi ya kazi za maendeleo na kutekeleza yafuatayo:-

a)       Kikosi kimewapatia sare na vifaa Maafisa na Askari wote.
b)       Vyombo vikubwa na vidogo vya doria baharini vimekuwa katika hali ya utayari na vinaendelea kupata matengenezo yanayohitajika kila mara.
c)       Kikosi kimefanya matengenezo ya banda la askari Msuka na Ofisi mpya ya uzamiaji (Diving) Makao Makuu Unguja. Aidha, ujenzi wa Hospitali ya Kibweni unaendelea katika ghorofa ya kwanza pamoja na ujenzi wa Laundry. Hanga la kulala askari la kambi mpya ya KMKM Tumbatu limeezekwa.
d)       Chombo KM 204 Miwi na KM 103 vimeshashuka chelezoni baada ya kumaliza matengenezo yaliyokusudiwa.
e)       Vifaa vya uzamiaji vimenunuliwa vikiwemo suti na mitungi ya gesi. Boti aina ya fibre na mashine yake imenunuliwa kwa ajili ya usafiri wa wazamiaji.
f)        Ulinzi wa doria umeimarika zaidi baada ya kupata boti mpya tano za fibre, vile vile vifaa vya mawasiliano (Radio Base Station) vimenunuliwa.
g)        Kikosi kimeweza kudhibiti utoroshaji wa zao la karafuu na jumla ya matukio 14 yalidhibitiwa. Pia Kikosi kimefanikiwa kukamata vitu vifuatavyo:- Mafuta  ya Diesel 25,950  Litres, Mafuta ya Petrol 1,790 liters, Sukari 20,250 kgs, kgs 76,800 za mchele na karafuu mbichi 200 kgs.
h)       Kikosi kimewapatia mafunzo Maafisa na Askari 42 katika fani ya uhasibu, sheria, utawala, afya, manunuzi, taaluma ya bahari na ufundi.
i)         Vifaa vya upasuaji kwa Hospitali ya KMKM Kibweni vimenunuliwa.

15.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) kimejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Kuendeleza kuimarisha nguvu za doria baharini.
b)       Kuimarisha sehemu ya uzamiaji (Diving)kwa kununua mashine ya kuhifadhi maisha ya binaadamu chini ya bahari (chamber), vifaa vya uzamuaji (lifting bag), nguo za kuogelea na mashine ya kujazia hewa (compressor).
c)       Kuhakikisha wafanyakazi wote wanawajibika ipasavyo kwa kuwapatia stahili zao
d)       Kuendelea kuwapatia sare na vifaa vya kulalia Wapiganaji
e)       Kuendelea kuwapatia elimu ya kazi wapiganaji nje na ndani ya Kikosi.
f)        Kuendeleza matengenezo na ujenzi wa majengo KMKM katika kambi mbali mbali.
g)       Kuendeleza ujenzi wa Hospital ya KMKM Kibweni.

16.            Mheshimiwa Spika, ili Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 9,660  milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS 200 kwa matumizi ya kazi za maendeleo.

JESHI LA KUJENGA UCHUMI (JKU)


17.            Mheshimiwa Spika, Jeshi la Kujenga Uchumi limeanzishwa kwa Sheria Namba 6 ya mwaka 2003 na lina jukumu la kuwafunza vijana katika nyanja za uchumi, kilimo, viwanda vidogo vidogo, uvuvi na mafunzo ya amali pamoja na kutoa huduma ya ulinzi kwa Taasisi za Serikali. Vijana wa JKU hufunzwa kwa kufuata mfumo wa ujenzi wa Taifa ili waweze kujiajiri wenyewe wakati wanapomaliza mafunzo yao.

18.            Mheshimiwa Spika, Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), kwa mwaka wa fedha 2011/2012 liliidhinishiwa TZS 4,668 milioni kwa matumizi ya kawaida na TZS 450 milioni kwa kazi za maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi 2012, Jeshi la Kujenga Uchumi liliingiziwa TZS 4,431.7 milioni sawa na asilimia 94.9 ya matumizi ya kawaida na TZS 195.6 milioni sawa na asilimia 43.5 ya makadirio ya matumizi ya kazi za maendeleo na kutekeleza yafuatayo:-

a)       Jeshi la Kujenga Uchumi limekamilisha uchoraji wa ramani ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari pamoja na kukusanya vifaa mbali mbali vya ujenzi wa msingi wa jengo la ghorofa moja.
b)       Wafanyakazi 25 wamepatiwa mafunzo katika fani ya sheria, udaktari, uuguzi, ualimu, uhasibu, ufugaji nyuki, ushoni na kompyuta.
c)       Mazao ya aina mbali mbali yamelimwa ikijumuisha ekari 156 za mpunga, ekari 82 za mahindi na mtama, ekari 80 za muhogo,  ekari 13 za kunde, ekari nne za viazi  vitamu ekari 21 za bustani ya miti ya matunda.
d)       Jeshi la Kujenga Uchumi limenunua mashine moja ya kutotoa vifaranga “incubator” ili kurahisisha upatikanaji wa vifaranga na kazi ya kuzalisha vifaranga tayari imeanza na inaonesha maendeleo mazuri.
e)       Jeshi la Kujenga Uchumi limechimba kisima kimoja cha maji na cha pili kipo katika hatua za mwisho ili kurahisisha upatikanaji wa maji safi na salama katika Skuli ya Ufundi na Sekondari ya JKU Mtoni.
f)        Baadhi ya zana za kufundishia zimenunuliwa kwa ajili ya kuimarisha mafunzo kwa vitendo katika Skuli ya Ufundi JKU Mtoni.
g)       Ujenzi wa nyumba ya pili ya wataalamu Bambi umekamilika na kuanza ujenzi wa msingi nyumba ya tatu. Kuchimba kisima kimoja kwa ajili ya kuongeza uwezo wa maji ya umwagiliaji kwenye   ekari 28 za mboga mboga na ekari 5 za alizeti ambazo zimelimwa.
h)       JKU imefanya mapitio ya uendeshaji wa shamba la mboga mboga Bambi ili kuweza kuleta tija kama ilivyokusudiwa.
i)         Kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Maliasili, JKU imelima ekari 15 za mbegu ya mahindi, ekari 40 za mbegu ya mpunga aina ya Nerica, ekari 10 za mbegu ya mtama.
j)         Kwa kushirikana na Vikosi vyengine JKU imeshiriki katika operasheni karafuu kisiwani Pemba katika msimu huu wa karafuu uliomalizika.
k)       JKU kwa kushirikana na JKT, imeshiriki katika maonesho ya Saba Saba na Nane Nane katika Mikoa ya Dar es salam, Morogoro na Dodoma.  Pia Jeshi la Kujenga Uchumi kwa njia ya uwakala limeleta matrekta 14 kutoka SUMA JKT kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa matrekta nchini.
l)         Vituo vya afya vya JKU Saateni na Wawi vimetoa huduma kwa Askari na Maafisa wa JKU pamoja na raia wa maeneo jirani. Kwa mwaka 2011/2012, jumla ya wagonjwa 27,653 wamepatiwa huduma tofauti za matibabu.
m)     JKU imeshiriki katika michezo ikiwemo mpira miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu, mpira wa mikono, riadha pamoja na kutoa burudani kupitia vikundi vyake vya sanaa na utamaduni. 
n)       Jeshi la Kujenga Uchumi limeweza kufanya ukarabati mkubwa wa majengo mbali mbali ikiwemo jengo la Ofisi ya JKU Upenja, nyumba moja ya kuishi wafanyakazi na ukarabati mabanda ya kuku katika kambi ya JKU Upenja.
o)       Kuendeleza ujenzi wa nyumba ya Kamanda wa JKU Pemba.

19.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/1013, Jeshi la Kujenga Uchumi limejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Kuwaendeleza kielimu watumishi wa JKU katika fani na ngazi mbali mbali ili kuleta ufanisi katika kazi.
b)       Kuendelea kutoa mafunzo ya uzalendo kwa vijana wa Zanzibar ili waweze kuitumikia nchi yao.
c)       Kuimarisha ufugaji wa kuku na ng`ombe wa maziwa pamoja na kufufua ufugaji wa nyuki.
d)       Kuimarisha kilimo cha mazao ya nafaka na miti ya matunda
e)       Kuimarisha Skuli za Ufundi na Sekondari za JKU kwa kuzipatia vifaa vya kufundishia mafunzo kwa vitendo ili ziweze kutoa elimu bora kwa vijana.
f)        Kuendelea kutoa elimu juu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi kwa wana JKU.
g)       Kuimarisha na kupanua mafunzo ya kijeshi kwa watumishi wa JKU
h)       Kuendeleza Michezo mbali mbali na utamaduni
i)         Kuendelea kutengeneza mazingira bora kwa kuwapatia wafanyakazi zana na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi pamoja na kutoa maslahi kwa wapiganaji.
j)         Kuendeleza uimarishaji wa miundombinu ya mradi wa shamba la mboga mboga liliyoko JKU Bambi.
k)       Kujenga ghala la kisasa la kuhifadhia mazao na ujenzi wa nyumba ya tatu ya wataalamu Bambi.
l)         Kununua samani na vifaa vya nyumbani, pamoja na kusimamia utendaji wa shughuli za kila siku za shamba.

20.            Mheshimiwa Spika, ili Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) liweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 7,504  milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS 300 milioni kwa ajili ya kazi za maendeleo.

IDARA YA CHUO CHA MAFUNZO (MF)


21.            Mheshimiwa Spika, Idara ya Chuo cha Mafunzo imeanzishwa kwa Sheria Namba 1 ya mwaka 1980 na ina jukumu la kuwapokea, kuwalinda wanafunzi na mahabusu kwa lengo la kuwarekebisha tabia na kuwapatia taaluma ili wawe raia wema. Pia Idara inashirikiana na Idara Maalum za SMZ na vikosi vya ulinzi na usalama vya SMT katika kuimarisha ulinzi, usalama, utulivu na amani.

22.            Mheshimiwa Spika, Idara ya Chuo cha Mafunzo (MF), kwa mwaka wa fedha 2011/2012 iliidhinishiwa TZS 3,938 milioni kwa kazi za kawaida na TZS 400 milioni kwa matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi 2012, Kikosi kiliingiziwa TZS 3,307.6 milioni sawa na asilimia 84.0 ya makadirio ya matumizi ya kawaida na TZS 315.6 milioni sawa na asilimia 78.9 kwa matumizi ya kazi za maendeleo na kutekeleza yafuatayo:-

23.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Chuo Cha Mafunzo kimepokea jumla ya wanafunzi 479. Kati ya hao, wanafunzi 462 ni wanaume na wanafunzi 17 ni wanawake. Idadi hii inaonesha kuongezeka kwa wanafunzi 17 waliopokelewa Chuoni hapo ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2010/2011 kama inavyoonekana katika Kiambatanisho Namba 11.

24.            Mheshimiwa Spika, Chuo Cha Mafunzo kimepokea jumla ya mahabusu 2,620, kati ya hao 2,510 ni wanaume na 110 ni Wanawake. Mahabusu 2,110 waliruhusiwa kwa dhamana na wengine kuachiliwa kwa kuonekana hawana hatia na waliobakia wanaendelea kusubiri hatma ya kesi zao. Makosa makubwa ya wanafunzi wanaoletwa chuoni ni kuua, wizi wa kutumia silaha, wizi wa mazao, shambulio, kubaka na kuvunja nyumba na kuiba. Hakuna mtu hata mmoja aliopo kizuizini kwa masuala ya kisiasa.

25.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Idara ya Chuo cha Mafunzo imetekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Imepima mashamba ya Hanyegwa Mchana na Kambi ya Kinumoshi na eneo la ujenzi wa gereza jipya Hanyegwa mchana.
b)       Imefanya matengenezo ya kuezeka Chuo cha Mafunzo cha Ubago.
c)       Imeendelea na ujenzi wa Bweni la kulala Wanafunzi Kinumoshi kwa kuweka madirisha 4 mapya na hatua ya plasta inaendelea.
d)       Vifaa vya kuezekea nyumba ya familia mbili Kangagani Pemba vimenunuliwa.
e)       Wanafunzi wote wamebadilishiwa kivazi kwa kushonewa sare za rangi ya machungwa.
f)        Imeimarisha huduma za chakula kwa wanafunzi na wanapata chakula cha kutosha kwa siku.
g)       Imelima Ekari 50 za mpunga, Ekari 100 za muhogo, Ekari 5 za Viazi vitamu na Ekari 25 za Mahindi katika mashamba yake ya Kengeja, Kangagani, Ubago, Tungamaa, Kinumoshi na Langoni.
h)       Imepitia Sera ya Idara na kutayarisha Mpango Mkakati kwa hatua ya awali.
i)         Mradi wa ujenzi wa Chuo kipya Cha Mafunzo umeshaanza kwa kusafisha eneo la ujenzi, kununua vifaa vya ujenzi ikiwa ni pamoja na mashine za kufyatulia matofali, dampa moja na kusogeza miundombinu karibu na eneo la ujenzi kama vile maji na umeme.

26.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ya Chuo cha Mafunzo Kimekusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Kuendelea kuyapima na kuyapatia hati miliki mashamba ya Chuo cha Mafunzo Ubago, Kengeja, Langoni, Tungamaa na Kangagani.
b)       Kuendelea na ujenzi wa Chuo cha Mafunzo cha Ubago, Bweni la Wanafunzi Kinumoshi na Bweni la Wanafunzi Kengeja.
c)       Kuanza Ujenzi wa Ofisi Kuu ya Chuo Cha Mafunzo Pemba na kuendelea na ujenzi wa Ofisi ya Zoni ya Mashamba Unguja.
d)       Kulima Ekari 50 za mpunga, Ekari 130 za muhogo, Ekari 3 mbaazi, Ekari 55 za mahindi na Ekari 3 za kilimo cha mbogamboga na kuendeleza kilimo cha Mikarafuu katika mashamba yake ya Kengeja, Kangagani, Ubago, Tungamaa, Kinumoshi, Langoni na Hanyengwa Mchana.
e)       Kuweka vyoo katika Mabweni ya kulala Wanafunzi katika Chuo cha Mafunzo cha Langoni.
f)        Kuanza ujenzi wa majengo ya Chuo kipya cha Mafunzo Hanyegwa Mchana.
g)       Kukamilisha Mpango Mkakati wa Idara ya Chuo cha Mafunzo.

27.            Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Chuo cha Mafunzo (MF) iweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 5,890 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS 400 milioni kwa ajili ya kazi za maendeleo.

 

KIKOSI CHA ZIMAMOTO NA UOKOZI ZANZIBAR (KZU)


28.            Mheshimiwa Spika, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kimeanzishwa kwa Sheria Namba 7 ya mwaka 99 na kina jukumu la kusimamia shughuli zote za uzimaji moto na uokozi wa maisha na mali za watu. Vile vile kikosi kina jukumu la kutoa huduma za zimamoto kwenye viwanja vya ndege vya Unguja na Pemba. Aidha, Kikosi kinatoa ushauri wa kujinga na moto kwa wananchi, Taasisi za Serikali na za watu binafsi.
29.            Mheshimiwa Spika, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi (KZU), kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kiliidhinishiwa TZS 1,883 milioni kwa kazi za kawaida na hadi kufikia mwezi Machi 2012, Kikosi kiliingiziwa TZS 1,869 milioni sawa na asilimia 99.3 ya makadirio ya matumizi ya kawaida na kutekeleza yafuatayo:-

a)       Kikosi kimenunua gari mbili za kisasa za kuzimia moto na gari moja limepelekwa Pemba. Vile vile, vifaa vya aina mbali mbali vimepatikana kwa upande wa Unguja na Pemba.
b)       Mawasiliano ndani ya Kikosi yameimarika kwa kununua redio mpya 4, kufanyia matengenezo mbali mbali ya redio zilizopo Kikosini na Uwanja wa Ndege.
c)       Kikosi kimesafisha na kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mapumziko Chanjaani Pemba.
d)       Kikosi kimejenga banda la kuweka gari za kuzimia moto katika Kituo cha Mwanakwerekwe.
e)       Kikosi kimejenga nyumba ya vyumba vinne katika kituo cha Kigunda na kutia sakafu, plasta na sehemu ya mapokezi imewekwa dari.
f)        Kikosi kimenunua mabati kwa ajili kuezekea Kituo cha Zimamoto Kitogani.
g)       Kikosi kimejenga hodhi la kuhifadhia maji katika kituo cha Chanjaani.
h)       Kikosi kinaendelea na ujenzi wa uzio wa Kituo cha Mahonda.
i)         Kikosi kimenunua vifaa na samani kwa vituo vyake vya Unguja na Pemba.
j)         Kikosi kimewapatia Maofisa na Askari sare na vifaa vya kazi.
k)       Maafisa watatu wamehudhuria mafunzo nchini Singapore, maafisa 6 fani ya uhasibu, 11 mafunzo ufundi, watatu shahada ya sheria, wanne fani ya uboharia na manunuzi, 30 mafunzo ya uongozi mkubwa na 35  mafunzo ya uongozi mdogo
l)         Elimu imetolewa kwa njia ya redio na TV ambapo jumla ya vipindi 36 vilirushwa hewani. Aidha, vipeperushi juu ya kujikinga na majanga ya moto vimetengenezwa na maonesho ya utumiaji wa kifaa cha kuzimia moto kinachoitwa “Dry Sprinkler Power Aerosal” (DSPA) yamefanyika kwa Taasisi mbali mbali za binafsi na Serikali.

30.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Kikosi kimekusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Kuendelea kununua vifaa na gari za kutoa huduma za kuzima moto na uokozi.
b)       Kuimarisha mawasiliano ya uhakika ndani ya Kikosi.
c)       Kundelea kufanya matengenezo ya majengo na kujenga vituo vipya katika maeneo mapya.
d)       Kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi.
e)       Kuboresha huduma za kiutawala na michezo.
f)        Kukuza uwezo wa kiutendaji kwa Maafisa na wapiganaji kwa kuwapatia mafunzo ndani na nje ya nchi.
g)       Kuongeza uhusiano na mashirikiano ya namna ya kukabiliana na majanga mbali mbali kitaifa na kimataifa
h)       Kukuza uwelewa kwa wananchi, Taasisi za serikali, sekta binafsi, ili kuchukua hatua za tahadhari ya kujikinga na majanga ya moto.

31.            Mheshimiwa Spika, ili Kikosi cha Zimamoto na Uokozi (KZU) kiweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 3,099 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.

 

KIKOSI CHA VALANTIA ZANZIBAR (KVZ)


32.            Mheshimiwa Spika, Kikosi cha Valantia kimeanzishwa kwa Sheria Namba 5 ya mwaka 2004 na kina majukumu ya kutoa ulinzi kwa kushirikiana na Vikosi vya ulinzi na usalama vya SMT na SMZ, kusaidia kulinda raia na mali zao, kutekeleza shughuli za kijeshi kwa wakati wa dharura..

33.            Mheshimiwa Spika, Kikosi cha Valantia (KVZ), kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kiliingiziwa TZS 2,452 milioni kwa kazi za kawaida na TZS 100 kwa kazi za maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi 2012, Kikosi kiliingiziwa TZS 2,086.7 milioni sawa na asilimia 85.1 ya makadirio ya matumizi ya kawaida na TZS 50 milioni sawa na asilimia 50 kwa matumizi ya kazi za maendeleo na kutekeleza yafuatayo:-

a)       Kikosi kimeshiriki katika majukumu ya ulinzi na shughuli za uokozi kwa kushirikiana na vikosi vya SMT na SMZ.
b)       Kimewapatia elimu wapiganaji wake 13 katika fani za udaktari, uhasibu, mawasiliano ya redio, manunuzi na ugavi, utawala wa umma, TEKNOHAMA, utunzaji wa kumbukumbu, raslimali watu na mafunzo ya ufundi ndani na nje ya Zanzibar.
c)       Kikosi kimewapatia elimu ya ushauri nasaha juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI wapiganaji wake wote Unguja na Pemba.
d)       Kikosi kimewapatia sare Wapiganaji wake kwa kushonewa sare 500 na nyengine zinaendelea kushonwa katika kiwanda cha Ushoni cha Idara Maalumu za SMZ.
e)       Kikosi kimeendelea kuyafanyia matengenezo ya vibanda vitatu vya walinzi Makao Makuu Mtoni, matengenezo ya Kambi ya Kisakasaka na matengenezo ya Kambi ya Pangatupu kwa Unguja. Kwa upande wa Pemba Kikosi kimefanya matengenezo katika Kambi ya Ndugukitu.
f)        Kikosi kimeyapatia hatimiliki maeneo mawili (Kambi ya Mtoni na Kambi ya Micheweni) na maeneo yaliyobakia taratibu za kupatiwa hatimiliki zinaendelea.
g)       Kikosi kimekamilisha ujenzi wa jengo la Makao Makuu na ujenzi wa ghala la kuhifadhia vifaa uko katika hatua za mwisho.
34.            Mheshimiwa Spika, pamoja na kutimiza majukumu hayo iliyojipangia pia Kikosi cha Valantia Kwa kushirikana na vikosi vyengine kimeweza kushiriki katika operasheni karafuu kisiwani Pemba katika msimu huu wa karafuu uliomalizika hivi karibuni.

35.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013 Kikosi cha Valantia kitatekeleza malengo yafuatayo:-

a)       Kuimarisha nguvu za ulinzi na usalama.
b)       Kuwaongezea uwezo wa kiutendaji kwa kuwapatia elimu Wapiganaji kwa kozi mbalimbali ndani na nje ya kikosi.
c)       Kuweka mazingira mazuri ya kazi ikiwemo ununuzi wa gari.
d)       Kuendelea kuwapatia sare na vifaa vya ulinzi wapiganaji wote wa Kikosi.
e)       Kutengeneza majengo ya kikosi na kuendelea kuyapatia hatimiliki maeneo ya kikosi Unguja na Pemba.
f)        Kuendeleza ujenzi wa jengo la Makao Makuu yakiwemo ujenzi wa mesi na ujenzi wa ukumbi wa mkutano.

36.            Mheshimiwa Spika, ili Kikosi cha Valantia kiweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 3,784 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS 100 milioni kwa matumizi ya kazi za maendeleo.

JUMLA YA MATUMIZI YA OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013


37.            Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo juu ya utekelezaji wa malengo ya Idara na Taasisi zote zilizo chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, sasa kwa ruhusa yako naomba kutoa maelezo ya muhutasari wa maombi ya fedha kwa mwaka 2011/2012 na jumla ya matumizi hadi kufikia Machi 2012 na maombi ya fedha kwa mwaka 2012/2013.

38.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2012, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ilikadiriwa kutumia TZS 34,176.5 milioni. Kati ya hizo TZS 30,435.5 milioni kwa kazi za kawaida, TZS 1,930 milioni kwa kazi za maendeleo na TZS 1,811.0 milioni kwa ajili ya ruzuku za Baraza la Manispaa na Mabaraza ya Miji ya Mkoani, Chake Chake na Wete. Hadi kufikia Machi 2012, Ofisi imeingiziwa TZS  26,570.8 milioni sawa na asilimia 87.3 kwa kazi za kawaida, TZS 1,477.3 milioni sawa na asilimia 76.6 kwa kazi za maendeleo na TZS 1,381.7 milioni sawa na asilimia 76.3 za ruzuku.

39.            Mheshimiwa Spika, ili Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi iweze kutekeleza malengo na majukumu yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, inaomba kuidhinishiwa jumla ya TZS 50,698.1 milioni. Kati ya hizo, TZS 46,654.1 milioni kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida, TZS 1,906.0 milioni kwa matumizi ya kazi za maendeleo na TZS 2,138 milioni ni ruzuku kwa Baraza la Manispaa na Mabaraza ya Miji (Mabaraza ya Miji ya Mkoani, Chake Chake na Wete). 

40.            Mheshimiwa Spika, maelezo ya uchambuzi wa kina wa fedha zilizoombwa kwa mwaka 2011/2012, fedha zilizopatikana hadi mwezi Machi 2012, asilimia ya fedha zilizopatikana hadi mwezi Machi 2012 na makisio ya bajeti kwa mwaka 2012/2013 kwa kila Idara zimeoneshwa katika Viambatanisho Namba 12, 13 na 14. Aidha, Kiambatanisho Namba 15 kinatoa uchambuzi wa makushanyo ya fedha kutoka katika vyanzo vyao vya mapato ya Baraza la Manispaa, Mabaraza ya Miji ya Mkoani, Chake Chake na Wete na Halmashauri 9 za Wilaya.

HITIMISHO


41.            Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia hotuba hii, naomba kuchukua fursa nyengine kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wake makini wa kusimamia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kuendelea kunipa dhamana ya kuiongoza Ofisi hii. Aidha, natoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi wa Zanzibar kwa kuendeleza hali ya amani na utulivu iliyopo, kabisa tusiichezee. Natoa wito kwa wananchi kuendelea kuheshimu Sheria za nchi tulizoziweka wenyewe kwa lengo la kujenga mustakbali mwema wa maendeleo ya nchi yetu.

42.            Mheshimiwa Spika, mwisho, nawashukuru viongozi, watendaji na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa ushirikiano wao wa karibu wanaoendelea kunipa kila siku katika kutekeleza kazi zetu. Nawashukuru wote kwa kunisikiliza kwa makini wakati wote na natanguliza shukrani zangu kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili Tukufu kwa michango mtakayoitoa katika kujadili hotuba ya bajeti hii.

43.            Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.






(Dkt. Mwinyihaji Makame)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.